bayyinaat

Published time: 05 ,March ,2017      18:22:30
Hakika mwanadamu siku zote ni mwenye kuzungukwa na wasiwasi unaotokana na shetani, na mashetani hawa ima wawe ni katika watu au hata majini lakini ni kwamba siku zote wanajaribu kuitawala nafsi yake na kuiendesha. sasa katika sura hii.......
News ID: 29

Surat Nnas

(watu)

MAMBO YANAYOKUSANYWA NA SURA HII;

Hakika mwanadamu siku zote ni mwenye kuzungukwa na wasiwasi unaotokana na shetani, na mashetani hawa ima wawe ni katika watu au hata majini lakini ni kwamba siku zote wanajaribu kuitawala nafsi yake na kuiendesha.

Sasa katika sura hii ni kwamba Mwenyezi Mungu anamfundisha Mtume wake njia za kuweza kujikinga dhidi ya majini na mashetani hao kwa kujiweka karibu na mola wake.

FADHILA ZA KUSOMA SURA HII:

Imepokelewa kutoka kwa Abuu jaafar kwamba amesema "siku moja Mtume alishitakia kwa Mwenyezi Mungu juu ya maumivu makali yaliyomkuta, jibril akamjia huku akiwa na Mikaeli, kisha Jibril akamsomea sura hii na Mikaeli akamsomea surat falaq”.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu.

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ(1)

(1) Sema ninajilinda kwa mola wa watu.

مَلِكِ النَّاسِ(2)

(2) Mfalme wa watu.

إِلَٰهِ النَّاسِ(3)

(3) Mungu wa watu.

Hakika kama tutaziangalia aya tatu hizi tutakuta kwamba Mwenyezi Mungu (swt) ametumia sifa tatu ambazo ndio msingi wa kila kitu katika kinachokusudiwa na sura hii, sifa zenyewe ni MOLA, MFALME AU MMILIKI na sifa ya MUNGU. Hii yote ikiwa na maana kwamba, ambaye anaweza kumkinga mwanadamu kutokana na shari za mashetani basi ni ambaye ana sifa hizi tu na si mwingine yeyote yule.

Pia lazima ifahamike kwamba neno kujilinda lililotumika katika aya ya kwanza, halina maana ya kwamba mwanadamu awe ni mwenye kulitamka tu kwamba anajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shetani, bali inatakiwa kwa huyu mwanadamu awe ni mwenye kufikiria muda wote kwamba yeye yupo karibu na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kujilinda, pia afanye matendo yatakayoashiria kwamba ni kweli yupo karibu na Mwenyezi Mungu.

مِنْ شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ(4)

(4) Kutokana na shari za kila mwenye kutia wasiwasi na mwenye kurejea nyuma.

الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ(5)

(5) Ambaye hutia wasiwasi katika nyoyo za watu.

Wasiwasi ni nini?

Kama ambavyo inaelezwa katika vitabu vya lugha kwamba wasiwasi ni sauti isiyosikika. Lakini ikaja ikatumika hata katika kila jambo baya ambalo humjia mwanadamu na kulifikiria, na hii ni kutokana kwamba kufikiria jambo baya hufanana na sauti ambayo inakuwa inakunong`oneza sikioni.

Ni nani huyo mwenye kurejea nyuma?

Sifa ya mwenye kurejea nyuma ambayo imetajwa katika aya ya hapo juu, ni sifa ambayo inarejea kwa shetani ambaye hutia wasiwasi katika nyoyo za watu. Na sababu ya kusifiwa hivyo ni kwamba, pindi endapo mja atakuwa ni mwenye kujiweka karibu na mola wake, basi shetani hukimbia na hurudi nyuma na hata hujificha kabisa.

مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ(6)

(6) Ambaye ni katika majini na watu.

Aya hii ya mwisho ni ishara ya kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba mwenye sifa ya kutia wasiwasi si kwamba ni kiumbe cha aina fulani basi, bali kama ambavyo kinaweza kuwa ni katika majini pia kinaweza kuwa ni katika watu. Hivyo basi ni wajibu wa mwanadamu kuwa makini na kila aina ya kiumbe kiwe cha mbali au karibu yake.

Na hapa ndio tunapata maana ya kwanini tunakatazwa na Uislamu kuwa na marafiki waovu au hata viongozi waovu, kwani hawa wote wanakuwa katika mfumo wa kumtia mja wasiwasi na kumpelekea kuwa mbali na mola wake.

Mwisho kabisa tuangalie kwanini sura hii imeitwa kwa jina la watu? Hii ina maana kwamba fikra za watu wengi zipo katika kuamini kwamba wasiwasi hutokana na majini tu, na kwamba watu hawawezi kuwa na mchango katika hilo. Sasa sura hii imekuja kuonyesha kwamba ni tofauti na tunavyodhania, bali watu ndio wana mchango mkubwa sana katika kutia wasiwasi katika nyoyo za watu.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: