bayyinaat

Published time: 22 ,April ,2018      20:28:00
Tarehe 3 Shaaban ni siku ambayo mji wa Madina ulishuhudia kuzaliwa mtoto mwingine katika nyumba ya Bibi Fatimatuz Zahra (AS) binti mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
News ID: 307

Karibu mpenzi msomaji katika makala hii itakayoaangazia japo kwa muhtasari maisha ya Imam Hussein bin Abi bin Abi Twalib AS.

Tarehe 3 Shaaban ni siku ambayo mji wa Madina ulishuhudia kuzaliwa mtoto mwingine katika nyumba ya Bibi Fatimatuz Zahra (AS) binti mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Huyo alikuwa ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia hiyo ambayo Mtume Muhammad SAW alikuwa siku zote akiwaita watu wa familia hiyo kuwa ni Ahlul-Bayt wake na daima akiwaombea dua za kheri na amani. Katika Qur'ani Tukufu pia kuna aya inayotaja ubora, utukufu na usafi wa watu wa nyumba hiyo. Katika sehemu moja ya aya ya 33 ya Suratul Ahzab Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا

Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Ahlul Bayt (Watu wa Nyumba ya Mtume), na kukusafisheni baarabara.

Mama wa kitoto hicho kichanga alikuwa ni Faatimah, binti wa Bwana Mtume ambaye alikuwa na sifa za ukamilifu wa kibinaadamu alijipamba kwa sifa bora kabisa za kimaadili kiasi kwamba anahesabiwa kuwa ni mwanamke bora zaidi duniani. Mwenyezi Mungu anataja fadhila za Bibi Faatimah katika Suratu al Kauthar wakati maadui wa Bwana Mtume walipokuwa wakimfanyia tashtiti kuwa amekatikiwa na kizazi, Mwenyezi Mungu akamliwaza Mtume Wake akimwambia kuwa hao wanaofanya chagizo hizo wao ndio waliokatikiwa na kizazi kwani kizazi cha Bwana Mtume kingelineemeka na kuenea kote dunia kupitia kwa Bibi Fatimatuz Zahra SA. Baba wa kitoto hicho ni Ali mwanamme wa kwanza kuwa Muislamu. Imam Ali AS alijulikana vilivyo kwa ushujaa wake na kutotetereka kwake katika kuilinda na kuitetea dini tukufu ya Kiislamu.

Baada ya kuzaliwa, kichanga hicho kilipelekwa katika "mahdhar" tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Imam Ali AS akamuomba Bwana Mtume kwa heshima zote amchagulie jina mtoto huyo, naye Bwana Mtume hakuajizi ila alimchagulia jina mara moja akamwita Hussein.

Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwenu nyinyi nyote kwa mnasaba huo adhimu.

Mapenzi ya Mtume SAW kwa Imam Hussein AS

Mapenzi ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa Imam Husseiin AS yalikuwa makubwa kiasi kwamba hayakufichika kwa mtu yeyote yule. Binti ash Shatwi, msomi wa kike wa Misri anasema kuhusu mapenzi makubwa aliyokuwa nayo Bwana Mtume kwa mjukuu wake Imam Hussein kwamba:

"Majina ya Hassan na Hussein kwa Bwana Mtume yalikuwa mithili ya sauti ya kutuliza na kuburudisha moyo, na Bwana Mtume alikuwa hachoki kukariri mara kwa mara majina hayo. Alikuwa akiwaita Hassan na Hussein kuwa ni wanawe. Mwenyezi Mungu alimpa Zahra neema kubwa sana ya kuendeleza kizazi cha Bwana Mtume na alimpa heshima hiyo pia Ali ambaye kupitia kwake, kizazi cha Mtume kimeendelea hadi leo hii."

Mapenzi ya Bwana Mtume kwa mtoto huyo hayakutokana tu na uhusiano wake wa kidamu na nasaba. Kwani kwa mujibu wa hoja na dalili ni kwamba Bwana Mtume alikuwa hafanyi chochote kwa mapenzi ya nafsi, bali yote yalikuwa ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mapenzi ya Bwana Mtume kwa Hassan na Hussein yalitokana na nafasi ya aina yake waliyokuwa nayo watukufu hao mbele ya Mola Muumba. Moyo wa Bwana Mtume ulijaa mapenzi kwa wajukuu zake hao kiasi kwamba, amenukuliwa akisema: Yeyote anayewapenda wajukuu zake hao ni sawa na kwamba amempenda yeye na yeyote anayewafanyia uadui ni kana kwamba amemfanyia yeye uadui.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: