bayyinaat

Published time: 26 ,March ,2017      00:04:36
Lakini sasa haya maisha ya kijamii pamoja na kwamba yana faida kubwa sana kwetu pia ndani yake kuna matatizo na changamoto ambazo zinaweza kuwa sababu ya migongano au hata vita baina ya jamii husika, sasa je, nini kinahitajika ili kuweza kuondoa hii migongano?. Hapa ndipo ambapo tunakuta kwamba kuna haja ya kuwepo kwa...........
News ID: 63

Haja Ya Kuwepo Mitume -2

Katika makala na somo lililopita tuliweza kuangalia kwamba kuna haja ya kuwepo Mitume katika maisha ya mwanadamu, na hii ni kutokana na kwamba mwanadamu pamoja na kwamba kujiona amekamilika, ila bado anahitajia mengi sana kutoka kwa muumba wake, mfano wa hayo mengi ni kama:

1. Malezi

2. Mafunzo nk

Sasa katika sehemu hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tutakwenda kuangalia ulazima na haja ya kuwepo kwa mitume kwa kutumia dalili nyengine, lakini kwanza tutaanza na utangulizi na kisha kuingia katika mada husika.

Bila shaka sote tunatambua kwamba ili mwanadamu aweze kufikia kilele cha mafanikio yake, ni lazima awe ni mwana jamii, kwa maana ya kwamba ni lazima ajichanganye na wenzake ndipo aweze kufikia mafanikio hayo, na laiti kama mwanadamu huyu atakuwa ni mwenye kujikusanya peke yake bila ya wenzake, basi atakuwa siku zote ni mwenye kubakia na fikra moja na bila ya kuendelea, hivyo basi swala la mwanadamu kuwa ni mwanajamii na swala muhimu katika maisha yake.

Ndio, kwani imethibiti kwamba harakati za kijamii ndizo ambazo zimepelekea watu kufikia katika malengo makubwa, na sio harakati za mtu mmoja kama mmoja, angalia leo hii watu wanafanikiwa kufika katika sayari mbalimbali, sio kwamba ni wazo au juhudi za mtu mmoja, bali ni juhudi za wataalamu ambao kila mmoja alikuja na wazo lake, wakayakusanya na kisha kutoa jambo moja lenye tija na maana kubwa.

Au mwangalie Daktari ambaye leo hii anasifika kwamba ni mtaalamu wa mswala fulani, unadhani hii imetokea kwake mara moja tu akawa mtaalamu? Hapana! Bali alitumia muda mwingi sana katika kufanya majaribio mpaka akafikia katika utaalamu ule, sasa je kama asingepata ushirikiano kutoka kwa wanaomzunguka, unadhani angefikia katika utaalamu ule?, bila shaka hapana, na ndio maana tunasema kwamba maisha ya kijamii ndiyo ambayo humfikisha mtu katika malengo makubwa.

Lakini sasa haya maisha ya kijamii pamoja na kwamba yana faida kubwa sana kwetu pia ndani yake kuna matatizo na changamoto ambazo zinaweza kuwa sababu ya migongano au hata vita baina ya jamii husika, sasa je, nini kinahitajika ili kuweza kuondoa hii migongano?.

Hapa ndipo ambapo tunakuta kwamba kuna haja ya kuwepo kwa kanuni na maelekezo ambayo yatatuondolea matatizo hayo, na ili kanuni hizi ziweze kuondoa matatizo hayo basi ni lazima ziwe na sifa kuu tatu ambazo ni:

1. Ziwe ni kanuni ambazo zinabainisha na kuelezea majukumu ya kila mmoja kuelekea jamii anayohusu, yaani kila mmoja wetu ajue kwamba jamii inahitaji nini ili aweze kuipatia. Kisha ibainishe majukumu ya jamii kuelekea kila mwanajamii, yaani jamii kama jamii inatakiwa kufanya nini kwa ajili ya wanajamii wake.

2. Ziwe ni kanuni ambazo zinaandaa kwa mwanajamii njia bora kabisa katika kutekeleza majukumu yake.

3. Ziwe ni kanuni ambazo zitaweza kuchunga mipaka ya kila mwanajamii, kwamba kila mmoja aweze kutekeleza majukumu yake bila ya kuvunja mipaka ya mwenzake, na endapo kutatokea mmoja amevunja mipaka ya mwenzake basi kuwe na adhabu inayonasibiana na kosa lile.

Ni nani anafaa kuweka sheria hizi?

Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu anajiuliza kwa sasa baada ya kuona kwamba maisha ya kijamii ni lazima yawe na sheria ili kuweza kufikia lengo la juu kabisa. Na ili kuweza kujibu swali hili ni lazima kwanza tuweze kujua ni nani ambaye anaweza kuweka kanuni kwa hii jamii, kanuni ambazo zitakuwa ni zenye kutimiza masharti matatu tuliyoyataja hapo juu.

Hapa mimi kabla ya kumtaja huyu ambaye anafaa kuweka kanuni hizi, ningependa kwanza kutumia mfano ufuatao na kisha kuja kuuambatanisha na jamii ya wanadamu. Napenda kuifananisha jamii ya wanadamu na treni kubwa, kisha nafananisha wale wanaohukumu jamii ile na kichwa cha treni ambacho ndio kinaongoza treni lile, lakini mwisho nafananisha kanuni itumikayo kuendesha jamii ile na reli ambayo ni lazima mwongozaji aongoze treni kuelekea pale, na treni ni lazima ipite pale ili tu iweze kufikia safari yake. Lakini pamoja na hayo hii reli ambayo ndio kama kanuni bila shaka ni lazima iwe na sifa kadhaa mpaka treni ile ifike safari yake salama, mfano ni lazima reli ile iwe ni madhubuti kiasi ambacho hata kama treni itakaa juu yake basi haitaweza kudidimia wala kuvunjika na kusababisha madhara, pia ni lazima reli ile pia iwe na uwiano mzuri baina yake ili treni iweze kukaa vizuri juu yake, kama ambavyo piani lazima isiwe imepita katika miteremko au milima mikali ambayo itapelekea kichwa cha treni kushindwa kusukuma treni ile kwa umakini, na mengineyo mengi ambayo ni lazima kuchungwa katika reli.

Sasa ikiwa tumeona kwamba reli inatakiwa kuwa na masharti kadhaa ili tu treni iweze kufika salama, bai hivyohivyo mwekaji kanuni wa jamii ya wanadamu ni lazima atimize baadhi ya masharti na vigezo ili jamii ile pia iweze kufika katika malengo yake. Na miongoni mwa masharti hayo ni kama:

· Awe ni mwenye kuwatambua vizuri wanadamu wanaounda jamii ile, kwa maana ya kwamba awe anajua mapungufu yao, nini wanahitajia, matatizo yao na kila ambacho kinawahusu

· Awe na uwezo wa kujua mambo ambayo yanaweza kuisibu jamii ile miongoni mwa matatizo na kisha kuwapa njia bora ya kuweza kujitoa na majanga hayo yanayoweza kuwakumba

· Asiwe ni mwenye kunufaika na kanuni ile, si yeye wala watu wake wa karibu

· Awe na uwezo wa kutambua kila jambo ambalo linaweza kumuinua au kumuangusha mwanadamu

· Asiwe ni mwenye kufanya makosa si kwa makusudi wala kusahau

· Na mwisho kabisa ni lazima awe ni shujaa na mwenye kuthubutu, na si mwoga na mwenye kushindwa kupitisha kanuni kwa kuogopa lawama au chochote kutoka katika jamii anayoitungia sheria husika

Ni nani ambaye anatimiza sifa hizi?

Je anaweza kuwa mwanadamu? Ni lazima tuanzie hapa, maana hatuna katika viumbe, kiumbe ambacho kinaweza kutimiza sifa hizi kwa ukaribu zaidi ya mwanadamu, na hii ni kutokana kwamba anaweza kujigamba na kusema kwamba yeye ana akili ambayo viumbe wengine hawana.

Sasa je, mwanadamu anaweza kuwa na sifa zilizotajwa?, bila shaka hapana, nasema hivi nikimaanisha kwamba, ikiwa mpaka leo hii mwanadamu mwenyewe ameshindwa kupata jib kamili kuhusu yeye, vipi ataweza kupata jibu juu ya mambo yote yanayomuhusu, mwanazuoni mmoja ameandika kitabu akikipa jina la " Mwanadamu kiumbe Asiyejulikana” akiwa na maana kwamba kila siku mwanadamu anagundua kwamba bado hajafikia katika kilele cha kujifahamu, maana kila siku anakutana na jambo jipya ambalo jana alikuwa halijui, sasa huoni kwamba mwanadamu ana haja kwanza ya kujitambua kisha ndio aje aweke kanuni?, kwa hiyo ni kwamba mwanadamu hawezi kuwa mwenye kuweka kanuni kutokana na kwamba hana masharti.

Na ndipo tunapofikia katika natija ya kwamba, Mwenyezi Mungu pekee ndie ambaye anaweza kuweka kanuni kwa mwanadamu, kwa sababu yeye ndie mwenye kumjua mwanadamu na kila anachohitaji, na hii ni kutokana na yeye ndie muumba wake hivyo anajua mapungufu yake pia.

Na kanuni hizi ambazo yeye huzipanga bila shaka mwanadamu anazihitajia na sio Mwenyezi Mungu, kwani zote zinakuwa katika lengo la kumfikisha mwanadamu katika malengo makubwa. Na ndipo ambapo Mwenyezi Mungu huagiza mmoja katika watu ili kuweza kufikisha sheria zitokazo kwa Muumba. Na huyu ndie ambaye tulimpa sifa ya kwamba yeye ni kama kichwa cha treni ambacho kinaongoza treni baada ya kuwa tayari kuna reli, na ye ni Mtume na wala si mwingine.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: