bayyinaat

Published time: 25 ,September ,2018      21:29:07
Jambo la pili ambalo ni msingi wa kufanya mapinduzi ya Imamu Husein kubakia daima katika nyoyo za watu, ni kwamba yalikuwa yamepangika katika mfumo wa kuendana na maumbile au asili ya mwanadamu.......
News ID: 346

Katika mambo ambayo tunaweza sema ni msingi wa ubakiaji wa historia ya Uislamu mpaka sasa na swala zima la Ashuraa, Mwezi kumi Muharamu (mfungo 4), siku ambayo kuna watu ambao walikuwa katika hali ya kuteseka kwa kiu na njaa, watu ambao mikuki na mishale ndio ilikuwa mahala pake, watu ambao hata baada ya kufa kwao bado farasi na punda wakaamriwa kuwakanyaga na kuwaponda, watu ambao laiti kama ungaliwaona basi usingeweza kutofautisha baina yao na mchanga ama udongo, watu ambao naweza kusema walitoa kila kilicho chao kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watu wa baada yao wanaishi maisha ambayo Mwenyezi Mungu anayataka, watu ambao mbali na wanahistoria kuficha uhalisia wake lakini bado tunakuta kwamba historia inawahifadhi na kuwabakisha milele katika nyoyo za watu, sizungumzii wengine hapa mbali na mashahidi wa tukio zima la Ashura.

Naam, hii ndiyo sifa ya mashahidi, kujitolea kwa ajili ya maisha ya wengine, bila shaka katika hili walistahiki kutunukiwa na mola wao zawadi ya kubakia hai milele mbele yake, tena wakiwa katika hali ya kuruzukiwa na mola wao. Kama ambavyo walikuwa na kila haki ya kubakia hai katika nyoyo zetu kadri ambavyo tutaendelea kubakia, na ndio maana tunasema kwamba kuhuisha tukio la Ashura ni sawa na kuhuisha uwepo wetu.

Unaweza kushangaa ni kwanini tukio la Ashuraa pamoja na kupita kwa miaka mingi tangu kutokea kwake, bado linaonekana na bichi kila siku, na huku likiendelea kusambaa ulimwenguni kote?, jibu ni jepesi sana katika hilo, jaribu kurejea namna ambavyo tukio hilo lilikuwa, na ni jinsi gani limebeba mambo ambayo ni nadra sana kutokea katika maisha ya wanadamu, na hii ndio sababu kubwa iliyopelekea kubakia na kuenea kwa tukio hili.

Mbali na hilo, kuna baadhi ya mambo mengine ambayo endapo tutadurusu tukio la Karbala na Ashura kwa ujumla tunaweza yaona, mambo ambayo pia ni msingi wa kubakia milele kwa tukio hili adhimu.

1. Ashuraa ni mapinduzi ya kutafuta usuluhishi, na si mageuzi

Kuna haja ya kufahamu tofauti kubwa iliyopo baina ya mapinduzi na mageuzi ya kutafuta suluhu na mapinduzi au mageuzi ya kutaka tu kuleta utofauti. Imamu Hussein mpaka anafikia kutoka hakuwa na lengo tofauti na kutaka kuleta suluhu katika umma wa babu yake, na hakutoka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Yazid anatoka madarakani labda kwa kuwa muda wake umeisha au hakutakiwa kukaa pale.

Na hapa ndipo utagundua tofauti inayopatikana endapo tu utagundua kwamba Imamu Hussein (as) hakuwa amemkusudia Yazid kama Yazid, bali alikusudia Wanadamu kwa ujumla kwamba popote watakapokuwa basi ni lazima wawe na sifa ya kusimamisha ukweli na kuachana na dhulma na uonevu.

Nitapenda kufananisha mapinduzi ya Imamu Hussein na Atom (Dharra) ambayo inaweza kuwa ndogo kimtazamo wa kawaida, lakini punde tu inapotoka katika umbile lake na kuamua kulipuka ni namna gani ambavyo itashangaza wengi kwa ukubwa wa athari zake.

Kama ambavyo pia inatakiwa tutambue kwamba mapinduzi ya aina hii hayawezi kupimwa kwa nyakati bila nyakati nyingine, bali popote ambapo mazingira yatakuwa ni munasibu kwa ajili ya kupatikana kwa mapinduzi haya bila hata ya kuambiwa au kuandaliwa na mtu ni lazima yatatokea tu.

Na ndio maana kuna baadhi ya wanaharakati wanasema kwamba mapinduzi ya kweli hayawi ni kwa watu wa aina fulani bila ya watu fulani, huwezi kusema kwamba mapinduzi ya kweli yanamuhusu Mwislamu tu bila ya Mkristo au Yahudi, au hata asiyekuwa na dini, kwa sababu kuna wakati jambo ambalo linakusanywa na mapinduzi linakuwa ni jambo lenye kugusa watu waa aina zote na rika zote na dini zote, mfano wa mapinduzi hayo ni mapinduzi ya Imamu Hussein (as).

Angalia namna ambavyo mapinduzi ya Karbala yalivyoweza kuathiri watu mbalimbali bila ya kujali dini zao wala itikadi zao, angalia India mpaka wanafikia kupata uhuru wao na namna ambavyo Mahatma Ghandhi amejifunza kutoka katika tukio la Ashura na Karbala kwa ujumla. Angalia namna ambavyo Imam Khomeini alivyoikomboa Iran kutoka katika utawala wa Shah na kusimamisha Jamhuri ya Kiislamu badala yake.

Hii ni baadhi tu ya mifano katika kuonyesha kwamba mapinduzi yanapokuwa na lengo la usuluhishi basi hayawezi kuzuiliwa na mipaka ya aina yeyote ile, na hivyo ndivyo ilivyokuwa katika mapinduzi ya Imamu Hussein (as), na hiyo ndiyo sababu ya kwanza ya kufanya mapinduzi haya kubakia milele.

2. Mapinduzi ya Imamu Hussein yalikuwa ni yenye kuendana na asili ya mwanadamu

Jambo la pili ambalo ni msingi wa kufanya mapinduzi ya Imamu Husein kubakia daima katika nyoyo za watu, ni kwamba yalikuwa yamepangika katika mfumo wa kuendana na maumbile au asili ya mwanadamu.

Ndio, hatuwezi kusema kwamba hayakuwa katika msingi wa kulinda dini au kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt), bila shaka lengo hilo lipo na wala pia halipingani na hili ambalo tunalieleza katika nukta hii. Kwa maana dini ya Uislamu siku zote si yenye kupingana na maumbile ya mwanadamu, bali zinaendana na zinatembea katika mrengo mmoja.

Nukta hii ambayo naiashiria hapa tunaweza kuikuta katika mazungumzo ya Imamu Hussein (as) katika uwanja wa Karbala, baada ya kuona kwamba ameshatoa hoja zote kwa maadui na kuwakumbusha kuwa walifanyalo haliendani kabisa na ayatakayo Mwenyezi Mungu. Imamu alisema "......Ikiwa kama hamtakuwa watu wenye dini na si wenye kuogopa siku ya malipo basi kuweni huru katika hii dunia yenu....”

Hili ni jambo ambalo huwezi kulikuta katika kila mapinduzi yanayotokea, kwa maana ya kwamba mapinduzi yenye kubakia siku zote katika nyoyo za watu ni lazima yawe na msingi kama huu, Mahatma Ghandhi baada ya kutekeleza kazi kubwa ya kuliokoa taifa la India anasema ".....Nimeyasoma kwa kina sana maisha ya Hussein (as), na kuliangalia sana tukio la Karbala, nikafikia katika natija ya kwamba kama nikitaka kufikia katika malengo na ushindi basi sina budi kujifunza kutoka katika mwenendo wa maisha ya Hussein (as)....”

Kwa maana ya kwamba ili mwanadamu uweze kufikia katika malengo ambayo unayafikiria kwa ajili ya wengine, ni lazima kabla ya kusimamia jambo lako uweze kuhakikisha kwamba jambo hilo halipingani na asili ya kimaumbile ya wanadamu, kwa maana nyingine halipingani na akili za kawaida za wanadamu.

3. Lengo kubwa ni kutetea dini ya Mwenyezi Mungu na si dunia

Hii ni dalili ya tatu katika kuashiria kwamba mapinduzi ya Imamu Hussein hayakubakia tu bila ya kuwa na misingi, bali kuna misingi ambayo iliandaliwa mpaka kuwa katika hali tunayoiona leo.

Angalia mapinduzi mengi ambayo yametokea katika ulimwengu huu, ima yawe ni mapinduzi ya kukomboa nchi au mambo mengine, utakuta kwamba kila baada ya muda mapinduzi yale yanapoteza nguvu kama si kusahaulika kabisa. Kwa sababu katika dini ya Uislamu tuna msingi wenye kusema kwamba yale ambayo huwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu basi hubakia na kudumu, lakini kama hayatakuwa kwa ajili yake basi hufa na kupotea.

Imamu mpaka kuamua kutoka haikuwa tofauti na malengo ambayo Mwenyezi Mungu anayataka, bali alikuwa katika njia ya kuyatetea yale ambayo Mungu anayataka.

Mwandishi mmoja kutokea Uingereza kwa jina la Charles Dickens anaandika "....Ikiwa huyu Hussein alikuwa amepigana kwa ajili ya dunia bado nitakuwa sijaelewa kwanini akaamua kutoka na wanawake na watoto zake, na ndio maana akili salama itahukumu kwamba hakuwa na lengo tofauti na Uislamu tu....”

4. Aina ya mwenye kuleta mapinduzi

Jambo lingine ambalo linayapa uzito mapinduzi ya Karbala na kufanya yabakie milele na milele ni aina ya mtu ambaye amesimamia hayo mapinduzi.

Ndio, bila shaka ili watu waweze kuyapa uzito mambo yako bila shaka watakuangalia wewe mwenyewe kwanza kabla ya kufanya hivyo, ni nani asiyejua uzito na nafasi aliyokuwa nayo Imamu Hussein kuanzia zama za Mtume (saww) mpaka anachukua shahada yake?.

Hivyo nafasi aliyokuwa nayo, uzito aliokuwa nao, ni katika mambo ambayo yamefanya mapinduzi yake kuchukua uzito na nafasi kama aliyokuwa nayo.

Hizi ni baadhi tu ya nukta ambazo zinaashiria sababu iliyopelekea mapinduzi ya Imamu Hussein kubakia milele na kuwa mpya kadri masiku yanavyosonga.

Ila jambo la muhimu pia ambalo tunaweza kujifunza katika mapinduzi haya ni kwamba tukio la Ashura lilikuwa na lengo la kufikisha mafunzo kwa wanadamu wote, hasa katika kuelewa umuhimu wa utu na nafasi yake.

Maurice Bucaille, mmoja wa Madaktari bingwa kuwahi kutokea nchini Ufaransa anasema ".......Nasikia katika majlisi za kumkumbuka Hussein ya kwamba alijitoa kwa ajili ya kulinda heshima na sharafa za watu pamoja na kuhifadhi Uislamu kwa ujumla, basi nasi tuchukue mfano wake ili tuweze kujikomboa na huu ukoloni......”

Kama ambavyo pia mapinduzi ya Imamu yanatufunza kwamba mwanadamu anaweza kubadilika, bila ya kujali yupo katika hali gani.

Na mabadiliko haya sawa yawe ni kwa mtu mmoja mmoja kama ambavyo imetokea katika uwanja wa Karbala ambapo Hurr pamoja na kusimama katika nafasi kubwa ya kumzuia Imamu na kumzingira, aliweza kubadilika na kujiunga na Imamu. Au la, inaweza kuwa ni mabadiliko ya wengi na mpaka umma mzima.

Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe ni wenye kujifunza mengi kutokana na tukio la Ashura, kama ambavyo atujaalie tuwe ni wenye kuyafanyia kazi hayo ambayo tutajifunza. Amin.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: