bayyinaat

Published time: 26 ,February ,2018      19:22:29
News ID: 243

Mpenzi msomaji wa makala zetu Assalaamu alaykum. Leo nimeamua kuzungumzia japo kwa mukhtasari Baytul-Muqaddas pamoja na histora ya mji huu mtakatifu ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu, eneo ambalo katika miaka yote ya historia limekabiliwa na hujuma na njama za kila namna dhidi yake hususan kutoka kwa utawala haramu wa Israel. Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni njama hizo zimekithiri na kushadidi zaidi. Jiunge nami hadi mwisho wa sehemu ya kwanza ya makala hii. 
Mji wa Baitul Muqqadas ni moja kati ya miji muhimu ya kihistoria duniani wenye utambulisho wa kidini. Kwa mujibu wa baadhi ya maandishi ya kihistoria, mji huu uliasisiwa zaidi ya miaka elfu nne iliyopita.
Mitume na Manabii wengi wa Mwenyezi Mungu walizaliwa au kuishi katika mji huo mtukufu. Ni kwa sababu hii ndio maana mji huu ukazingatiwa na kuwavutia wafuasi wa dini tatu za mbinguni yaani Uyahudi, Ukristo na Uislamu.
Wakati Nabii Ibrahim AS alipohajiri kutoka Misri hadi Palestina, aliishi katika Mji wa Quds. Katika zama hizo Mji wa Quds ulijulikana kwa jina la  Yabus na ulikuwa mashuhuri kama mji wa amani na utulivu. Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Nabii Ibrahim AS aliujenga upya mji huo na kukarabati eneo lake takatifu yaani Msikiti wa al Aqsa ili wafuasi wa Tauhidi waweze kumuabudu Mwenyezi Mungu hapo.
Mji wa Quds pia ni mtakatifu kutokana na kuwa Nabii Mussa AS aliona nuru ya Mwenyezi Mungu na kuzungumza Naye akiwa hapo.  Katika zama zake, Nabii Mussa AS aliamua kuihamisha kaumu ya Bani Israel kutoka Misri hadi Palestina kutokana dhulma na ukandamizaji wa Firaun, lakini kwa sababu ya kaumu hii kukataa kutii amri, Mwenyezi Mungu aliwaacha watapetape jangwani kwa muda wa miaka 40 na hakuwaruhusu kuingia Palestina.  Hali hii iliendelea hadi mwisho wa umri wa Nabii Mussa AS. Inaaminika kuwa Nabii Mussa AS alizikwa karibu na mji wa Quds. Baadhi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu ambao majina yao yako katika Qurani Tukufu, wamezikwa katika ardhi ya Palestina. Mitume hao ni pamoja na Nabii Ibrahim AS, Nabii Yusuf AS, Nabii Yaaqub AS, Nabii Ishaq AS, Nabii Daud AS, Nabii Sulaiman AS na Nabii Zakaria AS.
Baada ya Nabii Daud AS kupewa Utume na Mwenyezi Mungu, aliamua kuupanua mji wa Quds  na kulijenga uypa eneo la ibada la mji huo ambalo kwa mujibu wa riwaya za kihistoria lilikuwa limeharibiwa na kukarabatiwa mara kadhaa.
Kati ya matukio mengine yaliyojiri katika ardhi za Palestina na hivyo kuongeza umuhimu  na utukufu wake miongoni mwa wafuasi wa dini za Tauhidi ni kuzaliwa hapo Nabii Issa AS.  Nabii Issa AS alikuwa mbeba bendera ya amani, utakasifu na ucha Mungu. Nabii Issa AS alizaliwa katika kijiji cha Baitul Lahm karibu na mji wa Quds. Nabii Issa AS alianza kuhubiri katika mji wa huo wa Baitul Muqaddas na hapo ndipo alipopaa na kuelekea mbinguni. Na mwisho kabisa Masjidul Aqsa katika mji wa Quds ndiyo sehemu ambayo Mtume wa Mwisho Muhammad al Mustafa SAW alipaa kuelekea katika mbingu katika tukio maarufu la Miiraj.
Palestina na Mji wa Baitul Muqaddas ni muhimu kwa Waislamu kutokana na kuwepo maeneo matakatifu hapo. Mwenyezi Mungu SWT katika kitabu chake cha mwisho yaani Qur'ani, ameutaja mji huo kuwa ardhi yenye Baraka na takatifu.
Masjidul Aqswa ni eneo la tatu kwa utukufu miongoni mwa Waislamu baada ya Masjidul Haram huko Makka na Masjidun Nabii huko Madina.

Itaendelea…

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: