Falsafa ya mambo kwa mujibu wa Uislamu


Miongoni mwa sifa ambazo dini ya Kiislamu inapambika nazo ni kwamba haikuja kumwamrisha mwanadamu kunako jambo fulani bila ya kumwambia jambo lile lina faida gani, na huku kumwambia kwamba jambo hili lina faida fulani kunaweza kuwa kwa njia moja ya mbili:

1. kubainisha kwa mwanadamu kila kitu na kila sababu kwa vipengele vyake, kiasi ambacho mwanadamu anakuwa hana maswali ya kwanini katika kichwa chake. Mfano mzuri ni pale Uislamu unaposema kwamba nyama ya nguruwe ni haramu kwa sababu tu ina madhara kiafya.

2. Kubainisha kwa mwanadamu kwa njia ya ujumla na bila kuainisha kila kipengele kiasi ambacho kuna uwezekano wa kubakia na maswali katika kichwa cha mwanadamu, lakini kwa kuwa tu jambo lile linatoka kwa mola wake na muumba wake basi hana budi kulikubali. Mfano tunapoambiwa kwamba swala ya asubuhi tuswali rakaa mbili, na adhuhuri rakaa nne, bila shaka tunajiuliza kwanini, ama tunafikia katika natija ya kwamba sisi jukumu letu ni kufanya kama tulivyoambiwa na Mwenyezi Mungu basi.

Kwa hivyo basi ni kwamba kila jambo ambalo lipo katika dini na hata maisha yetu kwa ujumla linakuwa na falsafa na hekima yake, ama swala la kuijua au kutoijua hekima hiyo ni swala lingine kabisa, na ndio maana dini ya Kiislamu inapoona kwamba kuna ulazima wakubainisha hekima ile basi inafanya hivyo.

Kwa mantiki hiyo tumeona kwamba ni jambo zuri sana endapo tutakuwa ni wenye kufahamishana kunako hekima zinazopatikana katika kila jambo ambalo linahusiana na sisi kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, na lazima ieleweke kwamba katika kubainisha hekima na falsafa hizi si kwamba watu wanakaa nakuamua kutaja kutokana na upeo wa akili zao, la hasha, bali ni kwamba watu wanajaribu kurejea katika maneno ya Maasumina (watakatifu) na kuona ni jinsi gani wameelezea hekima hizo kwa maneno yao. Kwa hivyo basi mfumo ambao tutautumia ni mfumo wa kuangalia riwaya na hadithi ambazo zipo katika mfumo wa kuelezea hekima na falsafa za kila kitu ambacho kinatuzunguka katika maisha yetu.

Mlango wa kwanza

Sababu za watu kuabudu asiye Mwenyezi Mungu.

(1) Sababu ya watu kuabudu moto

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Swadiq as kwamba amesema "baada ya moto kuja kutoka mbinguni na kuchukua nadhiri ya Habil, Ibilisi akamfuata Qabil na kumwambia "je unajua kwamba ule ndio moto ambao ndugu yako alikuwa akiuabudu na ndio maana umechukua nadhiri yake pasi na yako?”. Qabil akasema "kama ni hivyo basi sitauabudu moto ambao umeabudiwa na ndugu yangu, na mimi nitaanzisha moto wangu na kuupa nadhiri zangu na nina imani kwamba zitakubaliwa tu.....”.

Basi akaanzisha ujengaji wa nyumba ambazo ndani yake aliweka mioto na kuanza kuiabudu, na huo ndio ukawa mwenendo wake pamoja na kizazi chake kunako swala zima la ibada ya moto.[1]

(2) Sababu ya watu kuabudu masanamu

Imepokelewa kutoka kwa imamu Swadiq (as) kwamba katika kuifasiri kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo ".... na wakasema, msiache miungu yenu humo, na wala msimuache Wadda, wala Suwaa, wala Yaghutha wala Nasra....”[2] amesema " hakika watu wale (wenye hayo majina ya masanamu) walikuwa wanamwabudu Mwenyezi Mungu mtukufu, na hata kizazi chao na watu wao walikuwa pia wanamwabudu Mwenyezi Mungu, lakini baada ya kufariki kwao watu wao walihuzunika sana, na kusema kwanini wamefariki watu ambao ni muhimu sana kwao?. Hapo ndipo Ibilisi alipowajia na kuwapa njia ya kuweza kuondokana na machungu ya kufiwa na watu wale, ndipo alipowaambia kwamba wajenge masanamu ambayo yatakuwa yanafanana na wapendwa wao, na wabakie katika kumwabudu Mwenyezi Mungu, ila wawe wanawaangalia masanamu wale kama njia ya kupunguza machungu yao.

Basi ikaendelea ada hiyo kwa kizazi kile na wakawa bado wanamwabudu Mwenyezi Mungu na huku ndani yao wakiwa na masanamu yale. Mpaka kilipokuja kizazi baada ya kile ambacho hakikuweza kutambua kwamba masanamu yale hayakuwa ya kuabudiwa, bali ni kwa kujikumbusha tu kunako wapendwa wao, ndipo waliposema kwamba mababu zetu walikuwa wanaabudu masanamu haya na sisi hatuna budi kuyaabudu, ndipo ibada hiyo ilipopata nafasi ya kuendelezwa kizazi baada ya kizazi.

Sababu ya watu kuwa bora zaidi ya malaika au duni zaidi ya wanyama

Amepokea Ibn Sinan kwamba siku moja alimuuliza Imamu Sadiq kunako sababu ya mwanadamu kuwa bora zaidi ya malaika au kuwa dhalili zaidi ya mnyama. Imamu akasema "....Imamu Ally alisema kwamba Mwenyezi Mungu aliwaumba malaika na kuwapa akili tu bila ya matamanio, na akawaumba wanyama na kuwapa matamanio tu bila ya akili, lakini alipomuumba mwanadamu akampa akili pamoja na matamanio, kwa hivyo mwenye kuyashinda matamanio yake basi atakuwa ametumia akili yake na hivyo kuwa bora kuliko malaika, na endapo matamanio yake yakaishinda akili yake basi huyo atakuwa ni zaidi ya mnyama.[1] Rejea ilalu sharaii juz 1 mlango wa 2

[2] Surat Nuh aya 23