bayyinaat

Published time: 26 ,March ,2018      21:14:23
Hii ikiwa na maana kwamba jambo la utukufu wa mwezi huu si jambo la kubahatisha, kwa maana kwamba mpaka kufikia kunasibishwa na Mwenyezi Mungu basi bila shaka kuna fadhila nyingi ambazo tumeelezea baadhi yake katika makala zilizopita.
News ID: 278

Karibu ndugu msomaji na mfuatiliaji wa makala zetu ambazo zimekuwa zikilenga hasa jambo la kukumbushana, jambo ambalo katika maisha ya kila siku ya mwanadamu mbali na kwamba Uislamu umelihimiza, ni jambo lenye maana na kipaumbele kikubwa.

Katika makala hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutajaribu kuangalia namna ambavyo Mwislamu inapaswa auelekee mwezi mtukufu wa Rajab, na hii ni baada ya kutambua utukufu wa mwezi huu hasa baada ya kuangalia maneno ya Mtukufu Mtume Muhammad (saww) pale aliposema "....Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Shaban ni mwezi wangu, na Ramadhan ni mwezi wa Umma wangu”.

Hii ikiwa na maana kwamba jambo la utukufu wa mwezi huu si jambo la kubahatisha, kwa maana kwamba mpaka kufikia kunasibishwa na Mwenyezi Mungu basi bila shaka kuna fadhila nyingi ambazo tumeelezea baadhi yake katika makala zilizopita.

Hivyo katika makala hii ningependa kuongea na kila nafsi ambayo itakuwa inajiuliza kwa sasa, sawa mwezi huu wa Rajab una utukufu wake, lakini ni vipi tutaweza kuamiliana nao ili tu nasi tuweze kufaidi hizo baraka na fadhila zake?.

Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu atakuwa anajiuliza katika kuuelekea mwezi huu mtukufu, na hiyo ndiyo sababu iliyopelekea mpaka kuamua kuandika makala hii ili kuweza kukumbushana mambo ambayo yanatupasa kuyafanya kwa lengo la kuingia mwezi wa Rajab huku tukiwa tayari kuoga na kuchota fadhila zilizomo.

1. Mwelekeo kamili

Hii ni hatua ambayo tunaweza kusema ni kama utangulizi wa kuuelekea mwezi wa Rajab, ambapo kila mmoja wetu anatakiwa kabla ya kuingia mwezi wa Rajab basi ni vyema akaufahamu mwezi huu kinaga ubaga. Kwa maana ya kwamba ni lazima kila mmoja wetu afahamu kwamba mwezi huu pamoja na kuwa na fadhila nyingi pia ni mwezi ambao huhesabika kama maandalizi ya kuutafuta ule usiku wa cheo (Lailatul Qadr), hivyo ni vyema tukaingia katika mwezi huu kwa ukamilifu kabisa, yaani akili pamoja na nyoyo zetu ziwe tayari kuingia katika mwezi huu.

Hii pia maana yake ni kwamba pamoja na kwamba akili na moyo kuwa tayari bado kuna haja ya kuutambua mwezi huu kwa maana ya kuutambua, hivyo ambaye hana elimu juu ya mwezi huu ajitahidi aweze kuujua, na yule ambaye ana elimu na mwezi huu basi ajitahidi kuyafanyia kazi yale ayajuayo ili aongeze maarifa yake kwanza, na pili aweze kuzinduka zaidi katika kuutumia mwezi huu.

2. Kuwa na moyo wa kukubali

Hapa kuna nukta moja ningependa kuiashiria katika jambo hili, mara nyingi tunapokuwa tunaingia katika miezi mitukufu kama hii tunakutana na riwaya mbalimbali zenye kuzungumzia fadhila na baraka ambapo wakati mwingine akili zetu zinakuwa ni zenye kukataa uhakika au hata uhalisia wa riwaya zile, na mwisho wake tunaangukia katika janga la kuacha kutenda yaliyo mema basi tu kwa kigezo cha kuachana na riwaya iliyotaja jambo lile.

Sawa ni muhimu kuweza kuchunguza uhakika wa riwaya, kwa maana kukubali jambo bila ya dalili ni hatari, lakini pia lazima tutambue ya kwamba kukataa jambo bila ya dalili pia ni hatari zaidi, kwani huwezi jua ni mangapi ambayo utayakosa kwa kukataa kwako ambayo laiti kama ungaliuliza ungalifaidika nayo.

Hivyo basi ili tusiangukie katika janga hili la kukubali au kukataa jambo bila ya dalili, katika kuelekea safari yetu ya kuchuma fadhila za mwezi wa Rajab, ni vyema tukafungua nyoyo zetu na kuwa wazi pale tunapoambiwa jambo fulani, lakini hatua hii inakuja baada ya sisi wenyewe kutumia muda wetu katika kutafuta ukweli wa yale ambayo tunataka kuyajua.

3. Kutenda zaidi

Ndio, kwani katika mwezi huu hakuna ambalo utalichuma bila ya kulifanyia kazi, hivyo kuna kila haja ya kutenda zaidi yenye kumridhisha Mwenyezi Mungu.

Usikubali nyakati zako zikawa zinapita bila ya kuwa katika yenye kumridhisha Mungu, iwe usiku iwe mchana, hakikisha kwamba upo katika kutenda matendo mema.

4. Kuichagulia nafsi yako masira sahihi

Kwa maana nyingine ni kwamba siku zote uwe ni mwenye kupigana na nafsi yako na uhakikishe kwamba wewe ndio unaichagulia njia ya kupita.

Hii ni pamoja na kuielewesha kwamba hapa duniani ni wenye kupita, na sehemu yetu ya milele inategemea na tunavyoijenga sisi wenyewe, hivyo fanya kila uwezalo ili tu uweze kuwa ni katika wenye kufaulu huko tuendako.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo sisi kama Waislamu kuna umuhimu wa kushikamana nayo kabla ya kuingia katika mwezi wa Rajab, japokuwa ni mengi sana ambayo inapaswa kushikamana nayo, inatosha tu kuwa na kipimo kwamba mwezi huu ni mwezi wa kuchuma, hivyo kila lenye kumridhisha muumba basi ni lazima tushikamane nalo.

Tumalizie maongezi yetu kwa kutaja maneno matakatifu ya mtukufu Mtume Muhammad (saww):


إن الله تعالى نصب في السماء السابعة ملَكاً يقال له الداعي، فإذا دخل شهر رجب نادى ذلك الملك كل ليلة منه الى الصباح يقول: "طوبى للذاكرين، طوبى للطائعين"، (يعني هنيئاً) ويقول الله تعالى
:"أنا جليس من جالسني ومطيع من أطاعني وغافر من استغفرني. الشهر شهري والعبد عبدي..والرحمة رحمتي، فمن دعاني في هذا الشهر، أجبته وجعلت هذا الشهر حبلاً بيني وبين عبادي، فمن إعتصم به وصل إلي

"….Hakika Mwenyezi Mungu ana malaika wake katika mbingu ya saba kwa jina la "Mlinganiaji”, pindi tu unapoingia mwezi wa Rajab hunadi kuanzia usiku mpaka asubuhi na kusema "…Heri wenye kumtaja Mwenyezi Mungu, Heri yao wenye kumtii Mwenyezi Mungu”. Na pia Mwenyezi Mungu mwenyewe husema "…..Mimi huwa karibu na mwenye kuwa karibu nami, humsikia mwenye kunitii, husamehe mwenye kuniomba msamaha, mwezi huu ni mwezi wangu na mja ni mja wangu kama ambavyo rehema ni rehema zangu, hivyo mwenye kuniomba katika mwezi huu humjibu, na mwezi huu nimeufanya kuwa ni kamba baina yangu na waja wangu, hivyo mwenye kushikamana nayo atanifikia….”

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal (Abuu Asghar).


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: