Je kifo ni mwanzo au mwisho?
Kwanini watu wengi wamekuwa wakiogopa
kifo? Kuna sababu gani nyuma yake? Hapa ndipo tutaanzia makala hii ambayo
inalenga kumuelimisha Mwislamu juu ya uhakika wa Kiyama au siku ya marejeo. Na hii
ni kutokana na kwamba hakuna njia ambayo tunaweza kupita ili kufikia siku hiyo
tofauti na kifo au mauti, na kwakuwa siku zote kifo kimekuwa ni kitu ambacho
kwa mwanadamu ni chenye kutisha mno, na wakati mwingine hata kumnyima uhuru na
furaha ya kutenda majukumu yake muhimu kuelekea kwa mola wake, na si tu kwamba
neno kifo au kifo chenyewe ndivyo humwogopesha mwanadamu bali tunakuta wakati
mwingine mwanadamu huyu anakuwa ni hata mwenye kuogopa makaburi yanapokuwa
katika hali yake ya kawaida, na ndipo wengine leo hii hujitahidi kuyafanya makaburi
hayo kuwa mfano wa majumba ya kifahari ili tu angalau iweze kuwasahaulisha
uhakika wa nyumba ile ya kila mmoja wetu. Je kuna nini katika hiki kifo mpaka
kimekuwa ni kitu chenye kuogopesha na kutisha kiasi hiki?.
Lakini pia hebu tuangalie upande wa pili,
upande ambao tunakuta kuna baadhi ya watu ambao hawakiangalii kifo kwa sura
ambayo kinaangaliwa na watu tuliotoka kuwazungumzia hapo juu, hapa tunawakuta
watu hawa wanakiangalia kifo kwa namna ya kukifurahia na hata kutamani kiwajie wakati
wowote. Kwani tukirejea katika historia tunaambiwa kwamba kuna baadhi ya watu
ambao walikuwa wakikesha kutafuta mambo ambayo yatawafanya siku zote wawe hai
na vijana, wakati ambapo kuna ambao walikuwa siku zote wakitamani Jihadi ije
ili wakapigane na waelekee kwa mola wao, nini siri na sababu ya kila kundi
katika makundi haya?.
Kwanini tunaogopa kifo?
Kama tutakuwa ni wenye kufanya tafiti basi
tutafikia katika natija ya kwamba hofu ya kifo inatokana na mambo makuu mawili:
1.
Kutafsiri
kifo kwamba ndio mwisho wa kila kitu
Hii ikiwa na maana kwamba
kawaida ya mwanadamu siku zote amekuwa ni mwenye kukimbia sana swala la
kutokuwepo na kupenda mno swala la uwepo. Mwanadamu anapenda sana uwepo wa afya
na hapendi hata siku moja afya ile isiwepo, na ndio maana anajitahidi kadri
awezavyo ili tu asipate maradhi na abakie ni mwenye afya siku zote. Kama ambavyo
mwanadamu huyu anakimbia sana giza ambalo humaanisha ukosekanaji wa nuru na
mwangaza, na mifano mingi ambayo inaweza kuthibitisha jambo hili. Lakini jambo
la kushangaza zaidi ni kwamba mwanadamu huyuhuyu anamkimbia hata ambaye jana
alikuwa hai (maiti) hii yote ni kwanini, ni kwamba siku zote uwepo wa kitu
unapenda kuambatana na uwepo mwenzake, yaani mwanadamu anaamini kwamba yeye
yupo, kwa hivyo ni lazima pembeni yake kuwe na kitu ambacho kipo na si kitu
ambacho kimepoteza uwepo. Sasa hapa ndipo tunapata jibu la kwanini mwanadamu
anakuwa ni mwenye kuogopa kifo au hata maiti na makaburi pia, ni kwamba
mwanadamu huyu ameweka katika akili yake kwamba kifo ni mwisho wa kila kitu
kama ambavyo pia kifo ni kutokuwepo kwa kitu, na ndio maana kutokana na msingi
wake wa kupenda kuwa na vitu ambavyo vipo katika uwepo, anatokea kuchukia kifo
kwa sababu tu kifo si kitu ambacho kipo, bali ni mwisho wa kila kitu.
2.
Ukurasa
mchafu
Hii ni sababu ya pili
ambayo inasababisha wanadamu kuogopa kifo, kwamba kuna wakati unakuta mtu
anakubali kwamba kifo siyo mwisho wa maisha au mwisho wa kila kitu, na kwamba
kuna maisha baada ya kifo, lakini bado unakuta mtu huyu anaogopa kifo kile. Sababu
ni kwamba mtu wa namna hii anakuwa hana matendo mazuri ambayo ameyatanguliza
ili kesho atakapokwenda katika huo ulimwengu wa baada ya kifo yawe ni yenye
kumwokoa, na ndipo unakuta mtu kama huyu pia anaogopa kifo pamoja na kwamba
haamini kwamba ni mwisho wa kila kitu.
Na hii ndiyo hali ya kila mwovu hapa
ulimwenguni, anatamani kwamba maisha haya yawe ndiyo maisha yake milele, kwani
anajua kwamba endapo maisha haya yatakatika na kuanza maisha mengine baada ya
haya, bila shaka atakuwa katika adhabu na masikitiko makubwa. Lakini kwa ambao
ni wema hapa ulimwenguni tunakuta kwamba mambo ni kinyume kabisa, kwani hawa wanajua
kuwa furaha ya kudumu inapatikana baada ya kifo, hivyo ndio maana kifo kwao
kinakuwa ni chenye kusubiriwa muda wote tena kwa furaha.
Muhimu
Kifo sio mwisho wa maisha ya mwanadamu, bali ni mwanzo wa maisha ya
awamu ya pili ya mwanadamu huyo.
Tukutane wakati ujao katika mwendelezo wa
makala hizi.
Sh Abdul Razaq Bilal.