SEHEMU YA KWANZA
(1)
MAANA YA 'ADL' (uadilifu)
Neno 'Adl' hasa limetungwa kuleta maana ya "kufanya vitu
viwili sawa" na "kugawa sawasawa" kwa lengo la kutekeleza haki
na wema. Vivyo hivyo kwa neno 'Insaaf' ambalo maana yake hasa ni "kugawa
sehemu mbili". Wazo la kugawa sawasawa linaleta maana ya "usawa"
au "uadilifu". Kwa hivyo, neno 'Adl' lina maana ya
"Uadilifu", "Usawa", "haki", "kufanya mambo
mema,' "unyofu", "kutopendelea" na "kutoonea".
Kinyume chake ni 'Jawr' na "Dhulm'. 'Jawr' maana yake ni "kupendelea".
"Kuonea" na "Ujeuri". 'Dhulm' maana yake ni "kuweka
kitu mahala pasipohusika" kama vile, hakimu mwonevu katika hukumu yake
anavyomnyima haki mwenye kuonewa na hivyo anaweka hukumu yake mahali
pasipohusika, basi huitwa "Dhalimu" Kufuatana na madhehebu ya Shia
Ithnaasharia, Uadilifu ni moja katika sifa muhimu kabisa za Mwenyezi Mungu.
Kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na Umoja wake huja chini ya mzizi wa kwanza wa dini,
"Tawheed" na vimeelezwa katika kitabu chetu "Mungu wa
Uislamu". Lakini Vitendo vya Mwenyezi Mungu huja katika huu Msingi wa
Pili, yaani Uadilifu. Ilivyokuwa tofauti kati ya Waislamu juu ya Uadilifu wa
Mwenyezi Mungu ni kubwa na ya namna nyingi basi ni lazima kuzisoma sura
zifuatazo kwa makini. Kumbuka kwamba kila neno au fungu la maneno katika sura
hizi lina maana na ikiwa msomaji atajaribu kulibadilisha neno lolote au fungu
lolote la maneno, basi atajitia katika msongamano wa hitilafu na maneno
yasiyohusika.
(2) MEMA NA MAOVU
Tofauti kuu ya kwanza ni kuwa madhehebu ya
Sunni wanaamini kwamba kitu chochote kwa dhati yake yenyewe si chema wala kiovu
na kwamba kile Mungu anachotuamrisha kufanya kinakuwa chema, na kile
Anachokataza kinakuwa kiovu. Kwa upande wa pili, madhehebu ya Ithnaasharia
wanaamini kuwa, bila kujali maamrisho ya dini, kuna mema na maovu katika
vitendo mbalimbali, hii ndiyo sababu kwamba Mwenyezi Mungu anatuamrisha kufanya
kitendo hiki kwa sababu ni chema na Anatukataza kufanya kitendo kile kwa sababu
ni kiovu.
(3) VITENDO VYA MWENYEZI MUNGU
Mwenyezi Mungu hatendi makosa au maovu.
Situmii kifungu hiki kwa maana ya "Mfalme hafanyi makosa", kwa sababu
"Mfalme hafanyi makosa" maana yake hasa ni kwamba yeye hafanyi
chochote isipokuwa hutia sahihi yaliyopasishwa na Bunge. Lakini "Mwenyezi
Mungu hafanyi makosa" maana yake ni kwamba Yeye ni Hodari na Mwenye Nguvu,
lakini hafanyi makosa. Yeyote anayefanya makosa au Dhulma, hufanya ama kwa
sababu hajui kwamba kufanya hivyo ni makosa, (lakini Mwenyezi Mungu anajua kila
kitu), au kwa sababu yeye huhitaji kitu ambacho hawezi kukipata ila kwa kufanya
maovu, (lakini Mwenyezi Mungu si Mhitaji). Au kwa sababu amelazimishwa na mtu
kufanya huo uovu. (Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye Uwezo juu ya kila kitu na
hakuna mtu ye yote awezaye kumlazimisha). Hivyo, haiwezekani kiakili kwa
Mwenyezi Mungu kufanya dhulma au makosa yo yote.
(4) KILA KITU KINA SABABU
Mwenyezi Mungu daima hatendi kitu
bila ya shabaha, yaani bila ya sababu au makusudio. Vitendo vyake vyote
vinatokana na busara na sababu ya kiujuzi, ingawaje hatuwezi kuzijua. Kwa
upande wa pili, Sunni wanasema kwamba, hakuna maovu hasa katika kufanya bila
shabaha, na ikiwa Mwenyezi Mungu anafanya chochote bila ya sababu, basi kufanya
huko kwa Mwenyezi Mungu kutakifanya kitendo hicho kuwa chema.
Itaendelea....