bayyinaat

Published time: 08 ,May ,2017      10:23:27
Imepokelewa katika riwaya kwamba uadui wa Abuu lahab kwa mtume na kwa Uislamu kwa ujumla haukuwa uadui mdogo, bali ulikuwa umefikia kiasi ambacho hata kama Abuu lahab alikuwa anaumwa hoi hakuweza kuvumilia kukaa kitandani huku Mtume akiendelea kulingania watu, bali alikuwa akimfuata kila kona ambayo alikuwa akienda huku akimwandama kwa maneno mabaya na matusi.........
News ID: 81

Suratu Al masad

(kamba iliyosokotwa)

Imeteremka Maka na ina aya 5

Mambo muhimu yaliyokusanywa na sura hii

Kwanza kabisa ni kwamba hii sura ni katika sura ambazo zimeteremka mwanzoni kabisa kipindi ambacho mtukufu mtume alikuwa akiwalingania watu kwa siri, na ni sura ya pekee mno ambayo inataja moja kwa moja jina la adui mkubwa wa Uislamu na Mtume kwa ujumla ambaye ni Abuu lahab. Hivyo katika sura hii Mwenyezi Mungu anatuashiria kunako uadui mkubwa ambao alikuwa akiufanya mtu huyu akiambatana na mkewe ili tu kuweza kuisimamisha daawa ya mtume kwa kipindi kile, na mwisho kabisa Quran inaweka wazi kwamba mwisho wa watu hawa ni moto wa Jahanamu kutokana na matendo yao hayo.

Fadhila za kusoma sura hii

Imepokelewa kutoka kwa mtume (saww) akisema "mwenye kusoma sura hii namuombea kwa Mwenyezi Mungu asimuweke pamoja na Abuu lahab”.

Lakini jambo la muhimu hapa ni kwamba fadhila hizi zitamkuta mtu ambaye anaisoma na pia anajikinga kutokana na mienendo ambayo Abuu lahab alikuwa nayo, na si tu kusoma hali ya kuwa unafanya yaleyale ambayo alikuwa akiyafanya kipindi kile.

Sababu ya kushuka sura hii

Amepokea Said bin Jubair kutoka kwa Ibn Abbas kwamba amesema "siku moja mtume (saww) alipanda juu ya mlima wa Safa na kuita kwa sauti ya juu huku akitaka watu wote wamuelekee, walipomwelekea akasema "je nikiwaambia kwamba maadui watawavamia nyakati za usiku au asubuhi mtaniamini au mtanipinga?...” wakamjibu kwa kusema "hatuwezi kukupinga”. Akasema "basi nawapa habari kwamba mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwaonya juu ya adhabu kali..”. baada ya maneno hayo Abuu lahab akasema "hakika umeangamia!, je hili ndilo ambalo umetuitia?!..” na hapo ndipo ambapo Mwenyezi Mungu akateremsha sura hii.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ (1)

(1) Imeangamia mikono ya Abuu lahab na yeye pia amekwishaangamia.

kama tulivyoashiria kwamba sura hii inazungumzia juu ya uadui mkubwa mno kutoka kwa Abuu lahab ambaye pia alikuwa ni mjomba wa mtume (saww) kiasi ambacho mpaka akafikia hatua ya kumwambia Mtume kwamba ameangamia, na kwa ajili ya hilo Mwenyezi Mungu anamjibu kwa kumwambia kwamba kama kuangamia basi wewe Abuu lahab ndiye umeangamia.

Imepokelewa katika riwaya kwamba uadui wa Abuu lahab kwa mtume na kwa Uislamu kwa ujumla haukuwa uadui mdogo, bali ulikuwa umefikia kiasi ambacho hata kama Abuu lahab alikuwa anaumwa hoi hakuweza kuvumilia kukaa kitandani huku Mtume akiendelea kulingania watu, bali alikuwa akimfuata kila kona ambayo alikuwa akienda huku akimwandama kwa maneno mabaya na matusi.

مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ (2)

(2) Hazitamfaa mali zake wala chochote alichokichuma

Kwa maana ya kwamba pamoja na utajiri aliokuwa nao hatoweza kuepukana na maangamio ambayo ni lazima kwake, na hii ni kutokana na kwamba mali zake hizo ndio zinaongeza nafasi ya yeye kuingia katika moto, kwani inaelezwa kwamba alikuwa ni mtumiaji wa mali hizo katika kutaka kusimamisha daawa ya Mtume (saww).

سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ (3)

(3) Ataingia katika moto wenye miale

Na hayo ndio mafikio yake kutokana na matendo yake.

وَامْرَأَتُهُ حَمَّالَةَ الْحَطَبِ (4)

(4) Yeye pamoja na mke wake mbebaji wa kuni.

Aya inaashiria kwamba si Abuu lahab peke yake ndiye ambaye ataingia motoni, bali pia mke wake ataingia. Na hii ni kutokana na kwamba katika watu ambao walikuwa ni washirika wakubwa katika kumtendea maudhi Mtume ni mke wake Abuu lahab, ambaye alijulikana kwa jina la Ummu Jamiil, dada wa Abuu sufiyan, shangazi wa Muawiya. hapa Quran inamtaja kwa sifa ya mbebaji wa kuni ikiwa ni ishara ya moja ya matukio yake ambayo alikuwa akiyafanya, kwani inaelezwa kwamba alikuwa akipenda sana kukusanya kuni ni matawi yenye miba kisha kuja kuweka njiani ili Mtume ashindwe kupita.

فِي جِيدِهَا حَبْلٌ مِنْ مَسَدٍ(5)

(5) Ambaye shingoni mwake kuna kamba iliyosokotwa.

Sifa ya mwisho kabisa ambayo Quran inamsifia mwanamke huyu ni kwamba tayari kamba iliyosokotwa ikiwa na maana ya maangamio tayari ipo katika shingo yake.

Mwisho wa surat Almasad.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: