bayyinaat

Published time: 28 ,March ,2017      14:09:25
Namleta kwako ewe ndugu msomaji wa mada hii, kiumbe ambaye hujulikana kama popo, ni mdogo kimaumbile ukilinganisha na tembo, lakini katika kumfikisha mwanadamu kunako kuthibitisha umahiri wa muumba wana nafasi......
News ID: 68

Popo na Siri ya Uumbaji

Inawezekana tukawa tunatamani sana kufikia katika lengo la kuamini kwamba kuna muumba ambaye ni mahiri katika uumbaji wake, lakini imani ya kila mmoja wetu ikawa katika kuamini kwamba ili kufikia lengo hili ni lazima tutumie mambo au vitu vikubwa kwa sababu tunachotaka kuthibitisha ni kikubwa pia. Sasa katika mada hii nitajaribu kuelezea kwamba uhalisia wa kufikia lengo letu hausimamii tu katika mambo au vitu vikubwa kama tunavyodhani, bali hata katika mambo ambayo tunayaona ni madogo pia tunaweza kufikia lengo letu.

Namleta kwako ewe ndugu msomaji wa mada hii, kiumbe ambaye hujulikana kama popo, ni mdogo kimaumbile ukilinganisha na tembo, lakini katika kumfikisha mwanadamu kunako kuthibitisha umahiri wa muumba wana nafasi sawa.

Angalia jinsi anavyokata masafa marefu ndani ya usiku mnene, tena kwa kasi ambayo hata baadhi ya ndege warukao mchana hawawezi kwenda kasi ile, lakini inawezekana hii isiwe ajabu, je, umejiuliza kwanini ndege huyu huwa mjanja nyakati za usiku tu na si mchana? Ana kitu gani mpaka awe wa namna hii?.

Hapa inatubidi kwanza kabla ya kujua siri ya ndege huyu, tuangaze kidogo kunako kitu kinachoitwa "RADA”, tunaambiwa na ambao ni wataalamu wa maswala ya sauti kwamba, kuna kitu ambacho kipo nyuma ya sauti ya kila kitu ambacho huitwa ni "mawimbi ya sauti” na mawimbi haya kutokana na wingi wake ni kwamba masikio ya mwanadamu hayawezi kuyasikia hata mara moja. Sasa mawimbi haya endapo yatakuwa yanatoka katika kifaa chenye nguvu kubwa basi huenea kila sehemu, na endapo yatakutana na kitu chochote basi yatagonga sehemu ile na kurejea yalikotoka kuashiria kwamba kuna kitu kimezuia kuendelea kwake.

Na hivi ndivyo ambavyo tunaambiwa kwamba ndege nyingi hutumia kifaa hiki "rada” ili kuweza kujua njia salama na hata kujua kwamba mbele kuna hatari au la.

Sasa tukirejea katika kumwangalia ndege wetu ambaye ni popo, tunaambiwa kwamba pia kifaa chenye kufanya kazi sawa na rada hupatikana katika mwili wake, kwani yeye pia katika kujua njia sahihi au hata kujua kwamba mbele yake kuna hatari au la hutumia mawimbi yatokanayo na sauti yake, mawimbi ambayo yakikutana na kizuizi haraka sana huleta habari kwake, na yeye kwa kutumia masikio yake makubwa huzipokea habari hizo na kuchagua njia sahihi. Kwa hiyo tunafikia katika natija ya kwamba ndege aina ya popo huwa hategemei macho yake katika masafa yake ya kila siku, kwa sababu tumeona jinsi gani anakata masafa yake na kwamba kikubwa zaidi kwake ni mawimbi ya sauti yakishirikiana na masikio yake, na kuhusiana na hili mchunguzi mmoja kutoka nchi za Sovieti anasema "imethibiti kielimu kwamba endapo popo atakatwa masikio yake hatoweza kukata masafa yake nyakati za usiku, lakini hata kama utamtoboa macho yake haitakuwa sababu ya yeye kushindwa kukata masafa yake”. Na hii ni kutokana kwamba masikio kwake ni kiungo muhimu mno katika harakati zake. Je haya sio maajabu?!!

Sasa jambo la muhimu hapa ni sisi kujiuliza maswali yafuatayo, ni nani ambaye alimpatia kiumbe huyu vifaa hivi vyenye kufanana na rada ili kuweza kutumia katika harakati zake?, pia ni nani ambaye amemfundisha kiumbe huyu kwamba pamoja na kwamba amepewa macho, ila sio kitu kitakachomuwezesha kukata masafa na hata katika matembezi yake?, bila shaka jibu unalo katika nafsi yako na wala hakuna ambaye anaweza kufanya haya yote isipokuwa muumbaji wa kila kitu (Mwenyezi Mungu). Naam ni lazima awe yeye kwa sababu tabia au maumbile ambayo husemekana ndio sababu ya kutokea mambo ya ajabu kama haya, haiwezi hata siku moja kutengeneza mfano wa mambo kama haya ambayo tunaona kabisa kwamba yanahitaji akili ya hali ya juu na sio tu swala la kubahatisha na kutokea bila mipango.

Ametukuka mola wa viumbe na mola wa kila kitu.

Sh Abdul Razaq Bilal

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: