bayyinaat

Published time: 21 ,February ,2018      22:02:50
News ID: 233

Kama tulivyotanguliza ni kwamba kila mwanafamilia anatakiwa kuwa makini katika kuhakikisha kwamba nguzo za familia yake zinashikamana na mahusiano ambayo ni sahihi. Hapa tulikuwa tunajaribu kulenga kwamba kuna mahusiano ambayo si sahihi katika jamii, na mwisho wa mahusiano haya ambayo si sahihi ni kuharibu na kuvunja misingi ya familia n a jamii kwa ujumla kutokana na athari zake mbaya.

Tutajaribu kuelezea baadhi ya mahusiano hayo ambayo si sahihi pamoja na athari zake zinazoambatana nayo.

1. Kujichua (punyeto)

Ni miongoni mwa njia ambazo si rasmi katika kuelekea safari yetu ya kutengeneza familia, tena ukiachilia mbali kuharibu kwake familia pia utakuta kwamba jambo hili lina athari za kiafya kama vile kugubikwa na magonjwa ya msongo wa mawazo na mengineyo.

Na sisi tumeorodhesha hapa janga hili ili tu kuweza kubainisha kwamba kama mwanadamu atakuwa na nia ya kutengeneza familia basi ni lazima aweze kuepukana nalo, kwani ni jambo ambalo linapingana kabisa na falsafa ya kutengeneza familia.

Tiba yake:

Kunaweza kuwa na njia za aina mbalimbali katika kutibu maradhi haya ya kujiridhisha, na hii ni kutokana na tafiti mbalimbali ambazo hufanywa na wataalamu katika kudurusu na kuangalia mazingira au chanzo cha tatizo hili. Hivyo basi kutokana na jambo ambalo sisi tunalizungumzia hapa (Namna ya utengenezaji wa familia bora) tunaweza kusema kwamba hakuna njia salama na nzuri kabisa zaidi ya vijana kutokawia kuoa.

Ndio, ikiwa kama vijana watachukulia maanani jambo la kuoa mapema maana yake ni kwamba wameamua kuchukua uamuzi wa kufuata njia sahihi na kuachana na njia ambazo si sahihi.

Unaweza kusema kwamba mbona kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa katika mahusiano yaliyo sahihi (Ndoa), lakini bado wanakabiliana na janga hili la kujiridhisha, hapo sasa inakuwa ni kutokana na matatizo mengine ambayo si mahala pake hapa kuyajadili.

2. kuchukia jambo lenyewe

Njia ya pili ambayo inaweza kusaidia kuondokana na tatizo la kujichua, ni mwanadamu mwenyewe kulichukia jambo hili,na kuamini kwamba ni katika mambo ambayo hakuna mwanadamu mwenye akili sahihi ambaye anaweza kujihusisha na jambo hili, iwe anataka kujenga familia au hata ambaye hana mpango wa kujenga familia, kwa sababu athari za jambo hili zinaambatana na kila mwenye kulifanya na sio tu mwenye kulifanya huku akiwa anataka kujenga familia au kinyume chake.

3. kutojihusisha na filamu za ngono

Moja ya matatizo ambayo yameikumba jamii ya sasa ni swala zima la kushiriki katika utazamaji wa filamu ambazo hazina misingi ya kiakili, kidini, wala kibinadamu. Nalo ni swala la uangaliaji wa filamu zisizo na maadili, filamu za ngono.

Sasa kama mtu ana nia ya kuachana na swala la kijiridhisha basi ajitahidi kuachana na utazamaji wa hizi filamu.

Kuna jambo hapa ambalo ni lazima tuliweke wazi, nalo ni kwamba tunaposema utazamaji wa filamu za ngono, akili za wengi wetu huenda moja kwa moja katika filamu ambazo zinaonyesha kabisa tendo lenyewe, jambo ambalo si sahihi kabisa. Kwani sisi tupo katika kuangalia mambo ambayo yatamfanya mwanadamu aweze kuachana na tabia ya kujichua, na kutaja kwetu utazamaji wa filamu za ngono ni kutokana na kwamba utazamaji wake unainua hisia za mwanadamu, na kumfanya ahisi hamu ya kufanya tendo la ndoa, na anapokosa wa kufanya naye ndipo ambapo anahamia katika kushiriki tendo la kujichua. Hivyo sababu ya kukataza utazamaji wa filamu za ngono ni uwepo wa uamkaji wa hisia, na jambo hili halipatikanai tu katika hizo filamu, bali utakuta pia linapatikana katika utazamaji majarida yenye kuhamasisha ngono, picha za watu ambao hawana hijabu ya Kiislamu na mengineyo.

Na hapa ndipo utakuta kwamba Uislamu unamkataza mwanadamu kuinua macho yake kunako mambo ambayo yameharamishwa.

Itaendelea........

Sh Abdul Razaq Bilal


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: