bayyinaat

Published time: 19 ,December ,2018      19:40:26
Na kutokana na kuenea kwake huku katika jamii za wanadamu kunaweza kuwa ni kigezo kwao katika kuamini usahihi wake au hata kuamini kwamba Mwenyezi Mungu anaruhusu
News ID: 385

Katika mambo ambayo huwezi kukataa athari zake katika maisha ya binadamu ni pamoja na swala zima la muziki, na hii ni kutokana na kutumika kwake katika sekta mbalimbali za maisha ya kila siku. Endapo utaamua kurejea historia kuanzia zama zilizopita, utakuta ni namna gani muziki ulikuwa ni wenye athari si tu kwa watu wa kawaida, bali hata viongozi wao pia walikuwa wakitumia nyenzo hii muhimu katika kufikia malengo yao.

Na kutokana na kuenea kwake huku katika jamii za wanadamu kunaweza kuwa ni kigezo kwao katika kuamini usahihi wake au hata kuamini kwamba Mwenyezi Mungu anaruhusu jambo hilo, kwa kuangalia tu kwamba ni jambo lenye athari ya haraka katika maisha. Na ndio maana Uislamu haukuacha kuweka misingi thabiti katika kuhakikisha kwamba hilo halitokei kabisa.

Hukumu ya muziki katika Uislamu:

Inawezekana mmoja wetu akashangaa pindi atakaposikia kwamba muziki ni haramu katika dini ya Kiislamu, ndio, na hii ni kutokana na namna ambavyo muziki umekaa katika nyoyo za watu kiasi kwamba umekuwa ni jambo la kawaida mpaka kufikia hatua ya kuona kuwa si moja ya mambo ambayo yanatakiwa kukemewa na kukatazwa.

Allamah Majlisiy anasema:

"...Hakuna tofauti baina ya maulama kunako uharamu wa muziki, bali Shekh Tusiy, Allamah Ibn Idris wananukuu Ijmaa (makubaliano ya maulama katika jambo) juu ya hilo...”.[1]

Athari za muziki katika jamii:

Wataalamu wa maswala ya kijamii katika upande wa Uislamu wanaamini kwamba moja ya sababu zilizopelekea kuanguka na kupotea kwa baadhi ya jamii ni kutokana na kushikamana kwao na maswala ya muziki pamoja na viambatano vyake kama vile kucheza nk. Kwa maana ya kwamba endapo kama jamii itakuwa ni yenye kushikamana na maswala hayo basi bila shaka kuna mambo ya muhimu itaachana nayo kama vile elimu, kujishughulisha, kujitolea kwa ajili ya wengine nk.

Japokuwa katika hili pia tunakutana na changamoto ambazo unaweza kudhani kwamba zinakuja kubatilisha msimamo huu, napo ni pale ambapo unakuta kuna majina ambayo yanatumika katika kupamba muziki na viambata vyake, kama vile unapokuta muziki unapewa jina la fani, na kwamba hakuna tofauti baina ya fani ya muziki na fani nyinginezo. Au ukasikia kwamba kucheza leo hii kunaitwa ni mazoezi ni kuweka mwili sawa.

Haya yote tunaweza kuyaweka chini ya anuani ya aya iliposema:

أَفَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا ۖ فَإِنَّ اللَّهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ ۖ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ

"....Je! Yule aliye pambiwa amali zake mbaya na akaziona ni njema - basi hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa amtakaye. Basi nafsi yako isisononeke kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anajua wanayo yafanya...”

Naam, hiyo ndiyo kazi ya Shetani, kuhakikisha kwamba yale ambayo yamekatazwa na Mwenyezi Mungu yanaonekana ni mazuri kwa binadamu. Kwa sababu kama ni fani au mazoezi kama inavyodaiwa basi ni kwa nini isiwe katika misingi ambayo Muumba wako anaitaka?, je ni lazima iwe kwa njia ambayo haipendi?.

Hebu rejea katika jamii zetu hizi uone ni namna gani ambavyo vikao vyenye kushamili muziki kunakuwa na aina nyingine za maasi, unywaji pombe, uzinzi na mengineyo ni baadhi tu ya mambo ambayo mwanzo wake ni muziki. Na si kwamba jambo hili linahitajia dalili kubwa au usomi wa kiwango fulani katika kukubaliana nalo, kwa maana kila siku vyombo vyetu vya habari na mawasiliano vinaonyesha kila siku tena kwa sura ya wazi kabisa. Tena jambo la kushangaza zaidi ni pale unapokuta hao ambao wanajiita ni wenye fani ya muziki wenyewe kwa wenyewe wanashambuliana na kuambiana kwamba muziki wa fulani si fani na hauna fani yeyote ile bali ni upuuzi mtupu.

Inaendelea...
Sh Abdul Razaq Bilal (Abuu Asghar).

[1] Ainul Hayat Juz 1 Uk 379


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: