bayyinaat

Published time: 18 ,November ,2018      12:00:33
Tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiul Awwal ni moja ya siku muhimu katika historia ya Uislamu, Katika siku hii Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwaylid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu.....
News ID: 367

Tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiul Awwal ni moja ya siku muhimu katika historia ya Uislamu, Katika siku hii Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwaylid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu. Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw) Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenzi wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw).

Imani ya Bibi Khadija

Bibi Khadija AS alikuwa mfuasi wa mafundisho ya Nabii Ibrahim AS na alikuwa na ufahamu kuhusiana na Mtume wa Mwisho kupitia vitabu vya dini za kale na kupitia kwa mshauri mwenye hekima na msomi kama Waraqah bin Nawfal. Baada ya ushahidi na sifa mbalimbali kuonyesha kwamba, Mtume wa Mwisho anaweza kuwa ni Muhammad Amin, Bibi Khadija alikuwa na hamu ya kumuona Muhammad. Akiwa na lengo la kumtahini na kumtathmini, alimkabidhi mali zake na kisha kumtuma katika safari ya kibiashara. Aidha katika safari hiyo, alimtuma pamoja na Muhammad mmoja wa mtumishi wake aliyejulikana kwa jina la Maisarah ili atathmini utendaji wake katika safari hiyo.

Kwa hakika Bibi Khadija AS si tu kwamba, aliamini mafundisho yaliyoletwa na Mtume SAW, bali alijitolea pia kwa moyo wake wote kusaidia kueneza mafundisho hayo. Bi Khadija alikuwa akituliza na kupunguza machungu ya Mtume SAW ya kukadhibishwa na kuudhiwa na munafikina. Mtume SAW alifunga ndoa na bibi Khadija akiwa na umri wa takribani miaka 25. Kwa muda wa miaka 24 Bi Khadija alikuwa mwenza na mke wa Mtume SAW. Mtume SAW hakuoa mke mwingine katika kipindi cha uhai wa Bibi Khadija. Baada ya kuaga dunia Bi Khadija, Mtume SAW alioa wanawake wengine kulingana na hekima na sababu mbalimbali na kutoka kwa makabila mbalimbali, hata hivyo hakuna mwanamke yeyote kati ya wake zake hao aliyeweza kujaza pengo la Bibi Khadija. Aidha Mtume SAW hakujaaliwa kupata mtoto yeyote kutoka kwa wake zake hao wengine na hivyo kizazi cha Mtume SAW kuendelea na kubakia kupitia kwa Bibi Khadija.

Kuzaliwa Kwake

Bibi Khadija alizaliwa katika familia ya heshima na iliyokuwa na asili ya Kikureishi. Watu wa familia yake wote walikuwa wakisifika kwa fadhila, kujitolea na kuitetea na kuihami nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba. Bibi Khadija ni binti ya Khuwaylid bin Asad ibn Abd-Al-Uzza. Asad ibn Abd-Al-Uzza ni babu wa Bibi Khadija upande wa baba ambaye alikuwa shakhsia na mtu mahiri katika zama zake. Bibi Khadija binti Khuwaylid AS alikulia na kulelewa katika familia ya heshima na iliyokuwa na mizizi katika Bara Arabu na akachanua katika jamii hiyo. Hata hivyo, hadhi, heshima na utukufu wake haukutokana tu na asili ya familia yake, bali yeye mwenyewe bibi mwema huyo alijipamba kwa sifa njema na kuondokea kuwa mashuhuri kwa mwenendo mwema.

Ndoa ya Bibi Khadija na Mtume (saw)

Ndoa yake na Bwana Mtume SAW haikufanana wala kushabihiana na ndoa nyingine na ndoa yake haikuwa na mithili. Hii ni kutokana na kuwa, ndoa yao hiyo tukufu ilikuwa imejengeka juu ya msingi wa malengo aali na harakati ya Bibi Khadija ya kutafuta fadhila na ukamilifu na katu haikuwa na msukumo au malengo ya kimaada au mapenzi na ladha za kupita. Kwa hakika ndoa ya Mtume (saw) na Bibi Khadija AS ni kiigizo chema cha wanandoa na wale wote wanaoguswa na masuala ya kuijenga jamii na kuifanya kuwa bora na salama.

Itaendelea….

Na Al-Muhtaram Salum Bendera


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: