bayyinaat

Published time: 05 ,December ,2017      12:31:41
Kwa ufupi tunaweza kusema kwamba, kuna njia kuu mbili za kuweza kutolea hukumu jambo fulani, au Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika hali ya kuweka sheria fulani basi wanaweza kutumia moja ya njia mbili zifuatazo..........
News ID: 145

2. Je, Kusherehekea mazazi ya Mtume (saww) ni Bidaa?

Ili tuweze kupata jibu sahihi la swali hili itatubidi kwanza tuelezee ni wakati gani jambo linakuwa ni Bidaa au linakuwa ni ndani ya dini.

Kwa ufupi tunaweza kusema kwamba, kuna njia kuu mbili za kuweza kutolea hukumu jambo fulani, au Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika hali ya kuweka sheria fulani basi wanaweza kutumia moja ya njia mbili zifuatazo.

Moja ni Mwenyezi Mungu au Mtume wake akaweka tamko mahususi kunako kadhia fulani, kama vile ambavyo imekuja kunako kusherehekea masiku ya Eidul Fitr na Adh-ha, ambapo hapa hakuna anayesema kwamba ni Bidaa kwakuwa tu kuna matamko na sheria mahususi zinazohusu masiku haya.

Ama njia ya pili ni kwamba Mwenyezi Mungu au Mtume wake hawatoi tamko mahususi kuhusiana na kila tukio, bali wanaweka misingi ambayo Waislamu ndio watakaokuja kuhusisha matukio na misingi ile, ikiwa itaoana basi itakuwa ni ndani ya sheria, na endapo haitooana basi itakuwa ni nje ya sheria. N ahapa tuna mifano kadhaa katika kuthibitisha jambo hili:

1. Jambo la kujifunza na kwenda shule, ambapo ukichunguza utakuta kwamba jambo hili lina namna na njia mbalimbali ambazo zinabadilika kutokana na kubadilika kwa zama, zamani walikuwa wakiandika katika magome kwa kutumia labda manyoya ya ndege, lakini siku hizi mambo si hivyo tena bali kuna njia za kisasa katika uwanja huo. Hivyo unakuta kwamba Mungu yeye alichofanya ni kuamrisha tu watu wajifunze, lakini namna gani na wao wenyewe waangalie kutokana zama na maslahi ya nyakati husika. Isipokuwa tu ni kwa misingi ambayo haitatoka katika mafundisho ya Kiislamu.

2. Masahaba baada ya kufariki dunia bwana Mtume walisimama kidete katika swala zima la kukusanya Quran, lakini hakuna hata mmoja ambaye atasimama leo hii na kusema kwamba jambo hili ni bidaa, kwanini?, ni kwamba jambo hili la masahaba linakusanywa na kauli ya au msingi wa Kiislamu wa umuhimu wa kuhifadhi kitabu hiki kitukufu.

3. Swala la kuulinda na kuuhifadhi Uislamu, ni katika mambo ambayo hutokuta kwamba Mungu kawaaambia Waislamu kwamba fanyeni jambo fulani na fulani ili muweze kuwa na Nguvu ya kujilinda, bali unakuta kuna msingi mmoja tu ambapo anasema ".....Na waandalieni nguvu kwa namna muwezavyo....”[1] ama namna gani mtaweza kuziandaa nguvu hizo ni juu ya yenu Waislamu laini kwa kulinda misingi sahihi na mafunzo sahihi ya Uislamu.

Hii ni mifano katika kutaka kubainisha tu kwamba sio kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu au Mtume wake hakuweka neno mahususi juu yake basi tuseme kwamba ni bidaa, bali ni lazima kwanza tuangalie kwamba je, pamoja na kwamba jambo hili halina tamko mahususi, kuna asili au msingi wowote katika dini ambao unaweza kukusanya jambo hili?, hapo ndipo tutaweza kuhukumu kwamba jambo husika ni bidaa au la.

Ngoja tuongeze na maneno ya Maulama katika kufasiri maana ya Bidaa kisha tuone usahihi wa mambo:

1. Ibn Rajab anasema "....Mtume (saww) aliposema "Jiepusheni na uzushi, kwani kila uzushi ni upotevu”, alikuw ana maana ya kuhadharisha umma juu ya kufuata uzushi, na kisha akatilia mkazo kwamba kila uzushi ni upotevu, ila uzushi maana yake ni jambo ambalo limezuliwa katika dini na likawa halina tamko au msingi katika dini hiyo, n akuhusu mambo ambayo yanakuwa na misingi katika dini si bidaa wala uzushi, japokuwa kilugha unaweza kusema hivyo...”.

Naam, kilugha unaweza kuita kila jambo ambalo limetokea katika dini kwamba ni bidaa, maana Bidaa kilugha ni kila jambo ambalo halikuwepo zama fulani n a likaja likazuka baada yake. Ila sasa utakapokuja katika matumizi ya Istilahi (Matumizi maalumu ya neno katika sehemu maalumu), huwezi kuita jambo Bidaa mpaka yatakapotimia masharti yake, ambapo moja ya masharti hayo ni kwamba jambo hilo lisiwe na msingi katika dini.

2. Imepokelewa katika sahih Muslim kutoka kwa Jabir (ra), kutoka kwa Mtume (saww) kwamba alikuwa akisema katika hotuba zake "......Kwa hakika maneno bora hasa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu, na Mwongozo bora hasa ni mwongozo wa Mtume (saww), na mambo mabaya hasa ni mambo ya kuzushwa (Bidaa), kwani kila lenye kuzushwa basi ni upotevu.......”. kisha Jabir akasema "....Maneno yake aliposema kwamba kila lenye kuzushwa huwa ni upotevu, imekusanya mambo mengi mno, nao ni msingi mkubwa sana katika misingi ya dini yetu, n a hufanana hasa na maneno yake pale aliposema "....Mwenye kuzusha jambo katika dini na likawa halina asili basi si katika sisi”, kwa maana ya kwamba kila mwenye kuzusha jambo n a kisha akalinasibisha na dini hali ya kuwa halina asili wala msingi katika dini basi si katika watu wa Mtume (saww).[2]

3. Pia Ibn Hajar katika kufafanua hadithi isemayo "...Hakika maneno hasa ni maneno ya Mungu........ na mambo mabaya hasa ni mambo ya kuzushwa (Bidaa).....” anasema "...neno "mambo ya kuzushwa au Bidaa” maana yake ni jambo ambalo limezushwa n alikawa halina asili wala msingi katika dini, hivyo endapo jambo litakuwa na msingi katika dini basi si Bidaa, kwa sababu kisheria Bidaa ni mbaya japokuwa kilugha haitakuwa hivyo, kwani katika lugha kila jambo ambalo litazushwa na likawa halina mfano wake hapo kabla huitwa Bidaa, sawa sawa liwe jambo zuri au baya.....”.[3]

Hii ni mifano na baadhi ya maneno ya maulama katika kuelezea ni wakati gani tunaweza sema jambo fulani ni Bidaa na wakati gani tunatakiwa kusema kwamba jambo hili si bidaa, kiufupi ni kwamba endapo jambo litakuwa sawa halina hukumu yake mahususi, lakini ikawa kuna msingi maalumu ambao unakusanya pia jambo hilo kama moja ya vipengele vyake, basi jambo hilo si Bidaa kabisa.

Sasa hapa ndipo ambapo tunakutana na jambo la muhimu, nalo ni kwamba je, swala la kuadhimisha au kudumisha kumsifu Mtume (saww) lina msingi katika dini mpaka tuseme kwamba jambo hili si Bidaa?.

Usikose sehemu ya tatu ya makala hii......



[1] An-fal 60

[2] Jawamiul ulumil wal hikam 226

[3] Fathul Bari juz 13 Sharhi hadithi ya 7277


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: