bayyinaat

Published time: 19 ,September ,2018      10:17:42
Haikuishia hapo, bali ikafikia hatua ambayo Ibilisi anaweka viapo vya kuendelea kumsakama mwanadamu huyu katika maisha yake ya kila siku, ikiwa ni pamoja na kumkalia katika njia yake na kumuharibia mipango yake ya kumuelekea Mungu wake, isipokuwa waja wema ambao watakuwa wameshikamana na baadhi ya mambo ambayo kwa huyo Ibilisi yatakuwa ni kizuizi cha kuwakalia njiani.
News ID: 314

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu, Mwenyezi Mungu ambaye ndio msingi wa kila jambo, Mungu ambaye ndie hutoa nguvu za kupambana na kila jambo katika maisha yetu.

Kwa hakika lazima tukubaliane kwamba maisha ya mwanadamu ni maisha yenye kukutana na vikwazo vya kila aina, kuanzia mwanzo wa uumbwaji wake mpaka siku ya mwisho ambayo atarejea kwa mola wake. Nasema haya ikiwa ni baada ya kukumbuka tukio zima la mwanadamu pindi alipoanza kuonewa hasadi na Ibilisi hata kabla ya kuja katika ulimwengu huu, pale ambapo Mwenyezi Mungu alipomuumba Nabii Adamu na kisha kuamrisha malaika wote akiwemo huyu Ibilisi wa sasa wamsujudie, lakini kilichotokea ni kiburi pamoja na husuda ya kwanini mwanadamu asujudiwe na ambaye anajihisi bora.

Haikuishia hapo, bali ikafikia hatua ambayo Ibilisi anaweka viapo vya kuendelea kumsakama mwanadamu huyu katika maisha yake ya kila siku, ikiwa ni pamoja na kumkalia katika njia yake na kumuharibia mipango yake ya kumuelekea Mungu wake, isipokuwa waja wema ambao watakuwa wameshikamana na baadhi ya mambo ambayo kwa huyo Ibilisi yatakuwa ni kizuizi cha kuwakalia njiani.

Hii inamaanisha kwamba katika maisha ya mwanadamu, siku zote kuna kitu ambacho kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba mwanadamu hafikii yale malengo yake ya kuwa karibu na Mungu wake, na badala yake anakuwa ni mshirika wa karibu kabisa na yale yatakiwayo ni kitu hicho.

Si kingine zaidi ya Ibilisi, Ibilisi ambaye tukirejea historia yake tunakuta kwamba alikuwa ni kiumbe mwenye kuabudu zaidi ya viumbe wote, Ibilisi ambaye mpaka akafikia hatua ya kupewa jina la Baba wa kusujudu kutokana na wingi wa kusujudu kwake, lakini ndie ambaye leo hii kila mmoja wetu anamlaumu kutokana na kazi yake ya kupoteza watu na kuwatoa katika njia aitakayo Mwenyezi Mungu mtukufu.

Hayo yote yanaweza kuwa ni hatua ya kwanza katika kuelekea katika jambo ambalo tunataka kulizungumzia katika nafasi hii, hata ambayo inafuatiwa na hatua za kujua n i namna gani tunatakiwa kujidhatiti katika kupambana na adui huyu. Ndio, kwa sababu hakuna njia ya kwanza katika kila tatizo zaidi ya kulijua kwanza tatizo hilo na kisha ndio kujua ni njia zipi zitumike katika kulitatua.

Njia za Ibilisi:

Kama ilivyo kwa kila adui, huwa hasemi ni njia gani ambayo ataitumia katika kukuangamiza, kwa sababu itakuwa rahisi kwako kuweza kujitambua na hatimaye kujua ni namna gani ya kujikinga naye na hata kumshinda. Hivyo ndivyo tunakuta kwa adui huyu ambaye ni adui wa kila mtu, kwani tukirejea katika Quran tunakuta tu ahadi zake mbele ya Mwenyezi Mungu kunako kuwakalia wanadamu atika njia zao na kuwapoteza bila ya kusema ni njia gani atazitumia, na hata kama atataja ni njia gani basi si kwa namna ambavyo atatumia njia hizo.

Quran inasema:

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ

ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyo Nyooka.

Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao, na wengi wao wala hawatakuwa wenye kushukuru.[1]

Kwamba kwakuwa ameshajua ni mpotevu, basi anajitahidi kufanya juu chini kwamba asiwe peke yake katika kundi hilo, bali ni lazima awe pamoja na wengine wenye kushirikiana naye.

Jambo la muhimu hapa ni kwamba hakuna mwenye kujitapa kwamba anajua njia za Ibilisi katika kupoteza waja wa Mwenyezi Mungu, ikiwa bado hujajuzwa na Mungu mwenyewe kunako njia hizo, na ndio maana siku zote tunaomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba atujaalie tuweze kuepukana na Ibilisi huyo.

Mwenyezi Mungu kutokana na mapenzi yake, amekuwa siku zote akituhasa kuepukana na mambo ambayo yeye anayajua fika kwamba ni njia za Shetani katika kuwapoteza waja wake, lakini sisi wanadamu kutokana na ukaidi au nafsi zetu kutokubali tuambiwayo tumekuwa tukipinga na kukataa nasaha hizo. angalia leo hii Mwenyezi Mungu anapotuambia kwamba mali na watoto wetu ni Fitina na mtihani mkubwa, ni wangapi ambao tunakubali hili kimatendo na kuamua kufanya kwa mujibu wa Mungu atakavyo?, ni wachache sana kati yetu, bali tunakubali katika ndimi zetu tu, ila linapokuja swala la kufanyia kazi bado wengi tunafeli.

Hakuna sababu kubwa ambayo inatufanya tuweze kukataa na kutokubaliana na anayotuambia Mungu zaidi ya kwamba nasaha zote ambazo tunapatiwa zinakuja katika kuachana na mambo ambayo ni vipenzi vyetu, mambo ambayo ndio vitulizo vya nyoyo zetu, jambo ambalo ni gumu kuweza kukubaliana nalo kimatendo.

Lakini ni lazima tukubali kwamba katika hayo mambo ambayo ni mazuri kwetu, ndimo ambamo Shetani ameweka kamba zake na mitego yake.

Angalia leo hii kuna watu ambao wamefikia hatua ya kuabudu mali bila ya wao kujijua, ndio ni kuabudu!, kwa sababu inapofikia hatua ya kuona mali ndio lengo lako la mwisho katika maisha yako, na wala sio njia tu ya kukufikisha karibu na Mungu wako, bado tu kuna shaka kwamba utakuwa unaabudu mali?.

Angalia leo hii ni wangapi jambo la kutafuta mali linavyowapeleka puta mpaka kufikia hatua ya kuacha ibada zao za swala hasa nyakati za mchana tena bila ya udhuru, kwa kigezo tu cha kwamba muda huo yupo katika kutafuta riziki yake. Achilia mbali huyo wa baadhi ya swala zake, bali kuna ambao wamemaliza ujana wao katika kutafuta mali hizo huku wakiweka mbali upande wa Ibada wakiwa na matumaini kwamba wakishafikia uzee ndipo wataanza kumrudia Mungu kiibada.

Hii ni baadhi ya mifano tu ya kuweza kuonyesha namna gani Shetani anaitumia vyema njia ya mali zetu bila ya sisi kutambua, kwa maana kwanza ni jambo ambalo wanadamu tunalipenda, pili tumekuwa tukiona kwamba ni jambo ambalo Mungu analipenda kwa kila mja, kwani kutafuta riziki ya halali ni jambo lenye kusifiwa. Lakini tukumbuke kwamba hiyo ndiyo maana ya kauli ya Shetani pale aliosema atawapambia waja wa Mungu yale ambayo ni mabaya wayaone ni mazuri, kama ambavyo pia tukumbuke kwamba swala la kutafuta riziki huja baada ya kuongea na huyo mwenye riziki.

Njia nyingine ambayo Shetani amekuwa akiitumia sana katika kuwavuta waja wa Mwenyezi Mungu ni njia ya watoto na vizazi, akiwa na maana kwamba ukaribu wa mwana kwa mzazi unaweza kuwa silaha kubwa sana katika kutengeneza ukaribu wa mzazi na Shatani, au hata ukaribu wa Shatani na mtoto yule.

Na hili pia tunaweza kuliona katika maisha yetu ya kila siku, pale tunapoona kwamba mzazi anamtii mtoto wake na kuacha kumtii Mungu wake, kisha tu kutaka kulinda mapenzi na ukaribu wa kifamilia au kiukoo zaidi.

Hizi ni baadhi tu ya mambo ambayo tumeweza kuyajua, si kwa uwezo wetu kama wanadamu, bali ni kutokana na kurejea maneno ya Mwenyezi Mungu mtukufu pamoja na kudurusu maisha ya kila siku hasa baada ya kuona athari za mambo ambayo tumekuwa tukishikamana nayo.

Tumuombe Mwenyezi Mungu atuweke mbali na wasiwasi za Shetani na vitimbi vyake, na atubakishe katika njia yake iliyonyooka.



[1] Surat Aaraf aya 16 - 17


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: