bayyinaat

Published time: 19 ,December ,2018      19:26:56
Maasumu ni neno la Kiarabu lenye maana ya mtu ambaye hafanyi dhambi wala makosa, kama ambavyo inajulikana kwa Mitume na Maimamu (as). Sasa kwanini mwanamke huyu pia amekuwa maarufu kwa jina la Maasuma........
News ID: 380

Ibada yake:

Ni wazi kwamba mwanamke kama huyu atakuwa na ibada ya juu kabisa katika waja wake mwenyezi Mungu, na hii i kutokana na malezi ambayo amekulia katika maisha yake. Baba bora, kaka bora hali kadhalika mama bora pia.

Mihrab (Sehemu maalumu ya ibada) ya mwanamke huyu mpaka leo bado ipo mjini Qom, watu mbalimbali huenda kutabaruku na sehemu hiyo tukufu ndani ya msikiti maarufu kwa jina la Masjid Amir.

Kwanini aitwe (Maasuma):

Maasumu ni neno la Kiarabu lenye maana ya mtu ambaye hafanyi dhambi wala makosa, kama ambavyo inajulikana kwa Mitume na Maimamu (as). Sasa kwanini mwanamke huyu pia amekuwa maarufu kwa jina la Maasuma, je, na yeye pia ni katika wale ambao hawafanyi madhambi na makosa kama Mitume na Maimamu?.

Katika kujibu au kuelezea jambo hili kunaweza kuwa na mitazamo miwili ambayo yote kwa pamoja haipingani katika kuelezea sifa za mwanamke huyu.

1. Jamii aliyoishi

Kama inavyojulikana kwamba mwanamke huyu mtukufu aliishi katika jamii ya Kiirani, jamii ambayo neno "Maasumu” kwa lugha yao hutumika kwa mtu ambaye ni mpole, mkarimu na asiye na matatizo na watu, hivyo inawezekana kuwa kwake mashuhuri kwa jina hili ni kutokana na jamii husika aliyokulia hasa ukiangalia umri wake ambao amefariki nao ni chini ya miaka 30.

2. Kweli ni Maasumu lakini.....

Mtazamo wa pili ambao unaweza kuwa ni jibu au maelezo sahihi ya kuelezea sababu ya kuwa kwake mashuhuri kwa jina la maasumu, ni kusema kwamba ndio, yeye ni Maasumu, kwa maana kwamba hafanyi makosa na madhambi. Na hii ni kutokana na vigawanyo vya Maasumu kama ambavyo tumeelezwa na maulama wetu.

"..Isma” (..Kutofanya madhambi na makosa) kumegawanyika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni Isma ambayo inakuwa ni lazima na wajibu kwa muhusika, kwa maana kwamba yeye ni lazima awe hivyo kutokana na uzito wa majukumu yake. Na sehemu ya pili ni Isma ambayo inaweza kuwepo hata kwa asiyekuwa Mtume au Imamu, kutokana na namna ambavyo amehifadhi na kuichunga nafsi yake kunako madhambi na makosa. Na hii ipo wazi katika historia ya baadhi ya maulama wetu kwamba walikuwa wakizichunga nafsi zao hata kunako kufanya mambo ambayo ni makruhu au kuacha mambo ambayo ni sunna!. Hivyo ikiwa maulama tu wameweza kufikia cheo hicho vipi kwa mwanamke mtukufu kama huyu ambaye historia inaelezea utukufu wake?.

Kama ambavyo Pia baadhi ya maneno kutoka kwa Maimamu wenyewe yanaweza kuwa msumari mwingine kunako utukufu wa mwanamke huyu, imepokelewa kutoka kwa Maimamu kwamba mwenye kumzuru Fatma Maasuma mjini Qom huku akiwa anatambua haki yake basi pepo ni yake. Au iliyopokelewa kutoka kwa Imamu Ridhwa (as) aliposema:

"..."من زار المعصومة بقمّ كمن زارني"

"....Mwenye kumzuru Maasuma mjini Qom ni kama ambaye amenizuru mimi...”

Fatma Maasuma na Shafaa:

Ni cheo kingine ambacho Bibi Fatma Maasuma amebarikiwa na Mwenyezi Mungu, nayo ni nafasi ya kuweza kuombea watu siku ya kiama na kuwafanya kuingia peponi kupitia yeye. Imepokelewa kutoka kwa Imamu Swadiq (as) akisema :

"....Hakika Mwenyezi Mungu ana sehemu tukufu ardhini ambayo ni Makka, na Mtume pia ana sehemu Tukufu ambayo ni Madina, Imamu Ally pia ana sehemu Tukufu ambayo ni Kuffa, na itambulike kwamba Qom ndio Kuffa ndogo, kwa maana kuna mwanamke kutoka kizazi changu ambaye atafarikia huko, jina lake ni Fatma Binti wa Mussa, wafuasi wangu wengi wataingia peponi kupitia Shafaa yake...”[1]

Inaendelea....

[1] Biharul Anwar Juz 57 Uk 228


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: