bayyinaat

Published time: 02 ,March ,2018      12:53:04
News ID: 252

Na Salum Bendera

Tarehe 13 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 64 Hijria inakumbusha tukio chungu na lilojaa ghamu na huzuni kwani ndiyo siku aliyofariki dunia Fatima bint Hizam al Amiriyya al Kilabiyya, maarufu kwa lakabu ya Ummul Banin, mke mwema na mcha Mungu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Mpenzi msomaji, kwa mnasaba huu, nimekuandalia makala fupi kuhusiana na mwanamke huyu mcha-Mungu. Jiunge nami hadi mwisho wa makala hii ili kwa pamoja tupitie japo kwa mukhtasari historia ya mwanamke huyu mwema na wa kupigiwa mfano.

Wanahistoria wametofautiana kuhusiana na siku hasa aliyozaliwa Ummul-Banin na baadhi wanasema kwamba, alizaliwa mwaka wa 5 baada ya Hijra ya Mtume (SAWW). Imam Ali bin Abi Twalib alimuoa bibi huyu mwema baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Ummul Banin anatoka katika kizazi cha mashujaa wakubwa wanaopigiwa mfano baina ya Waarabu. Baada ya kuolewa, mtukufu huyo alimuomba Imam Ali ampe lakabu ambayo atakuwa akiitumia kumwitia badala ya jina lake la Fatima ambalo alichelea kwamba, litakuwa likiwakumbusha wajukuu wa Mtume mama yao, yaani Fatimatu Zahraa (as). Aliwapenda sana Ahlul Bait wa Mtume na historia inahadithia jinsi alivyowatuma watoto wake wote wanne kwenda kulinda familia ya Mtume hususan Imam Hussain katika ardhi ya Karbala. Watoto wote wanne wa Mtukufuku Ummul Banin, wakitanguliwa na Abul Fadhl al Abbas, waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kaka yao Hussein katika medani ya Karbala.

Zeinudeen Amili, fakihi na mwanazuoni wa Kishia wa karne ya 10 Hijria anasema hivi kuhusiana na Ummul-Banin: "Kwa hakika Ummul-Banin alikuwa mwanamke mwenye maarifa na upeo wa hali ya juu na fadhila nyingi. Alikuwa na mapenzi makubwa na familia ya Mtume SAWW na alikuwa na mfungamano shadidi na wenye ikhlasi na Ahlul-Baiti AS. Alijitoa waqfu kwa ajili yya kuwahudumia watu wa nyumba tukufu ya Mtume SAWW. Familia ya Mtume pia ilikuwa ikimpa heshima na daraja maalumu bibi mwema huyu."

Matunda ya maisha yake ya ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib AS yalikuwa ni kuzaliwa watoto wanne ambao ni Abul-Fadhl al-Abbas, Abdallah, Ja'afar na Othman ambao wote waliuawa shahidi mwaka 61 Hijria katika tukio chungu la Karbala la vita baina ya haki na batili. Ambapo jeshi la haki lilikuwa likiongozwa na mjukuu wa Mtume Imam Hussein AS huku lile la batili kinara wakew akiwa Yazid bin Muawiya mtu ambaye aliondokea kuwa mashuhuri kwa kucheza Kamari na kulewa.

Ummul-Banin alitambulika sana kwa subira na uchaji Mungu wake pamoja na subira isiyo na mithili. Wakati Ummul-Banin alipomuona Bashir aliyetumwa na Imam Sajjad AS kwenda Madina ili akawapashe habari watu wa mji huo kuhusiana na tukio la Karbala alimuuliza: Ewe Bashir, una habari gani kuhusu Imam Hussein AS? Bashir akajibu: Mwenyezi Mungu akujaalie subira kwani mwanao Abbas ameuawa. Ummul-Banin akasema tena kumwambia Bashir, nipe habari kuhusu Imam Hussein AS. Bashir akampa habari ya kuuawa shahidi watoto wake wengine watatu waliobakia. Hata hivyo Ummul-Banin akaendelea kusisitiza apewe habari kuhusu Imam Hussein kwanza kabla ya kitu kingine. Ummul-Banin akiwa na utulivu kamili na subira isiyo na kifani alisema:

Ewe Bashir! Nipe habari ya imam wangu (Hussein), kwa hakika watoto na kila kilichoko chini ya mbingu hii kiwe fidia ya Aba Abdillah (Imam Hussein). Alipopewa habari kwamba, Imam Hussein ameuawa shahidi, Ummul-Banin alipiga mayowe na kusema, Ewe Bashir kwa hakika umeupasua moyo wangu na kisha akapaza sauti ya huzuni. Wanahistoria wanasema kuwa, mapenzi haya ya hali ya juu ya Ummul-Banin kwa Ahlul-Baiti AS chimbuko lake ni daraja ya juu ya imani aliyokuwa nayo, maarifa yenye upeo wa juu na ufahamu aliokuwa nao kuhusu Uimamu (Imamah).

Sifa nyingine mashuhuri ya bibi mwema huyo na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib ni fasaha na balagha kubwa aliyokuwa nayo katika lugha ya Kiarabu. Aidha alikuwa malenga na mshairi mahiri na stadi. Ummul-Banin alitumia kipaji alichokuwa nacho kuvifikishia vizazi vilivyokuja baada yake sauti ya kudhulumiwa ya Imam Hussein AS pamoja na masahaba zake watiifu.

Hatimaye bibi mwema huyo aliaga dunia tarehe 13 Mfunguo Tisa Jamadi Thani mwaka 64 Hijria yaani miaka mitatu tu baada ya tukio la Karbala na kuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. Hata hivyo, roho yake iliyojaa mapenzi ya Ahlul Baiti AS pamoja na sifa zake adhimu za usafi, uchaji Mungu, utakasifu na pamoja na utajo wake vingali hai. Salamu na salamu za allah ziwe juu yake.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: