bayyinaat

Published time: 26 ,March ,2017      00:17:15
Ili kupata taswira nzuri kunako mtazamo wa Kiislamu tuangalie mpangilio wa kazi katika maisha ya bibi Fatima Zahara (a.s) Maisha ya bibi Fatma yanaashiria kwamba mpangilio wa kazi katika nyumba yake uligawika kwa kuzingatia haki na usawa.
News ID: 64

MWANAMKE NA KAZI KWA MTAZAMO WA UISLAMU

Moja kati ya matatizo makubwa zaidi yanayoikumba jamii yetu ya leo ni suala la mgawanyiko wa kazi kwa ajili ya kuboresha uchumi wa familia.

Lakini yapaswa ifahamike kwamba moja ya majukumu wanandoa ni kuandaa uchumi utakao endesha familia katika masuala yote yanayo husu familia hiyo, ila katika suala hili kuna tofauti kubwa baina ya mtazamo wa Kiislamu na mitazamo ya Kimagharibi.

Mtazamo wa Kiislamu ni kwamba kuandaa uchumi wa familia ni suala linalomuhusu mwanaume, na mwanamke hana wadhifa huo, na hii ni kwa sababu ya kutofautiana kimaumbile baina ya mwanamke na mwanaume hasa ukizingatia kwamba mwili wa mwanamke hauna uwezo wa kustahamili kazi ngumu kama mwanaume.

Ili kupata taswira nzuri kunako mtazamo wa Kiislamu tuangalie mpangilio wa kazi katika maisha ya bibi Fatima Zahara (a.s) Maisha ya bibi Fatma yanaashiria kwamba mpangilio wa kazi katika nyumba yake uligawika kwa kuzingatia haki na usawa.

Imam Baqir (a.s) amesema kazi za ndani ya nyumba ziligawika kati ya bibi Zahara na Imam Ally kama ifuatavyo:

Kazi za ndani ya nyumba mfano, kupika, kufagia na kusafisha nyumba zilimuhusu bibi Fatma, na kazi za nje ya nyumba zilimuhusu Imam Ally (as).

Imam Swadiq (a.s) amesema: (Mtume ndie alie gawa kazi katika nyumba ya bibi Fatma na Imam Ally kwa kusema; kazi za ndani ya nyumba ni za bibi Fatma na kazi za nje ya nyumba ni za Imam Ally.

Bibi Fatma akiwa mwenye furaha alisema: Ni Mwenzi Mungu pekee ndiye anayefahamu kwamba ni jinsi gani nimefurahi kutokana na kugawika kwa kazi, kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amenizuia kufanya kazi zinazo wahusu wanaume.

Mwanamke kupewa majukumu ya nyumbani na kutokuwa na majukumu ya nje inaashiria utukufu na thamani ya mwanamke, tukirejea zama za Mtume (s.a.w.w) tunaona kwamba mtume aliashiria kuwa mwanamke tofauti na kazi za ndani anaweza kujifanyia shughuli nyengine akiwa katika mazingira ya nyumbani zinazoweza kumletea kipato kama vile ushonaji ,ususi, ufumaji nk… kwani kazi hizi ni bora zaidi kuliko kufanya kazi nje mfano ukatibu au katika makampuni na sehemu mbalimbali ambazo hazina mazingira mazuri kwa mwanamke.

Lakini yawapasa kufahamu kuwa Uislamu haupingi mwanamke kufanya kazi za nje ya nyumba ila kuna masharti machache anayopaswa kuyatimiza mwanamke, nayo ni yafuatayo

1. Asifanye kazi kwa kulazimishwa

2. Kazi isiwe ni sababu ya kukiuka maadili ya Kiislamu

3. Isisababishe kupoteza nafasi yake (umama kwa watoto na mke kwa mume)

4. Kusisababishe ugomvi kati ya mume na mke

Na sasa tuangalie mtazamo wa kimagharibi kwamba uchumi wa kifamilia ni jukumu la mwanaume au mwanamke? mtazamo wa kimagharibi ni kwamba jukumu la uchumi wa familia ni la wote, na hii ni kutokana na kutozingatia maumbile ya mwanamke na mwanaume.

mnamo mwaka 1760 yalianza mapinduzi ya viwanda katika nchi ya Uingereza, na Uingereza ni nchi ya kwanza iliochukua mfumo wa viwanda Duniani, na kuwa ni nchi ya kiteknolojia.

Basi mapinduzi ya viwanda yalisababisha kupanuka zaidi mtazamo wa kufanya kazi kwa wanawake, na inawezekana kuwa sababu kuu iliowafanya wanawake nao waanze kufanya kazi ni kukithiri viwanda na uchache wa wafanya kazi, hivyo ikapelekea wanawake pia kufanya kazi katika sekta mbalimbali

Wanachuoni wa kimagharibi wamefikia tija ya kwamba, kazi anazozifanya mwanamke nyumbani zinasaidia katika kuimarisha familia ila ni kazi isiokuwa na malipo. wataalamu wa maarifa ya jamii pia wana imani kwamba, kazi isio na malipo hasa kazi za ndani ya nyumba hazihesabiki kuwa ni kazi, ama kazi ni ile yenye malipo.

Faida ya kufanya kazi kwa mwanamke

1. Kunaongeza maarifa na kujiamini.

2. Kupunguza suala la kutegemea upande mmoja kiuchumi.

Madhara yake

Pamoja na kwamba swala hili lina faida zake, lakini pia endapo halitafanywa kwa kufuata misingi husika na sahihi, linaweza kupeleka katika majanga yafuatayo:

1. Kuweka ufa kiroho baina ya mama na wana.

2. Kukidhi baadhi ya mahitaji ya kinafsi nje ya nyumba.

3. Kujihisi kutenda dhambi kutokana na kutokuwa karibu na watoto wake

4. Inapelekea kuhadaika na kudanganyika

5. Huleta kiburi kwa mumewe( hasa kipato chake kikiwa cha juu)

Imeandikwa na Ummu Muhammad Matenga

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: