bayyinaat

Published time: 02 ,October ,2018      21:06:36
Hivi ndivyo ambavyo mavazi hutumika na watu wenye akili salama, kwamba huyatumia kuangalia aliye ndani ya mavazi yale, na mavazi huwa ni kama njia tu. Sawa mavazi yanaweza kuwa mazuri sana............
News ID: 352

1. Mavazi ni kioo

Ndivyo ambavyo tunaweza kusema kwa haraka, au ndivyo ambavyo tunaweza kufananisha mavazi na kioo, kioo ambacho tunatumia muda mwingi sana kukiangalia, lakini hakuna hata mmoja ambaye utamuuliza unaangalia nini akakwambia anaagalia kioo, bali atakwamba anajiangalia yeye.

Hivi ndivyo ambavyo mavazi hutumika na watu wenye akili salama, kwamba huyatumia kuangalia aliye ndani ya mavazi yale, na mavazi huwa ni kama njia tu. Sawa mavazi yanaweza kuwa mazuri sana, ila haina maana kwamba na wa ndani yake pia ni mzuri.

Nasema hivi nikataka kusema kwamba mavazi ya mwanamke hasa, maana ndie ambaye tunamzungumzia kwa leo ni njia ya kumtafsiri mwanamke yule, na hii ni kutokana na misingi ya Saikolojia.

Mwalimu wa chuo kimoja cha Saikolojia nchini Misri Dk Muhammad Sayid Khalil, anaadika na kusema kwamba mwonekano wa mwanamke si tu ni ishara ya urembo wake kama ambavyo wengi wanadhani, bali pia ni ishara na huakisi hali ya kinafsi inayopatikana kwa mwanamke mwenye kuvaa mavazi hayo, na hii ni kutokana na misingi mitano muhimu katika elimu ya saikolojia. Misingi yenyewe ni kama ifuatavyo:

1. Msingi wa matamanio

Miongoni mwa mambo ambayo kila mwanadamu ameumbwa nayo ni matamanio, matamanio ambayo tunaweza kuyadhibiti au yenyewe yakatudhibiti.

Matamanio ya kutamani kuonekana mrembo mbele ya kila mmoja ni jambo ambalo linapatikana kwa kila mwanamke, lakini linapokuja swala la kufaa kwa jambo hilo au la ndipo tunapohukumu kwamba mwanamke huyu amefanikiwa au la?.

Bila shaka dini tukufu ya Kiislamu haijaacha mwanamke awe ni pambo kwa kila mwenye macho, bali ni pambo kwa macho ya yule ambaye ameruhusiwa kisheria kupambika naye. Kwa mantiki hii basi, endapo ukaona mwanamke ameachia maungo yake mbele ya wote basi tambua kwamba mwanamke huyo ameshindwa kudhibiti matamanio yake, jambo ambalo limepelekea kufeli katika kutekeleza jambo stahiki katika dini. Na endapo ukaona mwanamke ni mwenye kujisitiri ila kwa ambao ameruhusiwa kutofanya hivyo, maana yake ni kwamba huyu ameweza kudhibiti matamanio yake na hivyo amefaulu katika ambayo dini yake inamtaka kuyatimiza.

2. Akili ya muhusika

Bila shaka miongoni mwa mambo ambayo mwanadamu amekirimiwa nayo na kumfanya awe tofauti na wanyama wengine ni kupewa kwake akili.

Akili ambayo humfanya awe na uwezo wa kupambanua mambo na kuweka kila moja katika nafasi yake na kwa wakati wake.

Hivyo basi kwa kupitia mavazi tunaweza kuhukumu nguvu ya akili inayopatikana kwa muhusika, kama ambavyo tumeweza kutambua nguvu yake ya kudhibiti au kudhibitiwa na matamanio yake.

Kwa maana ya kwamba akili ya muhusika kama itakuwa salama basi atakuwa ni mwenye kushikamana na mavazi yanayohitajika na kila mmoja, na hatakuwa mwenye kuvaa mavazi yatakayoonyesha maungo yake na kupelekea watu wengine kuhukumu mambo mbalimbali.

3. Kujali au kutojali kwa muhusika

Ndio, kupitia mavazi tunaweza tambua ukubwa wa nguvu ya kujali au kutojali kwa muhusika.

Tumezoea kuona wanawake wengi ambao wanavaa mavazi yasiyo stahili, wakisema kwamba wanachojali wao ni maisha yao na jinsi ambavyo wao wanapenda kuishi, na si kwamba watu wengine wanasema nini. Lakini cha ajabu ni kwamba wakati ambao wanavaa mavazi hayo wanasubiria kwa watu mitazamo yao na namna ambavyo watu wale watahemuka na mavazi yao.

Hivyo kama mtu atakuwa ni mwenye kujali mitazamo ya watu basi hawezi kuvaa nguo ambazo zitapelekea watu kuhukumu vibaya kuanzia nje mpaka undani wake. Lakini kama hatokuwa ni mwenye kujali basi atajiamulia lolote bila kuangalia kwamba nini kitatokea, muhimu ni kwamba ajue kuwa kupitia kitendo chake hicho watu wanaweza kujua ukubwa wa nguvu yake ya kujali au kutojali.

4. Hofu au ushujaa

Ni mambo mawili ambayo yanaweza kutafsiriwa kwa maana nyingi mno, miongoni mwa maana zake n i pale ambapo mtu anakuwa na hofu ya kuonekana hana tabia njema, jambo ambalo bila shaka ni katika ukamilifu wa binadamu

Lakini wakati mwingine mtu kutojali au kutokuwa na hofu ya kuonekana hana tabia njema huona kwamba ni ushujaa kwa sababu tu anaona ameweza kufanya kile ambacho nafsi yake inataka, bila kukumbuka kwamba kuna njia ambazo Muumba wetu anataka tupite.

Kwa vyovyote vile, muhimu ni kwamba kupitia mavazi ya mwanamke tunaweza kutambua kwamba fulani ana hofu katika kufikia ukamilifu, na huyu ni yule ambaye atakuwa ni mwenye kujiheshimu na kujilinda. Ama yule ambaye anaona ushujaa kuvaa kama atakavyo yeye, na kuona kwamba ni ushujaa basi bila shaka atakuwa hana ile hofu ambayo kila mwanamke anatakiwa kuwa nayo, hofu ambayo endapo mwanamke atakuwa nayo anahesabika ni mwenye kukamilika.

5. Heshima

Jambo la mwisho na ambalo karibuni kila mwenye nafsi hupenda kuonekana nalo ni jambo la heshima.

Nalo pia tunaweza kulitambua kupitia mavazi ya muhusika, kwamba je mtu huyu anajali heshima yake, na kweli hiyo heshima anayo au la?.

Mwenyezi Mungu ajaalie wake, ndugu na wa karibu wetu wawe ni wenye kushikamana na mavazi ambayo Mwenyezi Mungu ameyataka, mavazi ambayo hayatakuwa sababu ya wengine kuhukumu ubaya wa tabia zao au udhaifu wa imani zao. Amin.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: