bayyinaat

Published time: 21 ,November ,2018      18:40:54
Uislamu umeufanya umoja kuwa jambo la wajibu na lazima miongoni mwa Waislamu na waumini na dini nyinginezo za mbinguni zinazomwamini Mwenyezi Mungu Mmoja. Uzito wa jambo hili .................
News ID: 371

Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 hadi 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia. Kundi jingine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani tofauti yake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitangaza kipindi cha tarehe mbili hizi kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Umuhimu wa Umoja

Uislamu umeufanya umoja kuwa jambo la wajibu na lazima miongoni mwa Waislamu na waumini na dini nyinginezo za mbinguni zinazomwamini Mwenyezi Mungu Mmoja. Uzito wa jambo hili unaonekana wazi katika aya za Qur'ani Tukufu na riwaya zilizopokelewa kutoka kwa Maimamu Maasumu (as). Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 103 ya Surat Aal Imran kitabu hicho kitakatifu:

وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُواْ وَاذْكُرُواْ نِعْمَةَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاء فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا

Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu.


Historia ya Kiislamu inaonyesha wazi kuwa kila mara Waislamu wa madhehebu tofauti wanapochukua uamuzi wa kuungana na kushirikiana katika ngome moja dhidi ya adui, jamii ya Kiislamu huwa ni tukufu na yenye nguvu na maadui kuwa dhaifu, lakini Waislamu wanapoghafilika na kusahau amri hiyo muhimu ya Mwenyezi Mungu, hukabiliwa na misiba mingi ukiwemo wa kudhibitiwa na maadui na kuhatarishwa kizazi na jamii nzima ya Kiislamu. Qur'ani Tukufu inasema katika aya ya 46 ya Surat al- Anfaal:

وَأَطِيعُواْ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَلاَ تَنَازَعُواْ فَتَفْشَلُواْ وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ

Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu.

Njama za kila upande dhidi ya Waislamu

Hii leo Waislamu duniani wanaandamwa na njama za kila upande za maadui, kutokana na mifarakano, hitilafu ndogondogo na kushindwa kuwa na umoja baina yao. Mashariki ya Kati, ambayo ni kitovu cha kijografia cha dini ya Uislamu imekabiliwa na wimbi la mauaji, vitendo vya ukatili na vya kufurutu mpaka vinavyotokana na hatua za Wazayuni, pamoja na makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka yakiwemo ya Taliban, Al-Qaeda, Daesh, Jabhat al-Nusra na mengineyo. Ugaidi wa kiserikali wa Kizayuni, kwa miaka kadhaa sasa unaendelea kuteketeza roho na maisha ya Waislamu wasio na hatia wa Palestina. Kwa upande mwengine, aidiolojia na itikadi za kufurutu mpaka, na magaidi ambao wenyewe wanayanasibisha wayafanyayo na Uislamu wamekuwa wakifanya ukatili na jinai za kutisha katika eneo hili. Kwa upande mwengine pia, utawala wa Kiwahabi wa ukoo wa Aal Saud, ambao ni miongoni mwa waungaji mkono wa kimaanawi na kimaada wa makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh, unaendeleza mauaji dhidi ya Waislamu nchini Yemen. Barani Afrika pia Waislamu hawajanusurika na njama dhidi yao ambapo makundi ya kigaidi kama ya Boko Haram huko Nigeria na Al-Shabab nchini Somalia yamekuwa yakihudumia malengo ya maadui wa Uislamu. Mauaji ya kinyama na ya kutisha ya hivi karibuni ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar ni mfano mwingine wa maafa na masaibu yanayowapata Waislamu katika maeneo mbalimbali. Hapana shaka kuwa, yote haya yanalazimu kuweko umoja imara na madhubuti baina ya Waislamu ili kuweka kukabiliana na njama za maadui.

Na Al-Muhtaram Salum Bendera


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: