Kwa kuzingatia kwamba, familia ina
nafasi muhimu katika saada na kutengemaa au nakama, ihlaki na kuharibika watu
katika kila jamii, Uislamu umetilia mkazo maalumu juu ya suala la ndoa na
kujenga familia, na ukaweka vigezo vya tabia na maadili katika suala zima la
kuchagua mke. Ndoa yenye saada na mafanikio ni ile ambayo misingi yake
imesimama kwa ajili ya kuunda familia salama, imara na yenye nishati,
uchangamfu na bashasha. Kwa hakika mwanadamu ni majumuu yenye
vipaji tele na uwezo tayarifu na hivyo ndoa inaweza kuandaa mazingira mwafaka
kwa ajili ya kustawi na kuchanua vipaji vilivyojificha katika ujudi na uwepo wa
mwanadamu huyu na dafina iliyoko katika kila ujudi wa ndani wa mtu. Mapenzi,
kudhamini hawaiji za maisha, usimamizi wa familia, mamlaka, kujitosheleza,
kupigania ukamilifu, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuwalea watu wema na
wastahiki ni mambo ambayo yanawezekana kupatikana kwa kuweko ndoa. Miongoni mwa
nukta muhimu katika maktaba ya malezi ya Mtume SAW, masahaba wema na dhuria
wake (watu wa nyumba yake tukufu yaani Ahlul-Beit), ni mtazamo wao wa kimaanawi
kuhusiana na suala la ndoa na upande wa utukufu wake. Ibara tunazozishuhudia
katika hadithi zinathibitisha hili kwa njia tofauti. Miongoni mwa hadithi hizo
ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume SAW akisema:
من تزوج فقد احرز نصف دينه فليتق الله في النصف الباقي
"Mwenye kufunga ndoa
amekamilisha nusu ya dini yake, basi na amche Allah katika nusu iliyobakia."
Au hadithi isemayo:
"Miongoni mwa nyakati za
kushuka rehma za Mwenyezi Mungu ni wakati wa shughuli ya akidi, nikaha na
kufunga ndoa."
Vile vile kuna hadithi nyingi ambazo
zinaonesha kuwa, akthari ya miamala ya kifamilia inahesabiwa kuwa sawa na
kufanya ibada. Mtume SAW amenukuliwa akisema kwamba:
"Mwanaume anayefanya bidii
kwa ajili ya familia yake, ni sawa na mujahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu."
Katika hadithi nyingine Mtume SAW amesema:
جهاد المرأه حسن التبعّل
"Jihadi ya mwanamke ni kuwa na
mwenendo mwema kwa mume."
Kwa hakika ibara zote hizi zinaonesha
jinsi Uislamu unavyoshajiisha juu ya suala la ndoa. Vile vile kunajitokeza
uhakika huu kwamba, masuala ya maisha ya dunia yanaweza kuwa njia ya kuelekea
katika ukamilifu wa kimaanawi na kiakhera. Miongoni mwa athari za kisaikolojia
za ndoa, ni kuathiriana pakubwa mume na mke. Kila mmoja yaani mke na mume
huathirika pakubwa na miamala, fikra na hata mtazamo wa mwenzake. Ni kwa
kuzingatia uhakika huo, ndio maana maktaba ya kimalezi ya Mtume SAW, masahaba
wema na dhuria wake ikakakoteza na kutilia mkazo juu ya kuzingatia suala la
kuchagua mume au mke kabla ya kuoa au kuolewa na kuzingatia zaidi suala la
thamani za kiakhlaqi na kimaadili.
Sababu ya jamii kuporomoka
kimaadili katika ulimwengu wa Magharibi?
Hii leo mmonyoko uliokithiri wa
kimaadili katika jamii za Kimagharibi chimbuko lake ni wanajamii kuweka kando
mafundisho sahihi ya dini hasa kuhusiana na suala la ndoa. Si hivyo tu, Wamagharibi
wamechupa mipaka na kuanza kutambulisha ndoa ambazo zinakinzana kabisa hata na
maumbile ya mwanadamu. Tunashuhudia hii leo katika ulimwengu wa Magharibi
kukieneza ndoa za watu wa jinsia moja, yaani ndoa baina ya mwanaume na mwanaume
(usenge na ushoga) au baina ya mwanamke na mwanamke (usagaji), kitendo ambacho
kimsingi sio ndoa na wala haifai kuita mafungamano hayo kuwa ni ndoa, bali ni
uchafu ambao jina lake hasa ni usenge, liwati na usagaji. Nukta ya kutilia
maanani hapa ni kwamba, dini zote na madhehebu zote zinavitambua vitendo cha
usenge, ushoga, liwati na usagaji kuwa ni dhambi kubwa na kinyume kabisa na
maumbile ya mwanadamu na zinawaonya wanadamu kujihusisha na vitendo hivyo.
Itaendelea…
Na Salum Bendera