bayyinaat

Published time: 31 ,May ,2018      13:17:16
Miongoni mwa fadhila kubwa za Imamu huyu ni kwamba kuna riwaya nyingi sana kutoka kwa Bwana Mtume ambazo zimekuja katika kuelezea hilo, miongoni mwa riwaya hizo ni:
News ID: 311

Fadhila zake na Tabia zake njema

Miongoni mwa fadhila kubwa za Imamu huyu ni kwamba kuna riwaya nyingi sana kutoka kwa Bwana Mtume ambazo  zimekuja katika kuelezea hilo, miongoni mwa riwaya hizo ni:

·       Siku moja mmoja wa Masahaba anasema kwamba alimuona Mtume amemuweka Imamu Hassan katika mabega yake  huku akisema ".....Kama unanipenda basi mpende na huyu”.

·       Pia imepokelewa kutoka Abuu Huraira kwamba amesema "....Hakuna wakati ambao nimemuona Hassan nisiokwe na machozi, na hii ni kutokana na kwamba siku moja nilimuona akimpandia Bwana Mtume kisha Mtume kuchukua mdomo wake na kuuweka katika mdomo wa Hassan huku akisema "...Ewe Mwenyezi Mungu, mpende mwenye kumpenda huyu, kwani mimi nampenda sana” mara tatu.[1]

Mbali na riwaya hizo pia kuna riwaya nyingi mno kutoka kwa Mtume ambazo zote zinaashiria ubora na fadhila za Imamu Hassan (as), kama zile riwaya zenye kusema ya kwamba Hassan na Hussein ni viongozi wa vijana wa peponi, au riwaya zote zenye kuamrisha kumpenda yeye kwani Mtume mwenyewe alikuwa akimpenda kijana huyu.

Mahusiano yake na Mungu wake:

Kama tunavyojua ya kwamba moja ya mambo ambayo yanafanya watu hawa waweze kuwa bora mbele ya Mwenyezi Mungu, ni kutokana na mshikamano wao wa nguvu na muumba huyo. Basi hata tukija kwa Imamu Hassan pia tunakuta kwamba hakuwa mbali na ada na mstari huo, kwani inapokelewa kwamba Imamu Hassan alikuwa ni mwenye kuabudu zaidi katika zama zake, mwenye kuipa dunia mgongo zaidi kuliko watu waote wa zama zake.

Tunaambiwa kwamba alikuwa  akitekeleza ibada yake ya Hijja miaka yote kwa kutembea kwa miguu, na kuna baadhi ya riwaya zinasema kwamba mbali na kutembea kwa miguu bado alikuwa akitembea peku. Alikuwa akikumbuka kifo, kupita katika sirat, siku ya kukutana na Mungu hulia mpaka kufikia hatua ya kuzimia.

Kifupi ni kwamba katika maisha ya Ibada ya Imamu Hassan, tunaweza kupata masomo yafuatayo:

·       Ibada haina maana kwamba mwanadamu ajitenge kabisa na wenzake, kwani pamoja na kwamba Imamu alikuwa yu karibu sana na Mwenyezi Mungu bado tunakuta maisha yake ya kijamii yalikuwa ni yenye kuimarika  katika kila nyanja.

·       Ibada si tu matendo maalumu ya Kidini kama vile Swala, Funga na mengineyo. Bali kila tendo ambalo kulifanya kwake kunakuwa na kutafuta radhi ya Muumba huhesabika ni ibada. Matendo kama kusaidia wengine, kushiriki katika shughuli za kijamii, kuishi vizuri na watu na mengineyo, endapo yatafanywa kwa nia ya kutafuta radhi za Mwenyezi mungu basi huingia katika ibada pia, hivyo hakuna haja ya kukaa nyuma katika maswala hayo.

·       Ibada haina maana kwamba unakuwa umeepukana na sheria za Muumba. Kwa maana ya kwamba kufanya kwako ibada kusikuweke katika hali ya kuona kwamba tayari umeshamaliza kila kitu, na kwamba hakuna tena jukumu lolote ambalo unatakiwa kulisimamia, bali mwanadamu pamoja na kufanya ibada zake, bado anatakiwa kubakia katika hali ya shauku juu ya ibada zake, kwani hakuna anayejua uhakika wa kukubaliwa au kukataliwa ibada zake.

 

 

Upole wake

Katika sifa za Imamu Hassan ni upole, upole ambao kwao aliweza kuwavuta watu katika dini ya Mwenyezi Mungu bila hata ya kutumia nguvu nyingi.

Inapokelewa kwamba siku moja alikuja mzee kutokea mji wa Sham na kuanza kumtukana Imamu (as), Imamu akamsikiliza mpaka alipomaliza na kumwambia "....Ewe Mzee wangu, najua kwamba ni mgeni maeneo haya, na najua fika kwamba umeshaambiwa mabaya kuhusu sisi, lakini laiti kama ungaliniomba msaada basi ningalikusaidia, na kama ungaliniuliza njia basi ningalikuelekea, na kama ulikuwa unahitajia jambo basi ningali kusaidia, na kama huna makazi basi tutakupatia, na kama muda utaamua kuondoka na sisi na kuamua kuwa mgeni wetu mpaka siku ya kuondoka kwako basi itakuwa ni vyema zaidi kwako, kwani tuna sehemu kubwa na mali za kutosha kwa ajili ya kukirimu wageni”.

Yule mzee baada ya kusikia maneno hayo akasema "....Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wewe ni kiongozi wa Mungu katika uso wa dunia, na kwa hakika Mungu hujua ni sehemu gani ya kuweka ujumbe wake, hakika wewe pamoja na baba yako mlikuwa ni watu ambao nawachukia sana, lakini kuanzia sasa nyinyi ni viumbe ni wapendao kuliko wote katika dunia..” Kisha akakusanya mizogo yake na kuelekea nyumbani kwa Imamu na kubakia naye kwa siku kadhaa mpaka alipoondoka.[2]

Huruma kwa wanyama:

Huruma kwa viumbe hai ni moja ya ishara za utu na ukarimu wa mwanadamu, kwa maana katika maisha yetu kuna viumbe vingine ambavyo tunashirikiana navyo na ambavyo vinahitaji ushirikiano kutoka kwetu.

Huu ushirikiano ndio ambao tunaukuta kwa Imamu Hassan (as), kwani inapokelewa kwamba siku moja alikuwa anakula chakula na pembeni yake kukiwa na mbwa, na kila ambapo alikuwa anakula tonge moja basi la pili yake alikuwa akimtupia mbwa yule. Sahaba mmoja akapita na kumuuliza Imamu juu ya jambo lile, Imamu akasema ".....Naam, muache ale, kwa maana ninaona haya kula chakula wakati ambao kuna kiumbe hai kinaniangalia na mimi nisimpatie chakula kile..”

Miongoni mwa nasaha za kutoka kwake:

Zifuatazo ni baadhi za nasaha kutoka kwa Imamu Hassan (as) katika kuhakikisha kwamba wanadamu wanakuwa katika mstari ulionyooka na hatimaye maisha yetu baada ya duniani yanakuwa pia katika hali nzuri.

·       Anasema "....Ewe mwanadamu, hakika maisha yako yapo katika hali ya kupotea tangu siku uliyotoka tumboni kwa mama yako, basi jitahidi kufanya yenye faida kwako, kwani muumini siku zote hujiandaa kwa ajili ya kesho, lakini kafiri huona maisha ni ya duniani tu...”.

·       Anasema ".....Kuosha mikono kabla ya chakula huondoa ufukara, kama ambavyo kuosha baada ya chakula pia huondoa huzuni”.

·       Anasema ".....Uulizaji mzuri ni nusu ya jawabu”. Kwa maana ya kwamba ili kupata jibu la swali lako basi unatakiwa uwe na njia nzuri za kuuliza swali lile, maana uulizaji mbaya unaweza kupelekea kukosa jawabu au kupata jawabu lisilo kamili.

Huyu ndiye Imamu Hassan (as) kwa kifupi, kwani hakuna anayeweza kuandika kwa kiwango cha ubora wa watu hawa.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal.[1] Al Bihar Uk 266 hadithi ya 32

[2] Alkamil fil Lugha wal Adab Juz 1 Uk 325

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: