bayyinaat

Published time: 12 ,February ,2017      20:35:41
Jambo la kwanza ni kuweza kutambua kwamba, ni kweli katika Quran kuna aya ambazo zinaelezea juu ya ukamilifu katika uumbaji wa dunia na vilivyomo, lakini isituchukue kusema kwamba aya hizi moja kwa moja zinalenga..........
News ID: 14RAI YA KWANZA

Na hii ni rai ambayo katika kujibu swali hili, inaelezea kwamba ndio katika Quran Mwenyezi Mungu ameelezewa juu ya uwepo wake, kwani aya zote ambazo zinazungumzia maswala ya viumbe na maumbile kwa ujumla zinaelekea au zinamaanisha uwepo wa Mwenyezi Mungu (swt). Mfano ni pale mwenyezi mungu aliposema " hakika yeye ndie ambaye ameumba mbingu saba katika matabaka, kwa hakika hakuna tofauti yoyote katika uumbaji, hebu rudia tena kutazama, je unaona kuna kasoro?”.[1]

Mazingatio:

Ni sawa katika Quran kuna aya nyingi mno ambazo zinaelezea juu ya maumbile ya aina mbalimbali, lakini tunawezaje kusema kwamba aya hizihizi zinatuonyesha uwepo wa Mwenyezi Mungu ambaye sisi ni lazima tumjue?, na swali hili linakuja baada ya kila mmoja wetu kutafakari natija ambayo anaipata baada ya kutafakari yale ambayo Quran inataka sisi tutafakari katika uumbaji wa dunia na vilivyomo, kwani tunakuta kwamba mwisho wa kutafakari kwetu tunafikia katika natija ya kwamba ni kweli uumbaji wa namna kama hii ni lazima kutakuwa na muumbaji, kwani haiwezekani hata mara moja ukapatikana bila ya kuwa na muumbaji, lakini ni nani huyo muumbaji?, hili ni swala la pili ambalo hatulipati katika makusudio ya aya kama hizi, bali itahitajia dalili ya ziada katika kuthibitisha hilo. Sasa je tunasemaje kwamba Quran imeelezea juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu?.

RAI YA PILI

Hii ni rai ambayo katika kujibu swali letu la msingi imeeleza kwamba, Quran kama yenyewe wala haikuja kuelezea swala la uwepo wa mwenyezi mungu (swt), kwani swala la uwepo wake ni swala ambalo kila mmoja wetu analitambua na wala hahitaji kuambiwa au kufundishwa. Ama kuhusiana na aya zote ambazo tunaziona katika Quran kwamba zinaashiria juu ya nidhamu ya uumbaji na ukamilifu wake, basi zipo katika mfumo wa kubainisha kwamba hakuna mwenye kufanya haya yote bali ni mmoja tu, na si wengi kama ambavyo watu wanadhania. Kwa maana kwamba aya hizo zipo katika mfumo wa kupinga ushirikina wa kudhania kwamba kuna washirika mbalimbali katika swala zima la kuanzia uumbaji mpaka uendeshaji.

Hizi ni rai mbili tofauti katika kujibu swali letu ambalo ni muhimu katika swala zima la kumjua Mwenyezi Mungu (swt), lakini pia ipo rai ya tatu ambayo kwa mtazamo wa haraka ndio rai ambayo yenye nguvu zaidi, na hii ni rai ambayo inakuja kutokana na mkusanyiko wa haya yote ambayo wameyataja waliotangulia katika rai mbili za hapo juu.

RAI SAHIHI

Baada ya kupitia rai mbili zilizotolewa katika kujibu swali letu, kuna mambo ambayo endapo tutayakusanya basi tunaweza kupata rai ambayo ndio sahihi na yenye nguvu zaidi.

Jambo la kwanza ni kuweza kutambua kwamba, ni kweli katika Quran kuna aya ambazo zinaelezea juu ya ukamilifu katika uumbaji wa dunia na vilivyomo, lakini isituchukue kusema kwamba aya hizi moja kwa moja zinalenga juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu, bali tuseme kwamba aya hizi zinatuweka katika njia ya kuweza kufikia lengo la kumjua Mwenyezi Mungu, kwa maana ya kwamba hayo ambayo yanatajwa na aya tukufu ni moja ya njia ya kuweza kufikia katika kumjua Mwenyezi Mungu, na si njia kamili katika hilo, kama ambavyo tutabainisha ni kivipi inakuwa ni moja ya njia na si njia kamili.

Tukutane wakati ujao katika mwendelezo wa makala hii.[1] Suratul mulk : aya 3

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: