bayyinaat

Published time: 06 ,October ,2017      11:48:27
Je! Wajifakharisha kuwa kwako mwanamke mwenye sifa ya pekee ya uanamke? Lakini tambua kuwa mwanamke na sifa zake, atakapokwenda kinyume nazo basi atapoteza sifa ya......
News ID: 101

Je! Wajifakharisha kuwa kwako mwanamke mwenye sifa ya pekee ya uanamke? Lakini tambua kuwa mwanamke na sifa zake, atakapokwenda kinyume nazo basi atapoteza sifa ya uanamke wake, na katu hazitarudi sifa hizo ambazo humtambulisha mwanamke na kumpamba katika macho ya mwanaume.

Sifa za mwanamke ni nyingi, na ambazo humtoa kasoro katika sifa hizo ni hizi zifuatazo:

1. JIKE DUME: Ni mwanamke anayejiweka katika mazingira ya udume na kujisahau kuwa asili yake ni uanamke. Na mwishoe kusimamia sifa ambazo si zake ili kujithibitishia nguvu/ ubabe.

2. MWINGI WA MANENO: Ni yule ambaye hamuachii mwingine nafasi ya kuongea ili kutaka kujitetea hata akiwa katika kosa, na ili achukue nafasi na dauru za watu wote. Hakika mwanamke wa aina hii huvumilika kwa muda mfupi sana, kwani yu karibuni kutengwa kwani ni jambo lisilowezekana kuishi pamoja nae.

3. MWANAMKE MCHEZA SHERE: Ni yule ambaye hupambika kwa sifa za uongo, usaliti na kujitenga mbali na ndugu zake na pia ndugu wa mume wake. Kwa hakika ni mwanamke mwenye kuibua hisia ili kuvutia kamba ya ushabiki upande wake kwa mara ya kwanza, ambapo yeye ni haraka mno kuwa kiherehere na hatimaye kumfanya mwanaume kujitenga mbali nae.

4. MWANAMKE ANAYEZEMBEA DHAHIRI YAKE NA KUJIONYESHA KATIKA MAZINGIRA YA HOVYO KILA KONA NA KILA NYAKATI: Ni mwanamke ambaye wakati wote hutokwa na harufu ya moshi, na mavazi ya kulalia (night dress) ndio mapambo yake ya msingi, hupuuzia mandhari yake na uzuri wake, na mwanamke huyo hakika mwanaume hamuangalii jicho la pili.

5. MWANAMKE MJINGA NA JAHILI: Asiyekuwa na la kusema wala mtazamo katika lile lililozungumzwa, maongezi yake ni upuuzi na ujinga wake hauna mpaka. Mwanamke huyu huhesabika kuwa ni (mwanamke) hasi katika jamii na katika familia pia, hakika ni mapema kupuuzwa, atapoteza sifa ya uanamke wake na hatimae kumfanya mwanaume kumkimbia kwa kutoendana nae kisifa n.k

6. MWANAMKE ANAYEJISHEMBENDUA: Ni mwanamke anayedhani kuwa yeye ni mwerevu na mjanja zaidi kuliko mume wake na kudhani kuwa ni bora zaidi kuliko wengine. Au kudai kuwa mumewe ni bora Zaidi na wanawe kuwa ni wazuri Zaidi na nyumba yake n kubwa mno kuliko (nyumba) za wengine na mavazi yake ni yenye mvuto Zaidi kuliko ya wengine… ewe mwanamke usitambulishe uliyo nayo kwa wengine, na wala usijifakharishe kwa kitu kilichokuwa ndani ya nyumba yako na maisha yako kwa wangine.

7. MWANAMKE MBABE KWA MUMEWE: Ni mwanamke ambaye hujaribu kumlazimisha mumewe kutenda kila atakalo… ni mwanamke ambaye hathamini maneno ya mume wake wala kutilia maanani mawazo yake. Na ni mwanamke anayetaka usawa na mume wake kila siku. Hufuatilia kwa siri nyenzo zake, makosa yake. Huzungumzia makosa yake (mume) mbele ya rafiki zake (shoga zake) na hata familia yake pia.

8. MWANAMKE ANAYEONYESHA UZURI WAKE KILA WAKATI: Kama vile mwanamitindo na mrembo wa dunia. Huyo pia huenda huwavutia watu wengine uzuri wake na kupelekea kumtamani, lakini pamoja na muda unavyozidi kwenda mbele atadharaulika na kukosa uaminifu na Amani pia.

9. MWANAMKE ANAYEJARIBU KUCHAFUA SIFA ZA UZURI WA WANAWAKE WENGINE: Mwanamke yeyote kwake ni adui na hasimu. Utakuta ni msimbuliaji wa ubaya wa wanawake wengine ambapo yeye ni mbaya zaidi wa sifa na tabia kuliko wao.

10. MWANAMKE MCHAFU WA TABIA: Ni yule ambaye anayependa matanuzi na mtumiaji vibaya wa mali za mume wake. Na mwenye tamaa ya mali. Huwa mbali na maamuzi ya mume yeye kama mwanamke. Na hatofautishi kati ya matumizi yake mabaya ya kifedha au kimwili, na huyo ni mwanamke ambaye humfanya mwanaume kumchukia haraka mno na kupoteza hisia za kimapenzi kwake.

11. MWANAMKE MCHAFU: Ni mwanamke asiyezingatia usafi wake na namna ya kujiweka kwa mume wake, anayemfanya mumewe kumtazama kama ndoto ya fadhaa inayompelekea kumkimbia. Hakika usafi ni alama kubwa ya mwanamke kwa mwanaume isiyoweza kupingika, na kutoweka kwake ni sawa na kuanguka nguzo ya uanamke na kumbadilisha mwanamke kuwa ni kiumbe asiyekuwa na thamani isiyo na mpaka wowote kwa mume.

12. MWANAMKE MWENYE HISIA KALI NA MWINGI WA KUJILIZA: Mwanamke ambaye huamsha hisia za mume wake tokea awali ili kumsumbua kila anapojisikia kutaka jambo. Na tabia hiyo kubadilika kuwa ni chimbuko la kero na adha kwake, kwa sababu (humfanya mwanaume huyo) kupumbazika kutokana na hisia za mke wake pindi awapo pamoja nae, na kuogopa kufanya jambo au kusema neno ambalo litaudhi hisia zake.

Imeletwa kwenu na:

Ndg: Juma. R. Kazingati


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: