bayyinaat

Published time: 19 ,December ,2018      19:23:41
News ID: 379

Tarehe 10 Rabiul Thani (Mfungo saba), ni siku ambayo Ulimwengu wa Kiislamu unashuhudia kuondoka na kufariki kwa Binti wa Imamu Mussa Alkadhim, Fatma Al Maasuma (as). Binti ambaye fadhila zake haziwezi kuelezeka kwa mikono ya waandishi, kwani midomo mitukufu ya Maimamu tayari imeshamaliza katika kumsifu na kumwelezea. Lakini kwa anuani ya kupata baraka katika kumwelezea basi tunachukua kalamu na kuanza kuzichuma baraka hizo.

Jina lake:

Ni Fatma Bint Mussa bin Jaafar bin Muhammad bin Ally bin Hussein bin Ally bin Abi Talib (as). Hivyo kwa nasaba hii inamfanya kuwa ni Binti wa Imamu, maana anazaliwa na Imamu Kadhim (as), pia anakuwa ni dada wa Imamu, maana kaka yake ni Imamu Ridhwa (as) ambaye wanakutana kwa mama, kama ambavyo pia anakuwa ni shangazi wa Imamu, maana ni shangazi wa Imamu Jawad ambaye ni mwana wa Imamu Ridhwa (as). Fadhila iliyoje kwa binti huyu!.

Kuzaliwa na kufariki kwake

Fatma Almassuma alizaliwa katika mji mtukufu wa Madina mnamo mwaka 173 H, na hii kwa mujibu wa kauli iliyo na nguvu miongoni mwa kauli mbili, nyingine ikiwa ni ile isemayo kwamba alizaliwa mwaka 183, mwaka ambao kwa mujibu wa historia ndio mwaka ambao alifariki Imamu Kadhim (as).

Ama mwanamke mtukufu kama huyu katika umri wa miaka 28 tu, ndani ya mwaka 201 aliweza kuaga dunia na kuifanya dunia kujaa huzuni na machungu mazito. Na hii ni kutokana na sumu aliyopewa na kupelekea kifo chake hicho.

Amezikwa katika mji mtukufu wa Qom, mji ambao umepewa sharafu ya kuwa ni Haram (sehemu tukufu) ya Maimamu (as). Sehemu ambayo watu kila mwaka hufunga safari kutoka sehemu za mbali kwa ajili ya kuja kumzuru mwanamke huyu ambaye ziara yake inasimama katika sehemu ya ziara ya Fatma Zahra kama tutakavyoeleza.

Baadhi ya Fadhila zake:

Ukiacha Imamu Ridhwa (as) katika watoto wa Imamu Mussa Alkadhim, basi hukuna mtoto mwingine ambaye alifikia cheo na daraja ya huyu mwanamke. Na hii ni kutokana na kulelewa kwake katika nyumba ya imani, tohara na utakatifu kisha yeye mwenyewe pia kukubali malezi hayo.

Historia inasema kwamba kutokana na baba yake kuwa kifungoni kwa muda mrefu kutokana na utawala wa kidhalimu, basi kaka yake Imamu Ridha ndiye alichukua jukumu la kumlea mwanamke huyu, hivyo muda mwingi alikuwa hayupo mbali na mafundisho matakatifu ya Kiislamu kupitia watu wenye dhamana ya kufundisha watu.

Sababu ya kuitwa Fatma:

Ukirejea katika historia basi utakuta ni namna gani ambayo Maimamu walikuwa wakipenda jina la Fatma, moja ya sababu ni kwamba jina hilo ndio lilikuwa jina la mama yao mtukufu, Binti yake Rasuli, mama wa Maimamu wote, Fatima Zahra amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Lakini pia mbali na kulipenda jina hilo bado unakuta walikuwa wakihimiza wafuasi wao kulitumia jina hilo kwa mabinti zao.

Imepokelewa na Sulaiman Jaafari kutoka kwa Imamu Kadhim (as) kwamba amesema: "...Ufukara hauingii nyumba ambayo ndani yake kuna jina la Muhammad au Ahmad au Ally au Hassan au Hussein au Jaafari au Twalib au Abdullah au Fatma...”.[1]

Pia Al Sakuniy anapokea kutoka kwa Imamu Ridhwa (as): ".....Siku moja nilienda kwa Imamu huku nikiwa nina huzuni na simanzi sana, Imamu akaniuliza "..Ni kipi kinakuhuzunisha ewe Sakuniy?”, nikamjibu kwa kusema "...Nimepata mtoto wa kike ewe Imamu”, Imamu akasema "....Huna haja ya kuhuzunika kabisa, kwa maana yeye yupo duniani lakini riziki yake inatoka kwa Mwenyezi Mungu, kama ambavyo ataishi kwa riziki mipango ya Mungu”. Kisha imamu akaniuliza kunako jina nililompatia, nami nikamjibu kuwa nimemuitwa Fatma, imamu akafurahi sana na kunishika katika paji langu la uso na kusema ".....Kwa kuwa umemuita Fatma basi huna haki ya kumtukana, kumlaani wala kumpiga...”[2]

Inaendelea......



[1] Alkafi Juz 6 Uk 19

[2] Alkafi Uk 48


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: