bayyinaat

Published time: 18 ,November ,2018      12:07:00
News ID: 368

Ukarimu Wake

Kila mhitaji ambaye alikuwa amekata tamaa ya kupata msaada kwa wengine, alikuwa akikata shauri na kuelekea katika nyumba ya Bibi Khadija na kukimbilia katika ngome hiyo ya huba, huruma na mapenzi ambayo ilikuwa ni dafina na hazina ya ukarimu, na kwa baraka za mapenzi ya ukarimu wa bibi mwema huyo, machungu ya maisha ya wahitaji hao yalikuwa yakipata pozo.

Bi Khadija bint Khuwaylid alikuwa akipenda mno kuwasaidia masikinina wenye shida. Kiasi kwamba, njia ya kuelekea nyumbani kwake daima ilikuwa na msongamano wa wahitaji. Bi Khadija alikuwa akiwasaidia wakati wowote ule wa mchana au usiku na kuwafanya warejee walikotoka wakiwa na tabasamu, bashasha na matumaini mapya. Si hivyo tu, bali alikuwa akizungumza nao kwa lugha ya upole na huruma na kusikiliza kwa makini shida na matatizo yao. Alikuwa akifuta machozi ya mayatima na akina mama na kisha kuwaita wafanyakazi wake na kuwataka walete mifuko ya pesa na mchele na kugawa baina ya masikini na wenye kuhitaji.

Heshima na Umashuhuri Wake

Pamoja na ukarimu, kujiheshimu pamoja na umashuhuri, Bi Khadija alifahamika pia mjini Makka kama mwanamke mzuri na mwenye ujamali wa aina yake. Imam Hassan bin Ali al-Mujtaba AS ambaye alikuwa akipigiwa mfano wa ujamali na uzuri wa kidhahiri baina ya Bani Hashim, alikuwa akihesabiwa kuwa mtu aliyefanana sana na Bibi Khadija.

Bibi Khadija aliheshimiwa sana na watu wa Makka kwa sababu ya tabia yake ya kuigwa na uwezo wake wa kupanga mambo. Kama ambavyo watu wa Makka walikuwa wakimuita Muhammad ‘Sadiqul- Amin’, yaani mkweli mwaminifu, walikuwa wakimuita Bibi Khadija ‘Tahira’, yenye maana ya "Aliye safi.” Alikuwa akijulikana pia miongoni mwa Waarabu kama ‘Malkia wa Wafanyabiashara.

Ujamali na uzuri wa Bibi Khadija na ukarimu ulikuwa hauna mithili kiasi kwamba, jamii ya wakati huo ya Waarabu iliyokuwa imezama na kughiriki katika ufisadi na upotofu ilikuwa ikimuita kuwa ni 'Malkia wa Kiarabu'. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana, viongozi wa makabila mbalimbali ya Kiarabu, mashuujaa wa Kikureishi, shakhsia wakubwa wa Bani Hashim, wafalme wa Yemen na viongozi wa Taifa wote walijitokeza na kumposa Bibi Khadija. Hata hivyo wote hao hawakukubaliwa.

Mwanzo wa Safari ya Huba

Bi Khadija alifanya uchunguzi kuhusiana na maisha ya Mtume Muhammad akichunga heshima yake na kujiepusha kabisa na hisia za kike. Maisarah naye baada ya kurejea kutoka safarini alimbainisha Bi Khadija matukio yote yaliyotokea safarini. Baada ya Bibi Khadija kusikia maneno hayo, alimuendea Waraqah bin Nawfal na kutaka ushauri kutoka kwake. Wakati huo uwepo wake wote ulikuwa umetawaliwa na mapenzi na huba kwa Mtume SAW. Baada ya hafla ya uchumba na ndoa, alimtumia Muhammad SAW mali nyingi kama zawadi kwa Mtume na kuumwambia Waraqh bin Nawfal kwamba, watangazie watu wote kuwa, kuanzia sasa na kuendelea, utajiri na suhula zote za kibiashara na kiuchumi za Khadija ni za Muhammad ambazo amempatia kwa moyo mkunjufu, nia safi na fakhari kamili. Waraqah bin Nawfal alifanya kama alivyotakiwa ambapo akiwa amesisima baina ya Zamzam na maqam Ibrahim aliwaita watu wote kwa sauti ya juu na kusema: Enyi watu! Shuhudieni na mtambue kwamba,Khadijaamempatia Muhammad utajiri wake wote kuanzia mashamba, bustani, mifugo mpaka watumwa na watumishi na hata huba na mapenzi yake na amempokea na kumkubali.

Salama na salamu za Allah ziwe juu yako Ewe Bibi Khadija, mama wa waumini, mke mwema wa mbora wa viumbe Mtume Muhammad SAW, mama wa Bibi Fatima na bibi wa Imam Hassan na Hussein AS.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: