Mpenzi msomaji, katika sehemu ya
kwanza na ya pili za makala hii ya "Ndoa, Msingi wa Kujenga Familia",
tuliashiria mambo kadhaa likiwemo suala la umuhimu wa ndoa katika jamii.
Tulisema kuwa, ndoa ni jiwe la kwanza la msingi la kujenga familia, na familia
ni taasisi kuu ya jamii. Tulizungumzia japo kwa muhtasari pia jinsi dini za
mbinguni zilivyoshajiisha na kulipa umuhimu suala la ndoa na kueleza kwamba,
Uislamu ndio dini iliyoko mstari wa mbele katika hili ambapo umeweka sharia,
misingi na hata vigezo vya kuoa. Kadhalika tulitupia jicho matatizo na chimbuko
la kuporomoka jamii katika ulimwengu wa Magharibi na kuona jinsi suala la ndoa
lilivyo na umuhimu katika kujenga, kulinda na kuimarisha familia.
Ifuatayo ni sehemu ya pili na ya
mwisho ya Makala hii.
Matatizo ya ulimwengu wa
Magharibi
Tab'an, hii leo ulimwengu wa
Magharibi unakabiliwa na tatizo jingine nalo ni maisha ya kuweko mzazi mmoja
kila familia. Yaani baadhi ya familia zina baba tu au mama tu na hivyo kupelekea
kuweko hali ya kulegalega ndani ya familia hizo. Hii leo kuna nchi nyingi
barani Ulaya ambapo asilimia 50 hadi 80 ya watoto wamezaliwa nje ya ndoa.
Ufaransa na nchi za Scandinavia ni miongoni mwa nchi hizo. Katika kipindi cha
maisha yao yote, watoto hawa huishi na mzazi mmoja au kutoishi na wazazi wao
wote wawili kutokana na kulelewa katika vituo maalumu vya malezi ya watoto.
Utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa, watoto wanaozaliwa katika familia na
kukulia humo huwa wazima zaidi kimwili, kiafya na kisaikolojia na wakiwa shuleni
au sehemu za kazi huwa na mahusiano bora, huishi maisha marefu na ni wenye
furaha na bashasha ikilinganishwa na watoto ambao wamezaliwa nje ya familia.
Kwa hakika ndoa ambayo wanandoa wake wamechaguana kwa kuzingatia masuala ya
kimaanawi na maadili mema huwaandalia uwanja wa ukamilifu na saada ya dunia na
akhera. Mtume SAW alifanya juhudi kubwa kueneza utukufu wa ndoa baina ya watu.
Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana Bwana Mtume SAW amenukuliwa katika
hadithi mashuhuri akisema:
النكاح من سنتي فمن رغب عن سنتي فليس مني
Ndoa ni katika sunna yangu na mwenye
kutenda kinyume na sunna yangu si katika mimi." Au hadithi hii iliyonukuliwa
kutoka kwa Imam Jafar Sadiq (AS) mmoja wa wajukuu wa Mtume SAW inayosema:
رَکعَتانِ یُصَلّیهِما المتزوج افضل من سيعين ركعة يصليها اعزب
"Rakaa mbili (anazoswali) za
mwenye kuoa ni bora (zenye thamani kubwa) kuliko rakaa sabini za kapera (mtu ambaye hajaoa.)"
Mtazamo wa Uislamu juu ya
vigezo vya ndoa
Katika mtazamo wa Mtume SAW na dhuria
wake wema ni kuwa, endapo mke na mume watakuwa na sifa tatu za elimu, ustadi na
tabia njema wanaweza kuiongoza na kuisimamia nyumba na familia kwa njia bora
kabisa. Katika familia kama hii, mwanaume atakuwa kiongozi laiki, mstahiki,
mwenye hima na mpole. Atadhamini mahitaji ya familia yake kwa njia za halali.
Kwa msingi huo atakuwa mume mwema na mwenye mapenzi kwa familia yake. Uongozi
na usimamizi wake kwa familia yake hautakuwa na misingi ya kutaka kutawala na
utumiaji mabavu. Atakuwa mwanaume mwenye kuihami na kulinda familia yake na
atakuwa ni mwenye kufanya jitihada kwa ajili ya kutoa miongozo na himaya kwa
familia yake na bila shaka atawashajiisha wanafamilia kuelekea upande wa
masuala ya kimaanawi. Nafasi ya mwanamke pia katika familia ina umuhimu mkubwa
mno.
Jukumu muhimu la mke ndani ya
nyumba
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu,
jukumu muhimu la mwanamke ndani ya nyumba baada ya kutekeleza taklifu za kidini
ni kumkidhia mumewe haja za kindoa. Subira na ustahamilivu wa mwanamke na kuwa
pamoja na mumewe katika dhiki na faraja, katika matatizo ya kijamii na kiuchumi
na vile vile kutokuwa na matarajio yaliyo nje ya uwezo wa mumewe ni mambo
ambayo yanaweza kuandaa uwanja mwafaka wa kuweko uhusiano mwema, mzuri na
unaofaa baina ya mume na mke; uhusiano ambao bila shaka utaimarisha pendo lao
na kuizatiti ndoa yao. Katika upande mwingine, mwanamke ni kituo cha huba na
mapenzi katika familia na jukumu la kuwalea watoto wema, wastahiki na wenye
imani liko katika mabega yake kabla ya mtu mwingine yeyote yule.
Wabillah Tawfiki,
Na Salum Bendera