bayyinaat

Published time: 09 ,March ,2018      07:35:04
News ID: 255

Nuru ya mwezi ilienea katika kona zote za Makka, mji ulikuwa umetulia. Katika lahadha hiyo Mtume Muhammad SAW alikuwa akisubiri kwa hamu kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mtume SAW na mke wake Bi Khadija walikuwa wanasubiri kuzaliwa binti ambaye Mwenyezi Mungu SWT alikuwa amemtaja kuwa Kauthar. Ili kupokea Kauthar, Mtume kwa amri ya Mwenyezi Mungu alifanya ibada kwa siku arubaini huku akiwa anakula chakula cha peponi. Muda wa kusubiri ulikuwa umefikia kikomo. Bibi Khadija alikuwa akisikia uchungu wa ajabu. Khadija alikuwa peke yake katika uchungu wake kwani wanawake wa Kiqureishi walikuwa wamejitenga naye kutokana na imani yake ya Kiislamu. Lakini hamu ya kukiona kiumbe cha mbinguni iliusahilisha uchungu wake. Ghafla harufu nzuri ya peponi ilijaa katika nyumba. Sauti laini ilimjia masikioni na kusema: 'Khadija usiwe na huzuni, iwapo wanawake Waarabu wamekuacha peke yako, sisi tumekuja, kwa idhini yake Mwenyezi Mungu, tukuhudumie'. Bi Khadija alifungua macho yake na akawaona wanawake wanne wa peponi wakiwa pembizoni mwake. Mmoja kati yao alisema: 'Mimi ni Sara, Mke wake Ibrahim, huyu ni Asia, Mke wa Firaun na huyu mwanamke ni Maryam, Mama yake Masihi na huyu mwingine ni Kulthum, Dada yake Musa. Sisi peponi vile vile tutakuwa pamoja nawe. 'Ghafla nuru ya malakuti ilijaa kwenye nyumba. Nuru ilitoka ndani ya nyumba kupitia mianya na milango na kuwastaajabisha wakaazi wa Makka. Kauthari ya Mohammad iliingia duniani.

Nuru yaenea baada ya kuzaliwa Fatima AS

Nuru ilienea kote katika Mji Mtakatifu wa Makkah na dunia iliingia katika furaha. Malaika waliteremka kutoka mbinguni kwa shangwe. Fatima, binti Maasumu wa Khadija, ambaye kumfurahisha kunaleta ridhaa ya Mwenyezi Mungu na kumkasirisha kunaleta ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, yeye ambaye Mwenyezi Mungu anajifakharisha kumuumba, alizaliwa. Fatima alikuja ili awe mwanga katika nyumba ya baba yake. Yeye alikuja ili awe mama wa baba yake. Fatima alikuja ili nuru ya maarifa yake ienee katika maisha ya mwanaadamu. Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Fatima Zahra, salamu ziwe juu ya nuru ya macho ya Mtume SAW, salamu ziwe juu yake ambaye alikuwa mwanaadamu azizi zaidi mbele ya Mtume SAW, salamu juu yake ambaye kizazi chake kilikuwa cha wabeba bendera ya haki katika kutetea na kulinda mafundisho ya Kiislamu.

Majina ya Fatima

Binti mtukufu wa Mtume SAWW ana majina ya kudumu na ambapo kila mojawpao ya majina hayo yana maana tele na maalumu. Jina takatifu la 'Fatima' ndilo jina lake la kwanza mashuhuri. Imam Ja'afar Swadiq AS anasema hivi kuhusu jina hili lenye baraka: "Mbele ya Mwenyezi Mungu, Fatima ana majina makubwa na teule na moja ya majina hayo ni Fatima. Fatima ni jina linalomaanisha kuwa yeye yuko mbali na lolote baya.' Imam Swadiq AS katika kujibu swali hili kuwa ni kwa nini bintiye Mtume SAW ameitwa Zahra alisema hivi: 'Ni kwa sababu alipokuwa akisimama kwenye mihrabu ya ibada nuru yake iliang'aa katika mbingu kama nyota zinavyoangaza ardhi." (Tazama Biharul Anwar Jz. 43 Uk. 10.)

Bibi Fatima Zahra SA alizaliwa tarehe 20 Mfunguo Tisa Jamadi Thani katika jamii ambayo haikuwa na nukta muhimu zinazochangia kuundwa mfumo wenye thamani katika jamii ya mwanaadamu. Wanahistoria wanasema, kabla ya Uislamu, jamii ya bara Arabu haikuwa na thamani za kibinaadamu bali wengi hapo walikuwa watu wenye kufuata mila potofu. Maisha ya kuuana ovyo, ukosefu wa maadili na kuwazika hai watoto wa kike punde wanapozaliwa ni kati ya tabia zilizokuwa zikitawala jamii ya Waarabu katika zama hizo za ujahiliya au ujinga.

Mtume SAW amtukuza Fatima (as) na kubatilisha mila potovu ya kuwadunisha wanawake

Ni katika jamii kama hii ndio Fatimat Zahra akawa kigezo pale Mtume SAW alipobatilisha zile itikadi za kale za kuwazingatia na kutowaheshimu wanawake na watoto wa kike. Katika zama ambazo watoto wa kike walikuwa wakizikwa wakiwa hai, mikono ya Bibi Fatima Zahra ilikuwa sehemu ya kubusiwa na Mtume SAW. Fatima alikuwa Kauthar yaani kheri nyingi kwa baba yake na alipendwa sana na baba yake huyo. Mapenzi ya Mtume SAW kwa Fatima SA hayakuwa tu mapenzi ya kawaida ya baba kwa mtoto wake. Mtume SAW alimtukuza Fatima kama njia ya kubainisha msimamo sahihi wa Uislamu wenye kuinua hadhi ya mwanamke na kuondoa fikra chafu za kuwadunisha wanawake.

Alipokuwa na masahaba zake, Mtume wa Mwenyezi Mungu alitumia kila fursa kuiarifisha shakhsia ya juu ya Fatima. Fadhila nyingi za Bibi Fatima (as) zimenukuliwa kutoka watu ambao si katika nyumba ya Mtume SAW. Nukta hii inaonyesha kuwa, Mtume SAW alikuwa akizibainisha fadhila za Fatima kwa masahaba zake ili shani na hadhi ya juu ya bibi huyo iweze kubakia katika jamii.

Saad ibn Abi Waqqas anasema: 'Nilisikia Mtume SAW akisema: 'Fatima ni Sehemu Yangu. Kila ambaye anamfurahisha Fatima ananifurahisha na kila anayemtendea ubaya huwa ameniudhi. Fatima ndiye kiumbe azizi zaidi kwangu.'

Fatima Zahra (as) ainukia katika nyumba ya Wahyi

Fatimatuz Zahra aliinukia katika nyumba ya Wahyi pembizoni mwa shakhsia adhimu ya Mtume SAW kwa hivyo alipata ufahamu wa juu zaidi kuhusu maisha. Kila wakati Mtume alipoteremshiwa Wahyi na kupewa majukumu ya kubainisha ukweli, Fatima kwa udiriki wa kina, aliweza kupata maarifa ya hali ya juu kutokana na maneno yaliyojaa hekima ya Mtume SAW. Bibi Fatima alikuwa na uono wa mbali katika suala la familia na jamii. Fatima Zahara kwa ustadi na busara aliweza kuleta mlingano katika majukumu ya kifamilia na kijamii.

Bintiye Mtume SAW hakupuuza masuala ya kijamii na kisiasa katika Umma wa Kiislamu na alikuwa na wale waliounga mkono haki kiasi kwamba, alikuwa mshauri na msaidizi wa karibu wa mume wake, Imam Ali AS katika masuala ya kijamii.

Hata katika vita vigumu alienda kumsaidia Mtume SAW na Imam Ali AS.

Bibi Fatima alilitazama kwa umuhimu mkubwa suala la kuwaachilia huru watumwa kiasi kwamba, siku moja aliuchukua mkufu wake aliokuwa amenunuliwa na Imam Ali AS na kuuza kisha kutumia pesa hizo kumkomboa mtumwa.

Mtume SAW alifurahishwa sana na amali hii ya bintiye na kumpongeza kwa alilofanya.

Baada ya kuaga dunia Bwana Mtume, Bibi Fatima SA aliamini kuwa ulikuwa wajibu wake kuthibitisha haki na kukabiliana na upotofu katika uongozi wa Umma wa Kiislamu. Baadhi ya nyusiku alikuwa akiandamana na mume wake katika nyumba za Muhajirina na Ansar na kuwakumbusha kuhusu wasia wa baba yake kuhusu kuchukua uongozi Imam Ali AS ambapo aliwataka watetee haki.

Maisha mafupi yaliyojaa baraka

Kati ya nukta muhimu katika maisha mafupi lakini yaliyojaa baraka ya Bibi Fatima ni kutetea haki na kusema ukweli katika medani za harakati za kijamii.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anasema hivi kuhusu suala hili: "Maisha ya Fatima SA ingawa yalikuwa mafupi na ambayo hayakuzidi miaka 20, lakini yalikuwa bahari kubwa kwa matazamo wa mapambano, kazi za kimapinduzi, subira, elimu, hotuba, kutetea Utume, Uimamu na mfumo wa Kiislamu. Maisha yake ya juhudi na mapambano hatimaye yalimalizika kwa kufikia daraja ya shahada. Maisha haya ya kijihadi ya Fatima Zahra ambayo yalikuwa ya kipekee na yasiyo na kifani kwa yakini ni nukta iliyong'ara na ya kipekee katika fikra za mwanadamu.'

Fatimat Zahra aliutazama ubora wa mwanamke si katika mashindano ya kitoto na haribifu na mwanaume bali katika kutekeleza ipasavyo wadhifa ambao mfumo wa maumbile ulimpa mwanamke. Huu ni wadhifa ambao wanaume hawawezi kutekeleza. Bibi Fatima SA alitekeleza kwa njia bora zaidi majukumu yake kama mke na mama na kupelekea mazingira ya kifamilia kububujika kwa mapenzi. Mwanamke huyu mtukufu wa Uislamu alijenga chuo kikubwa katika mazingira ya nyumba na familia. Katika nyumba yake ndogo, waliibuka wanaadamu wenye thamani.

Hayati Imam Khomeini Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alisema hivi kuhusu nyumba ya Bibi Fatima na familia yake: "Watu waliolelewa katika nyumba ndogo ya Fatima walikuwa wanne au watano lakini kwa hakika walikuwa kielelezo cha uwezo wote wa haki ya Mwenyezi Mungu na walitoa huduma ambazo ziliwavutia wanaadamu wote. Sala na Salamu za Mwenyezi SWT zimshukie Fatimat Zahra ambaye ni kielelezo cha adhama ya nuru ya Mwenyezi Mungu. Ni mwanamke ambaye katika nyumba ndogo na ya kawaida aliwalea wanaadamu ambao nuru yao inaangaza mbingu na ardhi.'

Bila shaka kauli bora zaidi kumhusu Bibi Fatimatuz Zahra ni maneno ya Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu imemtaja Fatima kuwa ni Kauthar.

Kauthar inamaanisha neema nyingi. Kile ambacho kinamfanya Fatima kuwa mfano bora wa kuigwa na wanadamu wote ni ukamilifu wake katika nukta zote za ubora wa mwanaadamu. Nafasi ya umaanawi ya Binti Mtukufu wa Mtume SAW ilikuwa kubwa kiasi kwamba, Malaika wa Mwenyezi Mungu walipokuwa wakizungumza naye walimtaja kuwa mwanamke bora zaidi duniani tokea mwanzo wa maumbile hadi Siku ya Kiyama.

Siku ya Mwanamke Iran

Siku ya kukumbuka kuzaliwa Bibi Fatima Zahra SA huadhimishwa kama Siku ya Mwanamke na Mama nchini Iran. Kwa mara nyingine tunatoa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kumbukumbu hii ya kuzaliwa Fatimatuz Zahra SA. Tunakamilisha kipindi hiki kwa kunukulu maneno ya mtukufu huyo kuhusu ulazima wa kuwaheshimu wazazi wawili aliposema: "Kuwatendea mema baba na mama huzuia ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na kwa kuzingatia suala hili muhimu kidini tutakuwa salama na adhabu ya Mwenyezi Mungu.' Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Imeandikwa na Salum Bendera


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: