bayyinaat

Published time: 03 ,December ,2017      18:30:51
Zakaria Razi alisifika sana kwa uhodari na uwezo wake mkubwa wa kihifadhi na kushika mambo mengi kichwani mwake. Ameandika katika kitabu chake alichokipa jina la "Shaka Kuhusu Galinos" (Doubts About Galen) akisema: "Katika ujana wangu nilikuwa na hamu ......
News ID: 142
Muhammad bin Zakaria Razi, Tabibu na Mkemia stadi wa Kiirani
Tarehe 5 Shahrivar inayosadifiana na 26 Agosti ni siku aliyozaliwa Muhammad bin Zakaria Razi, msomi, tabibu na mkemia mkubwa wa Kiislamu na Kiirani katika karne ya tatu Hijria. Razi alizaliwa katika mji wa Rei nchini Iran mwaka 251 Hijria sawa na mwaka 865 Miladia katika zama za utawala wa Wasamani na kipindi cha karne za kati barani Ulaya. Mji wa Rei una historia ya miaka mingi na ulikuwa na wakazi katika kipindi cha zaidi ya miaka elfu tatu kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masiih (as). Baba wa historia ya elimu, George Sarton, anasema: Muhammad Zakaria Razi alikuwa daktari mkubwa zaidi wa Kiislamu katika karne za kati. Naye mtaalamu wa historia ya elimu, Mjerumani Julius Ruska amesema: Zakaria Razi ndiye baba wa elimu ya kemia na mwasisi wa mfumo mpya wa sayansi. 
Uhodari wa Zakaria Razi
Zakaria Razi alisifika sana kwa uhodari na uwezo wake mkubwa wa kihifadhi na kushika mambo mengi kichwani mwake. Ameandika katika kitabu chake alichokipa jina la "Shaka Kuhusu Galinos" (Doubts About Galen) akisema: "Katika ujana wangu nilikuwa na hamu kubwa ya kufanya majaribio ya vitu mbalimbali". Ni hamu hii kubwa ya Razi ndiyo iliyomuelekeza katika elimu ya kemia na kugundua mada iliyobadili chuma cha kawaida na kukifanya chuma chenye thamani kubwa hususan dhahabu. Hata hivyo wakati anafanya kazi na majaribio ya mada za kemikali na karibu na moto, macho ya Razi yalipatwa na madhara. Hivyo aliamua kwenda kwa daktari kutibu macho yake. Gharama ya matibu yake wakati huo ilikuwa karibu dinari mia tano, ambazo zilikuwa fedha nyingi sana kipindi hicho. Wakati alipokuwa akilipa gharama za matibabu, Zakaria Razi alijisemeza mwenyewe kwamba: "Hii ndiyo kemia na si kazi unayoifanya wewe kwa sasa ewe Razi"!
Tangu wakati huo Muhammad Zakaria Razi aliacha elimu ya kemia na kuanza kusoma elimu ya utabibu. Alifanya jitihada kubwa kwa ajili ya kufikia muradi wake. Mtu mmoja aliyeishi na Razi mjini Rei Iran anasema: "Siku zote alitembea na kalamu na karatasi na daima alionekana akiandika". 
Safari ya kujiendeleza kielimu
Razi aliamua kuelekea Baghdad nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu zaidi. Zama hizo mji wa Baghdad ulikuwa na hospitali nyingi, na wanafunzi wa tiba walipata fursa ya kutekeleza kivitendo waliyoyasoma darasani. Katika upande mwingine, utawala wa Baghdad ulitenga kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya madaktari na wasaidizi wao na vilevile kwa ajili ya kutengeneza dawa. 
Razi alikuwa msomi hodari na mwenye bidii. Ameandika katika kitabu chake cha Mwenendo wa Falsafa kwamba: "Nilitumia miaka 15 ya umri wangu kuandika tabu kubwa la  al-Hawi fi al-Tibb hadi nikapatwa na udhaifu katika macho yangu na mshipa wa mkono wangu ukashindwa kufanya kazi na hatimaye nikashindwa kuandika. Hata hivyo sikuacha kufanya jitihada kubwa za kutafuta elimu na niliendelea kusoma na kuandika kwa msaada wa huyu na yule".
Umashuhuri wa Zakaria Razi waenea kimataifa
Razi alipata umashuhuri mkubwa wa kimataifa katika kipindi kifupi kwa kadiri kwamba watawala na wafalme wa zama hizo walianza kumwita na kumwalika. Alikubali wito wao na wakati mwingine kuandikia vitabu kwa majina yao. Miongoni mwa vitabu alivyowaandikia watawala wa zamani hizo ni kile cha  Kitab al-Mansuri fi al-Tibb (Liber Almansoris au Liber Medicinalis) aliporejea Rei kwa wito wa Abu Saleh bin Mansur bin Is'haq wa utawala wa Wasamani na kukubali kuwa mkuu wa hospitali ya mji huo. Kitabu hicho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri zaidi vya Razi barani Ulaya.    
Licha ya uhusiano wake wa karibu na watu wakubwa na watawala wa zama hizo, Muhammad bin Zakaria Razi alikuwa mtu wa watu wa kawaida na alikuwa mwema na mwenye huruma sana kwa watu maskini na wasiojiweza. Mwanahistoria Ibn Nadiim ameandika katika kitabu chake mashuhuri cha al-Fihrist kwamba: "Razi alikuwa mwema na mpole kwa watu wote hususan maskini na wagonjwa wake. Alikuwa akiwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa wake wasiojiweza na kuwatengea kiwango kikubwa cha fedha", mwisho wa kunukuu.
Zakaria Razi ameandika katika kitabu chake cha "Sifa za Hospitali" kwamba: Si kila mtu ana sifa za kuwa tabibu na daktari, na tabibu anapaswa kuwa na sifa makhsusi. Aliwapinga sana watu wenye elimu ndogo waliojiita madaktari na kupiga vita israfu katika utumiaji wa dawa. Alijiepusha sana kumpa dawa mgonjwa kadiri inavyowezekana. Pale ilipolazimu kutoa dawa kwa mgonjwa, tabibu Razi alianza kumpa dawa ya kawaida, na kama haikumfaa mgonjwa alimwandikia na kumpa dawa mchanganyiko. Msomi Razi alikuwa akiamini kwamba: "Tabibu anayeweza kutibu mgonjwa wake kwa kutumia chakula huwa amepata saada na ufanisi".
Siri ya mafanikio ya Zakaria Razi
Muhammad Zakaria Razi alikuwa daktari mvumbuzi na kamwe hakufuata kibubusa matabibu wenzake. Daima alikuwa akitafuta mbinu mpya kwa ajili ya kufaidika zaidi na elimu ya tiba. Katika hospitali yake, tabibu Razi alikuwa amezungukwa na wanafunzi wa wanafunzi wake na wanafunzi wake mwenyewe. Kila mgonjwa aliyekwenda hospitalini hapo kupata matibabu kwanza alipelekwa kwa wanafunzi wa wanafunzi wake. Pale wanafunzi wa wanafunzi wake waliposhindwa kumtibu au kuainisha matatizo yake, mgonjwa alipelekwa kwa wanafunzi wake asili na wakuu. Wanafunzi wakuu wa Razi walimshughulikia mgonjwa na pale waliposhindwa kujua ugonjwa wake, mgonjwa alipelekwa kwa mwalimu, yaani Zakaria Razi. Utaratibu huu ni miongoni mwa kumbukumbu zilizobakishwa na tabibu Razi na zingali zinatumika hadi hii leo katika hospitali nyingi za mafunzo duniani.  


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: