bayyinaat

Published time: 19 ,February ,2018      00:04:01
News ID: 229

Katika muda wote wa uhai wa baba yake Bwana Mtume Muhammad SAW na baada ya kutangulia mbele ya haki baba yake mtukufu, akawa pamoja na mumewe Ali AS, Fatima wakati wote alikuwa bega kwa bega na watukufu hao katika kupigania haki, kueneza uadilifu na kuhakikisha kuwa nuru ya Uislamu haizimi. Mtukufu huyo alikuwa na moyo wa hali ya juu wa kutekeleza vilivyo majukumu yake.

Mtukufu huyo alikuwa akihimiza kwamba mtu mwenye ufanisi ni yule ambaye anatekeleza vizuri majukumu yake mema. Muhimu ni kwamba mtu huyo ajue wajibu wake na autekeleze inavyopasa. Kutekeleza vizuri jukumu lake mtu kunahitajia welewa na maarifa pamoja na muono wa mbali. Na ndio maana wakati wote mtukufu huyo alikuwa akifanya juhudi kutumia nguvu zake zote katika kutekeleza mambo yanayomridhisha Mola wake. Tab'an alijua kuwa angeliweza kukaa pembeni na kutumia muda wake wote kufanya ibada na kunog'ona na Mola wake, lakini alitambua vyema pia kuwa, jukumu la mtu ni zaidi ya kufanya ibada, kwani Siku ya Kiyama watu wote wataulizwa walitekeleza vipi majukumu yao yote.

Mtukufu huyo, kutokana na muono wake wa mbali na mtazamo wake wa kina wa mambo aliona hatari kubwa ya kurejea watu kwenye zama za ujahilia hasa baada ya kufariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW. Alitumia hekima ya hali ya juu kuwalingania watu haki na hakumuogopa mtu yeyote katika kubainisha mafundisho ya Bwana Mtume SAW na kuulinda Uislamu.

Miongoni mwa urithi wenye thamani kubwa uliobakishwa na Bibi Fatimatuz Zahra SA ni hotuba yake yenye umuhimu mkubwa aliyoitoa baada ya kufariki dunia baba yake Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW. Aliitoa hotuba hiyo baada ya kuhisi kuzuka mipasuko na kupotoshwa mambo katika jamii ya Waislamu mara baada ya kufariki dunia Mtume. Ndani ya hotuba hiyo, Bibi Fatima ametaja sifa za Waislamu wa kweli. Hotuba hiyo ilikuwa mithili ya siraji inayowaangazia njia wapenda haki na wanaotafuta njia sahihi. Bibi Fatimatuz Zahra SA anataja njia ya kuweza kumwokoa mwanadamu kuwa ni kushikamana na haki na kuwa mtiifu mbele ya amri za Mwenyezi Mungu. Katika sehemu moja ya hotuba hiyo yenye thamani kubwa Bibi Fatimatuz Zahra AS anasema:

Enyi watu! Kumbukeni mlipokuwa ukingoni mwa shimo la moto! Kumbukeni mlivyokuwa duni na mkidharauliwa, na wakati wote mlikuwa mnaogopa wasije maadui kukushambulieni na kukutekeni! Hadi Mwenyezi Mungu alipomtuma Mtume Wake Muhammad SAW kwenu. Mtume wa Mwenyezi Mungu ameingiza nuru katika kiza cha kufru na shirki, akaondoa ugomvi na mizozo kati yanu na kufuta kwa nuru, vumbi lililokuwa limeyafunika macho yenu.

Assalaamu Alayki Yaa Fatimatuz Zahra, Sayyidatu Nisail L'aalamin.

Amani iwe juu yako Ewe Fatima, Mbora wa wanawake wote duniani.

Imeandikwa na Sheikh Salum Bendera
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: