bayyinaat

Published time: 11 ,March ,2018      22:26:32
Kwa vile matokeo yanayotokana na juhudi za watu mbalimbali huingiliana na kwa vile kila mtu hutaka kufaidika na matokeo ya matunda hayo, bila shaka hutokea matatizo yanayosababishwa na maslahi mbalimbali ya kibinafsi katika ushirikiano wao wa mara kwa mara. Ni jambo lililo wazi kwamba ni maslahi ya kawaida ndiyo husababisha kila aina ya tofauti. Chuki. Uadui. Dhulma. Na kutoaminiana. Kwa lengo la kuwafanya watu waaminiane, jambo huitajia silsila ya sheria ambazo utekelezaji wake huzuia kutokea kwa ghasia na fujo.
News ID: 269


Sehemu ya  kwanza

MWANADAMU KATIKA MAISHA YA KIJAMII

Tukijaribu kuyachunguza mambo yaliyoleta maendeleo katika jamii mbalimbali zilizopita tutapata ukweli huu kwamba mwanadamu katika jamii hizo alikuwa akiyafuata yale mambo yatakayomletea mafanikio na ukamilifu tu. Bila shaka asingaliufikia ufanisi huo bila ya kuyazingatia mambo yote yanayohitajika maishani mwake. Katika upande mwingine, mwanadamu hutumia ufahamu aliyopewa na Mwenyezi Mungu na kutambua kuwa hawezi kuyaandaa na kuyadhamini mahitaji yote ya maisha yake kwa kujitegemea mwenyewe tu. Huona kuwa hawezi kupata mafanikio maishani kwa sababu hatoweza kuyatatua matatizo yanayomkabili maishani na kufikia ukamilifu kwa kujitegemea mwenyewe. Kwa hiyo hulazimika kuishi maisha ya kijamii. Na kuyadhamini mahitaji yake katika jamii hiyo na kuuchukulia ushirikiano wa mwenzake kuwa njia fupi na nyepesi ya kufikia malengo yake. Huanza kujishughulisha na mambo yanayomdhaminia maisha yake kwa njia ya kijamii. Hii kusema kuwa kila mtu katika jamii hutekeleza wajibu wake na kuyadhamini baadhi ya mahitaji ya jamii kisha baadaye wote huyakusanya mahitaji hayo sehemu moja na kila mmoja kufaidika kutokana na mahitaji hayo kulingana na nafasi yake aliyonayo katika jamii hiyo. Kwa mfumo huu, mwanadamu hushirikiana bega kwa bega na wenzake katika kuyadhamini maisha yake. Ina maana kuwa kila mtu hutoa juhudi zake kwa maslahi ya wenzake na kuyakusanya pamoja matunda ya juhudi hizo. Hapo ndipo kila mmoja wao huja na kuchukua sehemu moja ya matunda hayo kulingana na juhudi alizozitoa katika utangulizi wa kuyakusanya matunda hayo.

HAJA YAKUWEPO SHERIAKATIKA JAMII

Kwa vile matokeo yanayotokana na juhudi za watu mbalimbali huingiliana na kwa vile kila mtu hutaka kufaidika na matokeo ya matunda hayo, bila shaka hutokea matatizo yanayosababishwa na maslahi mbalimbali ya kibinafsi katika ushirikiano wao wa mara kwa mara. Ni jambo lililo wazi kwamba ni maslahi ya kawaida ndiyo husababisha kila aina ya tofauti. Chuki. Uadui. Dhulma. Na kutoaminiana. Kwa lengo la kuwafanya watu waaminiane, jambo huitajia silsila ya sheria ambazo utekelezaji wake huzuia kutokea kwa ghasia na fujo. Ni wazi pia iwapo hapatakuwepo sheria za kuiongoza jamii, bila shaka jamii ya wanadamu itakumbwa na machafuko makubwa ambayo hayataiwezesha jamii hiyo kudumu kwa muda mrefu. Bila shaka hakuna jamii yoyote ambayo imetokea katika historia bila ya kuwa na kanuni, utamaduni wala sheria.

SHERIA KUFUATA MKONDO WAKE

Kwa vile mwanadamu hufanya vitendo vyake kwa khiari yake mwenyewe huhisi kuwa ana uhuru wa kiwango fulani wa kufanya vitendo vyake. Kwa kuuchukulia uhuru huo kuwa wa moja kwa moja usiokuwa wa masharti yoyote, hutaka apate uhuru zaidi na kamili na kuvikwepa vikwazo vyote. Kutokana na hali hiyo mwanadamu huhisi kuwa amezuiliwa na kudhulumiwa katika uhuru wake wa kutaka kufanya ayatakayo. Huchukia sana anapoona kuwa amewekewa masharti ya kuyatenda atakayo, hata kama ni masharti madogo tu yasiyokuwa na ugumu wowote katika kuyatekeleza. Hii ni kwa sababu hata masharti hayo madogo huzuia uhuru wake kamili katika upande wa pili huona kuwa iwapo hatapuuza sehemu fulani ya uhuru wake katika kuzitekeleza sheria zinazoilinda jamii na kuipa utulivu, basi patatokea machafuko makubwa yatayo uchukuwa uhuru wake wote.

Mfano huu wa yeye kuchukua sehemu moja ya kitu fulani kutoka kwa wenzake na hatimaye upande huu wa pili kuchukua sehemu kadhaa za kitu hicho au kukichukua chote. Kwa ibara nyingine hutambua kuwa iwapo atawadhulumu wenzake basi bila shaka wao pia watamdhulumu.

Kwa hiyo kuipuuza sehemu fulani ya uhuru wake kwa kuziheshimu na kutekeleza sheria za kijamii kwa lengo la kujidhaminia kiwango fulani cha uhuru wake.

HULKA BORA

Dini ya Kiislamu inatuamrisha kuwa na utu na tabia njema maishani. Lazima tulijue jukumu letu, tuwe na huruma, wenye kuwatakia kheri wenzetu, wenye kujitolea, tuwe na sifa nzuri, tuwe na uso wa kutabasamu na daima tuwe waadilifu. Tumekatazwa kuvuka mipaka na kuvamia mali, heshima na maisha ya wenzetu. Ni lazima tutumie uwezo wetu wote tulio nao kujitolea kwa lengo la kutafuta elimu na kuwa na adabu. Pia tuwe makini sana katika nyanja zote za maisha. Pia dini inatuamrisha tutende mambo yote ambayo yana faida kwetu sisi na kwa jamii zetu maishani mwetu na tujiepushe na mambo ambayo yanasababisha fujo na ukosefu wa adabu na uvunjifu wa amani. Pia inatufunza tusimamishe sala na kufunga (saumu) na kufanya mambo mengine mengi tuliyoamrishwa ambayo ni alama ya ucha mungu.

TABIA NJEMA

Tabia njema inakuwa ni: Hali ya kinafsi ambayo inayompelekea mwanadamu kuwa na uhusiano mzuri katika jamii, na kuwafanyia wema wanajamii, na kuwatolea maneno mazuri, na uhusiano uliokuwa bora wenye huruma, kama anavyotueleza Imam Jafar Sadiq (a.s) pindi alipoulizwa kunako tabia njema, akasema:

"تلين جناحک، وتطيب کلامک، وتلقی أخاک ببشر حسن"

"Uwe mpole, na utowe maneno yaliyo mazuri, na uwe na furaha pindi unapokutana na ndugu yako”

Mtume (s.a.w.w) amesema:

"إنّکم لم تسعوا النّاس باموالکم فسعوهم باخلاقکم"

"Hakika nyinyi hamtowatosheleza watu kwa mali zenu bali watoshelezeni kwa tabia zenu njema”.

Na huhesabika mtu mwenye tabia njema kuwa ndiye mbora na mwema, kwa sababu Mwenyezi Mungu mtukufu hakuwatuma mitume wake kwa watu isipokuwa baada ya kuwahalalishia tabia hiyo iliyokuwa bora, na kuwapamba nayo, nayo ni moja ya alama ya utukufu na ubora wao. Na ni moja ya anuani ya utu wao pia.

Mwenendo wa sera za kitabia za Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Mambo matatu ambayo yanajulikana kuwa ndio sababu ya kuinuka na kuenea kwa dini tukufu ya Kiislamu.

1. Tabia ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.): Jambo hili limechukuliwa kama ni muhimu katika kuenea kwa Uislamu. Mwenendo na tabia njema ya Bwana Mtume (s.a.w.w) na bashasha katika mazungumzo yake, na hakuwaponda maadui zake na aliwaheshimu.

2. Kujitolea kwa Imamu Ali (a.s) katika kuulinda Uislamu.

3. Mali za bibi Khadija (mke wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w).).

Hapa katika nafasi hii tunazungumzia juu ya maadili ya bwana mtume ambayo ni nguzo kubwa na muhimu sana katika kuendeleza Uislamu. Quran inatueleza jinsi maadili ya mtume yalivyosaidia kueneza Uislamu, na kuzivuta nyoyo za watu katika kuukubali Uislamu kwa kusema:

"فبما رحمة من الله لنت لهم ولو کنت فظا غليظ القلب لانفضوا من حولک،فاعف عنهم واستغفر لهم وشاورهم فی الأمر"

"Ewe mtume, kwa rehema ya mola iliyokufikia umekuwa ni mpole kwa watu, na kama ungelikuwa na moyo mgumu watu wangu kukimbia, basi wasamehe na uwaombee msamaha na shauriana nao katika mambo” (3:159)

Kwa kuangalia Aya hii tunaweza kusema:

1. Ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu.

2. Wenye nyoyo ngumu hawawezi kuwavutia watu katika jambo lolote.

3. Kiongozi bora ni yule aliye na mvuto kwa watu.

4. Kushauriana na watu juu ya mambo yaliyo na umuhimu linajenga umoja na mshikamano na pia ushirikiano.

Imam Ali (a.s) anatueleza namna tabia ya Mtume (s.a.w.w) ilivyokuwa kwa kusema:

"Alikuwa mkarimu sana kwa watu wote, na alikuwa msamehevu sana, na alikuwa ni mkweli zaidi, na alikuwa ni msikivu, na alikuwa ni mpole, na alikuwa na uhusiano mzuri na watu, kila mwenye kumuangalia huvutiwa na tabia yake, na mwenye kushirikiana nae na akamtambua basi humpenda, sijaona mfano wake kabla yake wala baada yake”.

Qur-ani inatuonyesha na kututhibitishia ni jinsi gani mtume Muhammad (s.a.w.w) alivyokuwa na tabia njema kuliko watu wengine:

"وإنّک لعلی خلقٍ عظيم"

"Na bila shaka una tabia njema, tukufu”(68:4)

ATHARI NA FAIDA ZAKE

Tabia njema ina faida hapa duniani.

FAIDA KWA MTU BINAFSI:

1. Kutukuka kwa mwanadamu.

2. Kuzidisha umri (maisha) wa mwanadamu.

3. Pia kuzidi kwa riziki za mwanadamu.

FAIDA ZA KIJAMII:

1. Kuwa na maisha yenye furaha na utulivu na amani.

2. Kuwa na uhusiano mwema na watu.

Kwa sababu mambo yanayomfanya mwanadamu kuwa na furaha na utulivu maishani mwake ni maadili mema, na mambo yanayomfanya kuwa na shida na karaha maishani mwake ni kuwa na maadili mabaya.

Hivyo basi inamlazimu mwanadamu kujipamba na tabia njema, ili afike kwenye lengo la maisha, ambalo ni kuwa na furaha katika maisha.

-------------------------------


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: