bayyinaat

Published time: 19 ,March ,2018      21:49:11
Jambo la kwanza kabisa katika riwaya hapo juu ni kwamba Mtukufu Mtume ameanza kutujuza ya kwamba mwezi wa Rajabu ni mwezi wa Mwenyezi Mungu (swt), na hili jambo pia tunakuja kulipata katika riwaya
News ID: 275


Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu.

Hakika utukufu ni wa muumba ambaye ametubariki kwa mara nyingine kukutana katika uwanja huu kwa lengo la kukumbushana mawili matatu kunako dini yetu tukufu ya Uislamu. Na mara hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutajaribu kuzungumzia kunako utukufu wa Mwezi huu ambao siku ya Jumatatu tumeuanza rasmi, nao ni mwezi wa Rajab, moja ya miezi minne mitukufu katika miezi kumi na miwili ya Kiislamu.

Tufungue maongezi yetu kwa kauli ya Mtukufu bwana Mtume Muhammad (saww) katika kuuzungumzia mwezi huu, imepokelewa kutoka kwake kwamba amesema:

ألاَ إنّ رجب شهر الله الأصمّ، وهو شهر عظيم؛ وإنّما سُمّي الأصمَّ لأنّه لا يقارنه شهر من الشهور حرمةً وفضلاً عند الله تبارك وتعالى. وكان أهلُ الجاهليّة يعظّمونه في جاهليّتها، فلمّا جاء الإسلام لم يَزدَد إلاّ تعظيماً وفضلاً

"....Kwa hakika mwezi wa Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu wenye sifa ya (Al Asammu) (Tutaeleza maana ya jina hili), nao ni mwezi mtukufu, na umepewa jina la Al Asammu kutokana na kwamba hakuna mwezi wowote wenye kuufikia kwa utukufu na fadhila mbele ya Mwenyezi Mungu (swt). Majahili katika zama zao walikuwa wakiutukuza mwezi huu, na ulipokuja Uislamu haukufanya zaidi ya kuuongezea utukufu....”

Jambo la kwanza kabisa katika riwaya hapo juu ni kwamba Mtukufu Mtume ameanza kutujuza ya kwamba mwezi wa Rajabu ni mwezi wa Mwenyezi Mungu (swt), na hili jambo pia tunakuja kulipata katika riwaya zilizopokelewa kutoka kwake Mtume zikiashiria kwamba mwezi wa Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu. Imepokelewa kutoka kwake akisema:

رجب شهر الله، وشعبان شهري، ورمضان شهر أمتي

"....Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Shaaban ni mwezi wangu, na Ramadhan ni mwezi wa Umma wangu”.

Kisha akaja kutueleza ya kwamba mwezi huu ni mwezi mtukufu, kwa maana ya kwamba katika miezi 12 ya mwaka kuna miezi ambayo ina utukufu wake, ambayo ni miezi ya Muharram (Mfungo nne), Dhul qaada, Dhul Hijja pamoja na huu mwezi wa Rajab.

Mwezi wa Rajab una majina mengi sana ambayo yote tukiyaangalia tunakuta kwamba yanarejea katika kuonyesha utukufu wa mwezi huu pamoja na fadhila zake, moja ya majina yake ni hili jina ambalo Mtume amelitaja katika riwaya ya hapo juu, (Al Asammu).

Nini maana ya Al Asammu?, ni neno la Kiarabu lenye maana ya kiziwi. Lakini cha kujiuliza hapa ni kwa nini mwezi huu umepewa sifa ya kutosikia?. Hapa ndipo tunakuja katika maudhui ya makala hii pale tuliposema kwamba ni mwezi ambao umetukuzwa tangu zama za ujahili, yaani kabla hata Uislamu haukuja.

Historia inatuambia kwamba katika zama za jahili mambo ya vita, vurugu, umwagaji damu ni mambo ambayo yalikuwa yameshamili mno, kiasi kwamba ilikuwa inahesabika ni katika mambo ya kila siku kutokana na kukithiri kwake, lakini jambo la ajabu ni kwamba ilipokuwa ikifikia mwezi wa Rajab, mambo haya yalikuwa hayasikiki wala kuendelea, na kutokana na hali hiyo mwezi wa Rajab ukapewa sifa ya kiziwi, kwa maana ya kwamba tangu enzi za jahili haukuwahi kusikia vurugu wala mizozo na umwagaji damu.

Na hii yote ni kwamba majahili walikuwa na imani ya kwamba katika mwezi huu ni muhimu watu wote kujishughulisha na uombaji dua, na kumrejea muumba wao, hivyo walikuwa wakiusubiri kwa hamu kubwa mno ili kuweza kufanikisha mambo yao hayo ya kimaombi.

Mpaka hapo tunakuwa tumeshaelewa ni kwanii mwezi huu umepewa sifa ya kiziwi, kwa maana ya kwamba haukuwahi kusikia vurugu wala umwagaji damu, na ndio maana Mtume baada ya kutaja tu sifa hii moja kwa moja akaambatanisha na ada ya majahili katika kuutukuza mwezi huu.

Sasa hayo yote ni katika zama za jahili, zama kabla ya kuja Uislamu, ama baada ya kuja Uislamu nini kilijiri?.

Mtume katika riwaya anajibu kwa kusema kwamba Uislamu ulipokuja haukufuta ada ile, bali uliiboresha maradufu. Hapa kuna mambo mawili ya msingi ambayo tunapaswa kuyafahamu, nayo ni kwamba Uislamu haukufuta ada ile, na la pili ni kwamba Uislamu uliiboresha maradufu.

Ama kuhusu swala la kwanza ni kawaida katika sheria za Kiislamu kwamba kuna mambo ambayo yalikuwa katika zama za kabla ya Uislamu, na Uislamu ulipokuja uliyaendeleza mambo yale, si kwa maana ya kwamba Uislamu umeshindwa kuja na mbadala, la hasha, bali ni kutokana na kwamba dini ya Kiislamu si dini ya kupingana na maumbile sahihi ya wanadamu, hivyo wanapokuwa wanadamu wameshaelekea katika maumbile sahihi na ambayo Mwenyezi Mungu anayataka kwetu, kunakuwa hakuna haja ya kuyapinga maumbile yale eti kwa kuwa tu yamefanywa na majahili, kwani kipimo cha Uislamu ni usahihi wa jambo na si kwamba nani amefanya jambo lile.

Hivyo tukija katika swala la kumuomba Mwenyezi Mungu, kusimamisha mapigano, kutokuwepo na machafuko, haya yote ni mambo ambayo yanaendana na asili ya mwanadamu (Nature), na kwa kuwa Uislamu unakuja kwa ajili ya kudumisha mambo kama haya kunakuwa hakuna haja ya kuyapinga na kuyakataza.

Tukija katika swala la pili la kwamba Uislamu umekuja na kudumisha maradufu yale yaliyokuwa katika zama za Jahili, ni kwamba sawa katika zama za jahili walikuwa wameshaelekea katika asili wanayotakiwa wanadamu kuielekea, lakini je ni kwa misingi ipi?, ni kwa misingi ambayo Uislamu umeiweka? Au ni kwa misingi mingine tofauti na ya Uislamu?.

Kama tulivyoeleza ni kwamba zama za jahili walikuwa siku zote wapo katika machafuko, lakini punde tu ulipoingia mwezi wa Rajab walisimamisha machafuko yale kwa muda ule, ama baada ya kuisha kwa mwezi ule waliyaendeleza mpaka tena watakapoufikia mwezi mtukufu mwingine. Sasa hapa ndipo utaona tofauti ya uelekeaji kwa fikra za kijahili, na uelekeaji wa fikra za Kiislamu, kwa maana Uislamu unatuambia ya kwamba unapoingia katika mwezi mtukufu basi kujipamba na mambo mema yasiwe ni katika mwezi ule tu, bali iwe ndio mwanzo wa kujipamba hata baada ya kuisha kwa mwezi ule, kwa maana ya kwamba mwezi mtukufu uwe ni funzo la kuishi katika miezi mingine.

Kwa minajili hiyo basi, Uislamu ulipokuja uliboresha utukufu wa mwezi wa Rajab kwa kukubali kwamba ni katika miezi mitukufu mbele ya Mwenyezi Mungu, kama ambavyo pia uliongezea kwamba kujiamba na mema si tu katika mwezi huu bali yapaswa kuwa hivyo siku zote.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: