bayyinaat

Published time: 03 ,March ,2018      20:21:45
News ID: 253

Karibu tena ndugu msomaji na mfuatiliaji wa makala zetu hizi, ambapo kwa muda sasa tumekuwa tukizungumzia kunako mambo yanayohusiana na familia, ikiwa ni kuanzia namna gani inapaswa kuanza kujenga familia mpaka namna gani unatakiwa kuishi nayo kwa ujumla.

Na siku ya leo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tumekutana tena, ambapo kwa siku ya leo nitajaribu kujadili na wewe mambo ambayo huhesabika ni nguzo, misingi au nyenzo za kila familia ambayo inataka kufikia yale ambayo Mwenyezi Mungu ameyakusudia kufikiwa na kila mwanadamu.

Kama ilivyo kawaida ni kwamba katika uwanja huu, huwa najaribu kuja na mitazamo au mifumo mbalimbali kunako mada husika, na kisha kuja kuangalia mtazamo wa dini ya Kiislamu pia, hivyo katika sehemu hii tutajaribu kuangalia ni ipi misingi iliyowekwa kwa kuangalia mitazamo ya aina mbalimbali na kisha kuja kuangalia Uislamu pia unasemaje.

1. Uchaguzi sahihi

Baada ya kuwa kijana amekusudia kuoa au kuolewa, bila shaka itakuja wakati atakumbana na jambo hili, jambo ambalo tunaweza kusema kwamba ndio msingi wa kwanza katika harakati za kujenga familia bora, na kwa minajili hiyo ni lazima jambo hili lifanywe kwa kila aina ya uchunguzi na uchaguzi ambao utakuwa ni wenye kuendana na malengo ya muoaji au muolewaji, ambapo si mengine zaidi ya kujenga familia itakayokuwa bora kuanzia ngazi ya familia yenyewe mpaka kufikia ngazi ya jamii kwa ujumla.

Kwa maana nyingine ni kwamba uchaguzi sahihi ndio utakaofanya malengo yako kutimia, na kama hutafanya uchaguzi sahihi basi ni vigumu sana kuweza kutimiza hayo malengo.

Sasa katika swala hili la uchaguzi sahihi kuna nadharia za aina mbalimbali ambazo zimekuja kuelezea njia sahihi katika kufanya uchaguzi sahihi. Hebu ngoja tuzidurusu kwa pamoja njia hizo na kisha tuone ni njia ipi ambayo inafaa kufuatwa kutokana na kupelekea kwake utimiaji wa malengo yetu.

1. Nadharia ya "Romantiki”

Hii ni nadharia ya kwanza katika kuelezea njia inayopaswa kupitwa katika kuchagua mke au mume aliye sahihi, ambapo inategemea sana katika mapenzi ya pande mbili. Kwa maana ya kwamba ikiwa tu mwanamke na mwanaume wamependana basi hiyo ni ishara kwamba watakuwa na maisha ya kifamilia yenye kukamilika, kwa maana nyenzo muhimu katika kuanzisha maisha ya kifamilia ni kuwepo kwa mapenzi baina ya mke na mume.

Inawezekana ikawa ndio nadharia yenye kueneza zaidi ulimwenguni kwa sasa, kwa sababu ndio nadharia ambayo inapigiwa debe sana pamoja na kuungwa mkono na watu wengi sana, mfano mzuri ni maisha ambayo tunayashuhudia katika filamu zinazotengenezwa kila leo, zote unakuta zinaashiria kwamba mapenzi baina ya wawili ndio nyenzo muhimu katika kufanikisha maisha ya kifamilia.

Ndugu msomaji, siwezi kukataa kwamba mapenzi ni kiungo muhimu sana katika maisha ya familia, lakini kitu ambacho naweza kukataa ni kwamba, maisha ya familia na kufikia malengo husika vyote vinasimamia katika mapenzi tu.

Ili niweze kufahamika zaidi acha nikumbushie tena malengo ambayo Mwenyezi Mungu ametaka kuwepo na familia, moja ya malengo hayo ni ili kupatikane jamii bora, yenye kushikamana na mema na kuachana na kila aina ya mabaya. Na malengo haya si malengo ambayo yanapatikana ikiwa jamii husika imejengeka tu katika mapenzi baina ya mke na mume, bali yanapatikana ikiwa kuna nyenzo zaidi ya hiyo, ama ni nyenzo gani hizo naomba tuendelee kuwa pamoja.

2. Nadharia ya "Demokrasia”

Hii ni nadharia ya pili ambayo tunaweza kuipa jina la "demokrasia” kutokana na malengo na shabaha ya kuanzishwa kwake. Nadharia hii inaamini kwamba kila mmoja baada ya kubalehe yupo huru kuoa au kuolewa na ambaye amebalehe.

Hapa unaweza kuona tofauti kubwa iliyopo baina ya nadharia ya kwanza na nadharia hii ya pili, ambapo nadharia ya kwanza tuliona namna ambavyo wameshikilia tawi la mapenzi baina ya pande mbili kama msingi wa kumchagua wa kuanzisha naye familia, ama katika nadharia hii ya pili jambo la muhimu ni kwamba kila mmoja ana uhuru wa kuwa naye maadamu amebalehe kimaumbile.

Hapa nina imani kwamba sitokuwa peke yangu katika kupinga nadharia hii, bali nitakuwa na wenzangu wengi tu, na hii ni kutokana na namna ambavyo nadharia hii ipo mbali na kufikia malengo husika ya kuanzisha familia, kwa maana ya karibu ni kwamba hakutakuwa na tofauti baina ya mwanadamu na mnyama, ambaye yeye kutafuta mwenza kunategemea kukomaa kwake kimaumbile, na kwa kuwa hana lengo la maisha ya kifamilia basi anapokomaa tu kimaumbile anatafuta mwenza wa kuwa naye huku natija na mahusiano yao hayo kila mmoja wetu anaijua. Sasa kwanini wanadamu nao tena ambao wana malengo ya kuanzisha kwao maisha ya familia waingie katika mkumbo huo wa maisha ya kinyama?, kwamba jambo linalopelekea kutafuta mwenza ni kukomaa tu kimaumbile?.

Hivyo tunafikia katika natija ya kwamba nadharia hii pia ipo mbali sana na malengo ya kuanzisha familia, na hivyo haiwezi kuwa msingi sahihi katika kuchagua mwenza sahihi.

3. Nadharia ya Kudurusu

Hii ni nadharia ya tatu na ya mwisho katika mada yetu ya siku ya leo, mimi napenda kuiita nadharia ya kudurusu japokuwa ndiyo nadharia ya dini ya Kiislamu, kwa maana ukiangalia mifumo, misingi, mikakati yote kwa pamoja utakuta kwamba imejengeka katika kusoma na kuangalia kabla ya kutenda.

Ndio, kwa maana tatizo liliopo hapa ni kwamba kijana anataka kuoa au kuolewa, lakini anawezaje kutambua mwenza aliye sahihi ili aweze kuoa au kuolewa naye?. Ukiangalia tu swali lenyewe unajikuta unajijibu kwamba ni lazima kwanza usome mazingira na kudurusu kwa kina ili usije ukakosea njia.

Na kutokana na hayo unakuta kwamba Uislamu umechukulia swala la kusoma mazingira ya unayetaka awe mshirika wako ni swala la awali na muhimu sana.

Ukirejea mafundisho ya Kiislamu unakuta kwamba mwenye kutaka kuoa au kuolewa basi aanze kumuulizia huyo mwenza wake kwa ndugu zake, rafiki zake, jamaa zake ili tu aweze kupata maarifa sahihi juu ya mwenza wake wa maisha.

Ndugu msomaji, mwisho kabisa mwa makala hii, ningependa kutilia mkazo kunako ubatili wa njia mbili za awali kwa kusema kwamba mapenzi kama mapenzi sawa i muhimu kuwepo kwa wanafamilia, lakini mapenzi bila ya uelewa ni sawa na bure, kama ambavyo pia kumchunguza mwenza wako kwa kutumia misingi ambayo si sahihi pia ni sawa na bure.

Nasema hivi kwa sababu kuna ambao wanaweza kusema sawa wanachunguza wa kuwa naye, lakini ukiangalia vigezo ambavyo yeye kaviweka katika huo uchaguzi ni vigezo ambavyo si sahihi, kama vile kuangalia kwa mwenza mambo ambayo huhesabika ni yenye kuisha au yana uwezekano wa kuisha, kama vile uzuri, utajiri Nk.

Hivyo basi kuna kila namna ya kurejea kwa mara nyingine tena katika vigezo ambavyo Uislamu umeviweka kwa ajili ya kuchagua mwenza aliye bora kwa ajili ya kufikia malengo bora.

Sh Abdul razaq Bilal.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: