bayyinaat

Published time: 05 ,December ,2017      20:15:56
Historia ya Kiislamu inaonyesha wazi kuwa kila mara Waislamu wa madhehebu tofauti wanapochukua uamuzi wa kuungana na kushirikiana katika ngome moja dhidi ya adui, jamii ya Kiislamu huwa ni tukufu na yenye nguvu na maadui kuwa dhaifu, lakini........
News ID: 147

Uislamu umeufanya umoja kuwa jambo la wajibu na lazima miongoni mwa Waislamu na waumini na dini nyinginezo za mbinguni zinazomwamini Mwenyezi Mungu Mmoja. Uzito wa jambo hili unaonekana wazi katika aya za Qur'ani Tukufu na riwaya zilizopokelewa kutoka kwa Maimamu Maasumu (as). Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 103 ya Surat Aal Imran kitabu hicho kitakatifu:
وَاعتَصِموا بِحَبلِ اللَّهِ جَميعًا وَلا تَفَرَّقوا ۚ وَاذكُروا نِعمَتَ اللَّهِ عَلَيكُم إِذ كُنتُم أَعداءً فَأَلَّفَ بَينَ قُلوبِكُم فَأَصبَحتُم بِنِعمَتِهِ إِخوانًا 
Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu.

Historia ya Kiislamu inaonyesha wazi kuwa kila mara Waislamu wa madhehebu tofauti wanapochukua uamuzi wa kuungana na kushirikiana katika ngome moja dhidi ya adui, jamii ya Kiislamu huwa ni tukufu na yenye nguvu na maadui kuwa dhaifu, lakini Waislamu wanapoghafilika na kusahau amri hiyo muhimu ya Mwenyezi Mungu, hukabiliwa na misiba mingi ukiwemo wa kudhibitiwa na maadui na kuhatarishwa kizazi na jamii nzima ya Kiislamu.
 Qur'ani Tukufu inasema katika aya ya 46 ya Surat al- Anfaal: 
وَأَطيعُوا اللَّهَ وَرَسولَهُ وَلا تَنازَعوا فَتَفشَلوا وَتَذهَبَ ريحُكُم
Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. 
Suala la mfarakano baina ya Waislamu ambalo linatajwa kama sababu kuu ya kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kiislamu, siku zote limekuwa moja ya mambo yanayozishughulisha mno bongo za wanafikra, warekebishaji umma pamoja na wanasiasa wa Ulimwengu wa Kiislamu. Warekebishaji umma wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu wanaamini kuwa kujiweka mbali Waislamu na tunu na thamani za asili za Kiislamu na badala yake kufufua taasubi na ukereketwa wa kikaumu, kikabila na wa asili za watu wa zama za ujahilia, ndio sababu kuu ya mfarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Asili ya Wiki ya Umoja
Tumo katika siku za kukumbuka maulidi ya Mtume SAW, mbora wa viumbe na shakhsia ambaye ndiye chanzo na chimbuko la umoja katika vipindi vyote vya historia ya Uislamu. Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW ndiye dira ya hisia na itikadi za umma wa Kiislamu. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia. 
Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Kishia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla. 

Moja ya mambo hatari na tishio kubwa kwa jamii ya Kiislamu hii leo ambayo katika kipindi cha karne kadhaa zilizopita yamepelekea kutokea madhara na pigo kwa umma wa Kiislamu ni hitilafu na mifarakano na hatua za maadui wa Uislamu za kuzikuza na kuzishikia bango hitilafu ndogo ndogo zilizoko baina ya Waislamu. Kuitwa kipindi hiki cha baina ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiul Awwal kuwa Wiki ya Umoja, lengo lake ni kutaka kuonyesha kwamba, licha ya Waislamu kuwa na hitilafu katika baadhi ya masuala ya kihistoria na kifikihi lakini ni umma mmoja. 

Nini makusudio ya Umoja wa Kiislamu?
Kabla ya kueleza umoja baina ya Waislamu umepewa nafasi gani katika aya za Qur'ani tukufu ni vyema kwanza tukalitolea jibu swali hili, kwamba tunapozungumzia umoja baina ya Waislamu tunakusudia umoja wa jambo gani na wa aina ipi?  Kuna rai mbili zilizotolewa katika kujibu swali hili. Rai ya kwanza ni ya mtazamo wenye muelekeo ambao, tunaweza kuuita wa 'kiumakanika' juu ya umoja wa jamii ya Kiislamu, unaoitakidi kwamba ili kuwa na umoja, Waislamu wote, Mashia, Masuni na wengineo waache imani na itikadi zao za kimadhehebu na badala yake waamini na kuyatekeleza yale tu yanayoziunganisha pamoja madhehebu zote za Uislamu. Kwa mujibu wa mtazamo huu, Waislamu wote inapasa wafuate madhehebu moja ya pamoja, kwa namna ambayo hakutokuwapo na hitilafu wala tofauti yoyote katika itikadi na hukumu za kifiqhi katika jamii ya Kiislamu. Rai ya pili ina mtazamo mwingine kuhusu umoja na kuwaunganisha Waislamu. Rai hii ina muelekeo tuwezao kuuita wa kioganiki na wenye kuzingatia maumbile na hali halisi. Kwa mujibu wa mtazamo wa rai hii, madhumuni na makusudio ya umoja baina ya Waislamu ni kwamba sambamba na wafuasi wa kila madhehebu kushikamana na itikadi na hukumu maalumu za madhehebu yao, katika uhusiano wa kijamii, kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kiutamaduni wawe kitu kimoja na Waislamu wenzao na wazingatie maslahi makuu ya Uislamu na umma wa Kiislamu na wote kwa pamoja daima wawe mithili ya "mkono mmoja" na nguvu moja katika kukabiliana na maadui wa Uislamu.



maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: