bayyinaat

Published time: 02 ,October ,2018      21:02:03
Miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameikirimu dini ya Kiislamu kwayo, ni swala zima la kumpa thamani mwanamke wa Kiislamu pamoja na kumlinda dhidi ya mambo yasiyomfaa ikiwa ni pamoja........
News ID: 351

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na Mwenye kurehemu

Sifa zote njema ni za kwake Mwenyezi Mungu mola wa walimwengu wote, pia sala na salamu zimfikie Mtume wetu Muhammad (saww) pamoja na kizazi chake na masahaba zake walio wema.

Miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameikirimu dini ya Kiislamu kwayo, ni swala zima la kumpa thamani mwanamke wa Kiislamu pamoja na kumlinda dhidi ya mambo yasiyomfaa ikiwa ni pamoja na kumuwekea misingi ambayo ikiwa kama atashikamana nayo basi mwanamke huyu siku zote atakuwa katika ulimwengu wa amani na mafanikio ya kimungu.

Nasema hivi hasa baada ya kukumbuka namna ambavyo Mwenyezi Mungu kupitia Quran yake, ameshusha aya mbalimbali zenye kuwafunza wake wa Mtume namna ya kuamiliana na watu, wake za Mtume ambao ndio kiigizo chema kwa wanawake wa umma huu, au tunaweza kusema kwamba yale ambayo yameshushiwa kwao miongoni mwa mafundisho basi pia yanawahusu wanawake wote.

Mwenyezi Mungu anasema katika Quran tukufu:

http://www.iium.edu.my/deed/quran/arabic/33_32.gif

Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.[1]

Kwamba ikiwa wake za Mtume wataamua kutulia na kuwa wachamungu, basi hakutakuwa na mwanamke yeyote yule atakayekuwa mfano wao, kwa maana uchamungu na kufuata ambayo Mungu anayataka ndio kigezo na alama ya kuwa bora kuliko mwingine.

Na miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyaelezea kwao kuwa ni moja ya mambo yatakayoashiria uchamungu wao, ni swala zima la kuchunga sauti zao mbele ya wasiokuwa waume zao, kutolegeza sauti zao mbele yao, kwa maana jambo hilo linaweza kuleta madhara makubwa kama vile kuamsha hisia za upande wa pili na kupelekea kutenda haramu.

Katika uwanja wa leo sitaki kuashiria mambo ambayo mwanamke wa Kiislamu anatakiwa kuyafanya ili awe mchamungu, bali kubwa hasa ni kutaka kutumia aya hiyo hapo juu na kujaribu kuashiria namna ambavyo mwanamke wa Kiislamu anaweza kuathiri upande wa pili, athari ambayo inaweza kuwa ni kama ambayo Mwenyezi Mungu ameiashiria katika haya, au athari ambayo itapelekea upande wa pili kuwaza na kufikiria au hata kujua uhakika wa mwanamke huyu.

Nasema hivi nikiwa nalenga kwamba kuna wakati ili kuweza kumtambua mtu unahitajia moja kwa moja akwambie mwenyewe kwamba yeye ni wa aina gani, na kuna wakati mwingine unamfahamu mtu kupitia watu zake wa karibu, kama ambavyo kuna usemi maarufu wenye kusema "Nitajie rafiki zako nikwambie tabia yako”, lakini kuna wakati mwingine mwonekano wako tu unatosha kuashiria kwamba wewe ni mtu wa aina gani, na hili ndilo ambalo nataka kuliashiria katika makala hii.

Kama ambavyo pia kutokana na aya hiyo hapo juu tunaweza kugundua kwamba si njia ya sauti peke yake ndio inaweza kuleta madhara au athari kwa upande wa pili, bali pia upo uwezekano wa kuwepo kwa njia nyingine zenye uwezo huo, kama vile njia ya mavazi ambayo ndio nitakwenda kuiashiria katika sehemu hii.

1. Mavazi ya Mwanamke huakisi shahsia yake

Katika ulimwengu wa leo ni jambo lililowazi sana kusikia kwamba wanawake wanashindana kila kukicha kwenda na wakati hasa katika swala zima la mavazi na urembo, huku kila mmoja wao akiwa na lengo la kuonekana mzuri na mwenye kwenda na wakati.

Kwa maana ya kwamba jambo ambalo linazunguka katika akili za wanawake linapokuja swala la kwenda na wakati au kupendeza ni kuonekana mrembo na mzuri mbele ya wengine tu, wakati ambao kuna swala lingine la muhimu ambalo pia ilibidi lifikirike, lakini kwa masikitiko makubwa mno limekuwa likisahaulika kwa wanawake wengi mno.

"Shakhsia” au tuite "Uhalisia na Uhakika” wako, ndio jambo la muhimu ambalo limesahaulika. Nikiwa na maana kwamba kama ambavyo inafikirika kuwa kuvaa vizuri ndio ishara ya uzuri na urembo, basi pia mavazi hayohayo ni ishara ya wewe ni nani ambaye upo ndani ya mavazi hayo.

Mtafiti mmoja wa maswala ya Saikolojia kutoka Pakistan Dk Hassan Muhammad Ally, ameandika katika moja ya tafiti zake kwamba kuna uhusiano mkubwa sana baina ya mavazi na mwenye kuyavaa, uhusiano ambao unaweza kutujuza hali ya kinafsi aliyonayo mvaaji yule, mbali na urembo ambao unadhihirika.

Katika kuendana na hilo jarida maarufu nchini Dubai na Lebanon "Sayidaty” lilichapisha rai kadhaa za vijana ambao asilimia 68 kati yao walikiri kwamba mwanamke mwenye kuvaa mavazi ya kujiheshimu basi huashiria kwamba ni mwanamke ambaye ana tabia za juu na nzuri pia. Kama ambavyo pia kuna baadhi ya wanaume ambao walikubali kwamba mwanamke ambaye amejihifadhi basi anakuwa anavutia zaidi kuliko ambaye kajiacha wazi, kwa maana jambo ambalo limefichwa ndio lenye thamani ya kuwa nalo zaidi kuliko jambo ambalo lipo wazi.

Hii yote ni kuonyesha kwamba mavazi ya mtu ni mkalimani sahihi wa tabia za aliye ndani ya mavazi.

Itaendelea....

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal.



[1] Surat Ahzab aya 32


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: