bayyinaat

Published time: 23 ,September ,2018      11:22:19
News ID: 345

Miongoni mwa mambo ambayo yamepewa kipaumbele zaidi katika dini ya Uislamu ni swala la kuamrisha mema na kukataza maovu. Si tu kupewa kipaumbele bali tunakuta pia moja ya mambo yaliyofanya umma wa Mtume Muhammad kuwa bora kuliko umma nyingine ni kwa kuwa tu wanashikamana na jambo hili.

Mwenyezi Mungu anasema katika Quran tukufu:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ

"……Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu.....”.

Kwamba jambo la kuamrishana mema na kukataza maovu ni katika mambo ambayo yamepelekea umma wa Mtume Muhammad kuwa ni umma bora kuliko umma zote.

Na hata ukirejea tena katika Quran tukufu utakuta kwamba kuna umma ambazo zilikuwa na mwisho mbaya kama si kulaaniwa kabisa na Mwenyezi Mungu (swt), kwa sababu tu hawakuwa wakisimamisha jambo hili la kuamrishana mema na kukatazana maovu.

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ (78) كَانُوا لَا يَتَنَاهَوْنَ عَن مُّنكَرٍ فَعَلُوهُ ۚ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

"....Walilaaniwa walio kufuru miongoni mwa Wana wa Israel kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Mariamu. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapindukia mipaka. Walikuwa hawakatazani maovu waliyo kuwa wakiyafanya. Hakika ni maovu yalioje mambo waliyo kuwa wakiyafanya......”

Hii yote inaashiria uzito na umuhimu wa jambo hili kwa kiasi kwamba kuna ambao wanapanda daraja na kuna ambao wanashuka daraja kwa kulifanya au kulipuuzia na kuachana nalo.

Lakini ni lazima tutambue kwamba swala zima la kuamrisha mema na kukatazana maovu linaweza kuwa katika sura mbalimbali, kuna wakati unatimiza jukumu hili kwa mtu ambaye mnalingana nguvu kiasi kwamba unaweza kummudu na kumfikishia yaliyo sahihi. Lakini kuna wakati inakuwa la, bali unakutana na mtu ambaye amekuzidi nguvu kiasi kwamba inaweza hata kupelekea maisha yako kuwa hatarini endapo tu utathubutu kuinua mdomo wako au kuonyesha kwamba huridhiki na atendayo.

Bila shaka katika hali ya kwanza hakuna shaka kwamba kuna uwezekano wa kufanikiwa kwa kiwango kikubwa mno kwa sababu tu mazingira ya kufanya hivyo yanakuwa tayari yameshaandaliwa, tatizo linarudi katika sura ya pili, kwa maana ya kwamba hakuna njia nyepesi ya uweza kufanya hivi, sasa ni upi wadhifa wetu katika hali kama hii?, tuachane na jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu? Au nini kifanyike.

Katika masiku haya matukufu ya mwezi wa Muharamu tunaweza kupata mafunzo ya aina mbalimbali kutoka kwa Imamu Hussein (as) ambaye ni baba wa wapigania uhuru wote ulimwenguni, Imamu ambaye ndiye atakayetupatia jibu la nini kifanyike katika mfano wa mazingira ya pili, mazingira ambayo unakabiliana na ambaye amekuzidi nguvu katika harakati zako za kuamrisha mema na kukataza maovu.

Nasema hivi nikiwa na maana kwamba endapo tutarejea katika historia ya Uislamu basi tutakuta ipo wazi kabisa kwamba Imamu Hussein hakuwa na lengo ambalo linapingana na jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu. hayo tunaweza kuyakuta katika maneno yake matukufu aliyotamka wakati anaanza safari yake ya kuelekea Karbala ambapo alisema:

إني لم أخرج أشراً ولا بطراً ولا ظالماً ولا مفسداً انما خرجت لطلب الاصلاح في امة جدي

"....Sikuwa ni mwenye kutoka kwa ajili ya kutafuta shari wala ukubwa wala dhulma wala uharibifu katika ardhi, bali nimetoka kwa ajili ya kutafuta suluhu katika umma wa babu yangu (saww), nataka kuamrisha mema na kukataza maovu..........”

Akiwa na maana ya kwamba pamoja na ukubwa wa adui bado kuna kila haja ya kuamrisha mema na kukataza maovu.

Maovu ambayo yamenukuliwa na historia ya Uislamu kwa njia mbalimbali, kufikia kiwango kwamba watu wa zama ile hawakuwa wakijua thamani ya dini ambayo Mtume alihangaika nayo kwa miaka mingi kuiweka sawa, watu ambao walikuwa tayari wamesharidhika kutawaliwa na kiongozi wa aina yeyote yule kwa jina la khalifa wa Waislamu, hivyo ipo wazi kwamba jambo la kukataza mabaya lilikuwa ni la wajibu.

Kujitoa ndio njia pekee katika hali kama hii

Tumesema kwamba katika sura ya pili pamoja na kuwa yule unayekabiliana naye anakuwa na nguvu zaidi yako, haina maana kwamba jambo la kukataza mabaya linakufa. Bali ni vyema tukajifunza kutoka kwa Imamu namna ya kufikisha ujumbe kwa upande wa namna hii.

Imamu pamoja na kutambua kwamba kwa vyovyote hawezi kubakia baada ya kutoka kwake, lakini bado alitoka kwa ajili ya kukabiliana na watu waovu. Hii inaashiria kwamba kujitoa kwako katika kupambana na dhalimu ambaye anaeneza uovu katika ardhi si lazima kufikiwe malengo yake kwa njia ambayo wewe umeshaiandaa, kwamba utamwambia ataelewa na ataachana na maovu, bali kuna wakati mwingine unahitajika kuwa chambo, kuwa mwanzilishi ambaye atawazindua watu kwamba ni kweli kuna ubaya na uovu unaendelea na kuna ulazima wa kupambana nao.

Hivyo njia pekee ya kukabiliana na dhalimu ambaye anaeneza uovu ni kujitoa katika hilo.

Tumalizie na maneno ya Imamu Hussein alipokuwa akiwaadhi watu siku ya Ashura, wakati ambao anajua kwamba hawa anaopambana nao kila mmoja ana lengo lake, kuna ambao wanatamani malipo ya fedha, kuna ambao wanatamani mamlaka nk.

Imamu alisema :

"......Hebu chukueni mafunzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu namna ambavyo alikuwa akiwasema vibaya viongozi wa Kiyahudi kutokana na kuacha kwao kukataza maovu, angalia namna ambavyo wana wa Israel walilaaniwa kupitia ndimi za Nabii Daud na Issa (as), hii yote ni kwamba walikuwa wakiona watu wenye kueneza maovu bila ya kuwakataza, na hasa pale ambapo kulikuwa na wenye kutamani na wao siku moja wawe kama wao kwa nafasi zao.......”

Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe ni wenye kuamrishana mema na kukatazana maovu ili tuweze kuwa katika ambao wanakusanywa na rehema zake.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: