bayyinaat

Published time: 31 ,May ,2018      13:13:05
Jina lake ambalo hata katika kitabu cha Taurati lilikuwa limeshatajwa ni jina la Shubbar, kwa maana ya mzuri, jina ambalo ndilo lilikuwa jina la mtoto mkubwa wa Nabii Harun (as).
News ID: 310

Mnamo tarehe 15 Ramadhan, mwaka wa tatu Hijiria alizaliwa moja ya viumbe bora katika uso wa ardhi, si mwingine bali ni Imamu Hassan Bin Ally bin Abitalib (as).

Japokuwa kuna kauli isemayo kwamba alizaliwa mwaka wa pili, ila kauli hiyo ya kwanza ndiyo yenye nguvu miongoni mwa kauli hizo.

Jina lake ambalo hata katika kitabu cha Taurati lilikuwa limeshatajwa ni jina la Shubbar, kwa maana ya mzuri, jina ambalo ndilo lilikuwa jina la mtoto mkubwa wa Nabii Harun (as).

Miongoni mwa Kuniya zake ni Abuu Muhammad, kama ambavyo miongoni mwa lakabu zake ni Karima, Al Sayyid, AL Sibt, Al Amin, Al Hujja. Al Barru. Al Naqii, Al Zakiy, Al Mujtaba, na Al Zahid.

Historia ya jina lake tukufu:

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Zainul Abidin (as) kwamba amesema: siku ambayo Bibi Fatima (as) alijifungua, alimwambia mume wake ambaye ni Imamu Ally (as) kwamba ampatie jina kijana huyo. Imamu akajibu kumwambia Bibi Fatima "Sikuwa na jeuri ya kumtangulia Bwana Mtume katika jambo hilo”. Baada ya muda Bwana Mtume (saww) akaja, na baada ya kuona kwamba kijana yule amefungwa katika kitambaa cha njano akasema "...Kwani si niliwakataza kumfunga katika kitambaa cha njano?”, kisha akaagiza kitambaa cheupe na kumfunga nacho kisha akamwambia Imamu Ally "Je tayari umeshampatia jina?...”. Imamu akajibu kwa kusema "Sikuwa ni mwenye kukutangulia katika jambo hilo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu”. Bwana Mtume naye akasema "...Hata mimi sikuwa ni mwenye kumtangulia Mwenyezi Mungu katika jambo hili”.

Mwenyezi Mungu akamwambia Jibril "....Hakika siku ya leo Muhammad ameruzukiwa kijana, basi nenda ukampe sana salamu zangu pamoja na pongezi, kisha mwambie ya kwamba Ally kwake ni sawa na Harun alivyokuwa kwa Musa, hivyo basi kijana wa Ally apewe jina la kijana wa Harun.

Jibril akashuka kwa Bwana Mtume na kumpa salamu na pongezi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kisha akamwambia "...Hakika Mwenyezi Mungu anakwambia umpatie jina la kijana wa Harun”. Mtume akauliza "...Ndio alikuwa na jina gani?”. Jibril akasema "..Alikuwa anaitwa Shabbir”. Mtume akasema "...Lakini sisi ni Waarabu! (kwa maana jina hili ni la Kiibrenia)”. Jibril akasema "..Basi mwite Hassan (maana ya Shabbir kutoka lugha ya Kiibrenia”. Basi ndipo kijana yule akaitwa jina la Hassan (as).

Weledi wake

Imepokelewa kwamba miongoni mwa dalili za weledi na utambuzi wa Imamu Hassan ni kwamba alikuwa akihudhuria vikao vya Mtume Muhammad ingali bado alikuwa ni kijana wa miaka saba, na kisha kusikiliza aya au riwaya kutoka kwa kwake na kisha kuja kumsimulia mama yake kama ambavyo amesikia bila ya kuzidisha wala kuongeza chochote.

Na baadaye Imamu Ally anaporejea nyumbani humkuta mke wake akiwa na elimu ya siku nzima kutoka kwa Mtume kana kwamba alikuwa katika kikao hicho, kumbe ni kutokana na alivyosimuliwa na Imamu Hassan (as).


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: