bayyinaat

Published time: 08 ,October ,2017      10:28:21
Wewe umetuamuru kushuhudia ya kwamba tuamini kuwa ni Mungu mmoja na Wewe ni mjumbe wake, nasi tukashuhudia. Kisha ukatuamuru jihadi, Hijja, funga, Sala na Zaka, nasi tukakubali. Ama yote hayo .........
News ID: 110

Baada ya Mtume (s.a.w.w) kumtawalisha Ali (a.s) katika ghadir khum na yote aliyosema kuhusu yeye kwamba: "Yeyote ambaye mimi ni kiongozi wake, basi Ali pia ni kiongozi wake”. Habari hii ikaenea miji mbalimbali. Siku moja mtu mmoja kwa jina la Malik bin Harith fahriy alimjia Mtume (s.a.w.w) na akamwambia: Wewe umetuamuru kushuhudia ya kwamba tuamini kuwa ni Mungu mmoja na Wewe ni mjumbe wake, nasi tukashuhudia. Kisha ukatuamuru jihadi, Hijja, funga, Sala na Zaka, nasi tukakubali. Ama yote hayo hukuridhika mpaka kumteua kijana huyu kuwa khalifa wako na ukasema yeyote ambaye mimi ni kiongozi wake basi Ali pia ni kiongozi wake.

Je! Hii ni kutoka kwa Mungu au umetunga wewe? Mtume (s.a.w.w) akajibu: Ninaapa kwa Mungu ambaye hakuna mwabudiwa mwingine, hii ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Malik bin Harith fahriy alighadhibika na kuondoka huku akijisemeza mwenyewe: Mwenyezi Mungu! Ikiwa maneno haya ya Muhammad ni kweli, basi jiwe lianguke toka mbinguni na kumudhalilisha mmoja wetu ili iwe ni mazingatio kwa kizazi kijacho, na ikiwa kauli ya Muhammad (s.a.w.w) ni uongo basi mshushie adhabu. Hapo ndipo likashuka jiwe kutoka mbinguni na kupasua kichwa chake na kumuangamiza, na hapo zikashuka Aya hizi:

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ سَأَلَ سَائِلٌ بِعَذَابٍ وَاقِعٍ. لِلْكَافِرِينَ لَيسَ لَهُ دَافِعٌ.

"KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea. Kwa makafiri - ambayo hapana awezaye kuizuia”.[1]

AYA YA 74 YA SURAT TAWBAH.

Baada ya tukio la Ghadir khum na kabla Mtume (s.a.w.w) hajaingia katika mji wa Madina, kundi la wanafiki lilipanga njama za kumuua Mtume (s.a.w.w). mtume (s.a.w.w) akafahamishwa hila zao na akawaumbua na kisha akawauliza, pamoja na kukataa kosa lao na kula viapo: ndipo Mwenyezi Mungu akashusha Aya hizi:

«يحْلِفُونَ بِاللَّهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ وَهَمُّوا بِمَا لَمْ ينَالُوا وَمَا نَقَمُوا إِلَّا أَنْ أَغْنَاهُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ مِنْ فَضْلِهِ فَإِنْ يتُوبُوا يكُ خَيرًا لَهُمْ وَإِنْ يتَوَلَّوْا يعَذِّبْهُمُ اللَّهُ عَذَابًا أَلِيمًا فِي الدُّنْيا وَالْآخِرَةِ وَمَا لَهُمْ فِي الْأَرْضِ مِنْ وَلِي وَلَا نَصِيرٍ».

"Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao wamekwisha sema neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakajihimu kufanya ambayo hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kutokana na fadhila zake. Wakitubu itakuwa kheri kwao, na wakigeuka Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu chungu duniani na Akhera. Na wala hawana katika ardhi mlinzi wala wa kuwanusuru”.[2]

AYA YA 80 YA SURAT AZ-ZUKHRUF.

Baada ya tukio la ghadir mmoja kati ya wanafiki alisema; Ninaapa kwa Mungu kwamba, katu utume na ukhalifa haikusanyiki katika familia moja, hivyo hatutoi khumsi kwa familia hii. Hapo Mwenyezi Mungu akashusha tena Aya hii kwa Mtume wake mtukufu (s.a.w.w):

«أَمْ يحْسَبُونَ أَنَّا لَا نَسْمَعُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُمْ بَلَى وَرُسُلُنَا لَدَيهِمْ يكْتُبُونَ».

"Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika”.[3]

AYA YA 7 YA SURAT AL-MUJADALA.

Baada ya tukio la ghadir khum baadhi ya wanafiki akiwemo Salim, Mughira bin Shu’ba na Abdurahmaan bin A’uf walifunga mkataba wa kupinga azimio la Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na kuandika waraka wa kukataa ukhalifa wa Ali (a.s), na mwandishi wa waraka wa makubaliano hayo alikuwa ni; Abu u’baida bin Jarraah. Mwenyezi Mungu akashusha Aya kudhihirisha mbinu zao:

«أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مَا يكُونُ مِنْ نَجْوَى ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَى مِنْ ذَلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَينَ مَا كَانُوا ثُمَّ ينَبِّئُهُمْ بِمَا عَمِلُوا يوْمَ الْقِيامَةِ إِنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيءٍ عَلِيمٌ».

"Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye huwa ni wanne wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu”.[4]

AYA YA 9 YA SURAT AL-BAQARA.

Baada ya tukio la Ghadir khum na baada ya Abubakr na Omar na baadhi ya wakuu wa Kikuraish kumpongeza Ali (a.s), na wanafiki ili kudhihirisha Nia yao waliazimia kumnyang’anya Ali (a.s) madaraka hayo. Mwenyezi Mungu akashusha wahyi kuashiria kundi hili kwa Mtume wake (s.a.w.w):

«يخَادِعُونَ اللَّهَ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَمَا يخْدَعُونَ إِلَّا أَنْفُسَهُمْ وَمَا يشْعُرُونَ».

"Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui”.[5]

AYA NYINGINE ZA QUR’ANI

Jabir bin Abdilla al-ansariy anasema: Pindi Mtume (s.a.w.w) katika siku ya Ghadir alipotangaza kumtawalisha Ali (a.s), baadhi ya watu walisema: Ni hatua iliyo je! Ya kuinua mkono wa Mwana wa Ami yake juu! Na mwingine akasema; Ni urahisi ulioje! Wa kuinua kazi yake, ninaapa kwa Mungu kutomsikiliza wala kumtii, kisha kwa kiburi wakaondoka mahala pale. Ndipo Mwenyezi Mungu akashusha Aya hii tukufu:

«أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ أَنْ لَنْ يخْرِجَ اللَّهُ أَضْغَانَهُمْ».

"Je! Wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?”.[6]

AYA YA VITISHO KYA WAVUNJA AHADI.

Takriban SIKU tano baada ya tukio la Ghadir khum kundi la watu walikusanyika katika moja ya nyumba ya Sahaba wa Mtume (s.a.w.w) na kuandika mkataba wa makubaliano ya kupinga tukio la Ghadir na kunyang’anya madaraka baada ya Mtume (s.a.w.w). makubaliano hayo baada ya itifaki yao aliyoandika Said bin al-A’as alimkabidhi Abu u’baida ili auweke katika Ka’aba. Abu u’baida alificha barua ile ndani ya Ka’aba. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) baada ya Sala ya Asubuhi na kabla ya kupambazuka aligundua uwepo wa Abu U’baida. Alimueleza haya: Ubarikie sana, ni nani mfano wako. Wewe ni tegemeo la kila mtu katika umma. Kisha akasoma Aya hii:

«فَوَيلٌ لِلَّذِينَ يكْتُبُونَ الْكِتَابَ بِأَيدِيهِمْ ثُمَّ يقُولُونَ هَذَا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ لِيشْتَرُوا بِهِ ثَمَنًا قَلِيلًا فَوَيلٌ لَهُمْ مِمَّا كَتَبَتْ أَيدِيهِمْ وَوَيلٌ لَهُمْ مِمَّا يكْسِبُونَ».

"Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyo andika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayo yachuma”.[7]

Katika maongezi ya Mtume (s.a.w.w) aliashiria njama zao na mbinu zao na akasema; Laiti Mwenyezi Mungu angeteremsha amri kwa watu hawa, basi ningekata shingo zao. Hudhaifa bin Yamaan mmoja katika waumini wa kweli anasema; Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu pindi maongezi ya mtume (s.a.w.w) yalipofikia hapa, wanafiki walitetemeka sana na wote walioshiriki katika hadhira ile wakaelewa madhumuni ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).[8]

Sheikh : Juma. R. Kazingati.[1] Suratul Ma’arij/ 1-2.

[2] Surat at- tawba/ 74.

[3] Surat azzukhruf/ 80.

[4] Suratul Mujaadala/ 7.

[5] Suratul Baqara/ 9.

[6] Surat Muhammad (s.a.w.w)/ 29.

[7] Suratul Baqara/ 79.

[8] Bihar al-anwar, juz 28, uk 102-106.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: