Utangulizi
kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa
rehema na mwenye kurehemu.
Kila sifa iliyokuwa njema
inamstahiki Mwenyezi Mungu mola wa viumbe wote, ambaye hana mfano katika
wasiokuwa yeye. Kisha sala na amani na salamu nazipeleka kwa kiongozi wa umma
huu ambaye ni mtukufu Mtume (saww) pamoja na kizazi chake kitakatifu,
Hakika miongoni mwa sifa ambazo dini
ya Kiislamu imepambika nazo, ni kwamba kila mafundisho ambayo amekuja nayo
mtukufu Mtume Muhammad (saww), basi yatakuwa ni yenye kuwa na uongofu na
mafundisho ya kuchukuliwa na walengwa wa ujumbe na mafundisho yale. Na hali hii
si kwamba tunaikuta tu katika kitabu kitakatifu alichokuja nacho ambacho ni
Quran, bali pia hata katika mwenendo mzima wa bwana Mtume kuanzia maneno,
vitendo na hata mambo ambayo ameyaona na
kuyapitisha kwa ridhaa yake.
Na tunaweza kuchukua mfano mdogo
lakini ukawa na maana kubwa sana katika kuthibitisha jambo hili, nao ni pale tunaporejea katika baadhi
ya aya takatifu za Quran, tunakuta kwamba Mwenyezi Mungu (swt) anatunukulia na kutuelezea
baadhi ya habari za watu waliopita kuanzia namna ya maisha waliyokuwa wakiishi,
sababu za wao kuishi maisha yale, na je walifanikiwa au walifeli katika maisha
yale, na mpaka mwisho kabisa tunakuja kuelezewa mwisho wao ulikuwa vipi, je,
ulikuwa ni mwisho mzuri, au ulikuwa ni mwisho mbaya? Na ni mambo gani ambayo
yalipelekea wao kufikia mwisho ule? Haya yote tunayakuta ndani ya Quran tukufu
yakiwa yameelezewa kwa kirefu.
Lakini jambo la muhimu kwetu ni
kuweza kuchukua baadhi ya mambo katika visa na habari kama hizi ambazo zimekuja
ndani ya kitabu hiki kitakatifu, na kuweza kutambua kwamba, sababu ya kuweza
kuwa na mwisho mzuri au mbaya ni namna ambavyo mwanadamu anajipangia jinsi ya
kuishi au kwa maana nyengine ni kwamba ni aina gani ya mwanadamu anaichagua katika
kuishi? Hii aina inaweza kuwa sababu ya kuendelea na kuwa na mwisho mzuri, au
pia inaweza kuwa sababu ya kufeli na kuwa na mwisho mbaya.
Kama ambavyo sisi ambao leo hii
tunataka kujua sababu za kuendelea au kuanguka kwa tamaduni fulani, ni lazima kutambua
kwanza kwamba, tamaduni ni ile namna ambayo wale waliopita waliweza kukabiliana
na maisha waliyokuwa nayo, kama ambavyo tutakuja na kuelezea kwa kirefu zaidi.
Kwa maana hiyo basi, swala la kuweza
kutambua sababu zilizopelekea kuanguka au kuendelea kwa tamaduni fulani ni
swala muhimu mno, kwani ndani yake tunaweza kutambua kwamba watu wale waliishi
namna gani mpaka ikawa sababu ya kuendelea kwa tamaduni yao, na mpaka kufikia
kuwa na mwisho mzuri, kama ambavyo pia tunatambua kwamba watu wale walikuwa na
mfumo upi ambao ulipelekea kuanguka kwa jamii na tamaduni zao kwa ujumla na
hatimaye kuwa na mwisho mbaya, ili na sisi kupitia wao tuweze kuchagua misingi
sahihi ya kuweza kuendeleza tamaduni zetu, na hatimaye kuwa na mwisho mzuri.
Na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu (swt)
katika makala hii, tutajaribu kutumia njia ambayo ndio sahihi katika kusoma
jambo lolote ambalo linahitajia kupimishwa na jambo lingine, nayo ni njia ya
kusoma na kuangalia tamaduni zilizopita ili kuzifanya kama kioo na kipimo
katika maisha yetu na tamaduni zetu pia.
Na tutaanza kwa kueleza kwanza maana
ya tamaduni, kisha kuja na rai mbalimbali juu ya sababu ya kuanguka au
kuendelea na tamaduni hiyo, na kisha tutakuja na rai au mtazamo wa Quran tukufu
katika kuelezea sababu za kuanguka au kuendelea na tamaduni hizo.