bayyinaat

Published time: 15 ,December ,2017      12:29:29
Mitume wengi wa Mwenyezi Mungu walikumbana na matatizo makubwa katika umati zilizotangulia kwa sababu wengi wao walikuwa wanasifika na sifa ya kujikweza na kujiona, kwa vile sifa hii mwisho wake inapelekea pabaya , walikuwa wakiamua kuwaua (yaani mitume) . na hivyohivyo .............
News ID: 151

MAANA YA KUJIONA NA KUJIKWEZA

Kujiona na kujikweza maana yake takribani ni sawa: Maulama wanasema ni ile hali ambayo inamfanya mwanadamu ajione kuwa yeye ni bora kwasababu anamiliki mali chache au nyingi, au yeye ana cheo kikubwa, au nafasi yake katika jamii ni kubwa,hivyo basi inabidi aheshimiwe, au yeye ana elimu na maarifa makubwa . mara nyingi haya ndiyo yanayosababisha kupatikana sifa hii, ambayo haiko mbali sana na kiburi pamoja na umimi , yaani kwa namna moja ama nyingine hizi sifa zinataka kushabihiana .

Hakika sifa ya kujiona na kujikweza inampelekea mwanadamu kuwa mbali na Mwenyezi Mungu, na kuwa karibu na shetani, na mtu mwenye sifa hii mara nyingi hafanyi jambo lolote kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanasemaje ,bali yeye hufanya jambo lolote kwa kuangalia cheo chake ,au kuangalia jambo lolote miongoni mwa mambo ambayo tumeyaelezea hapo juu, ambayo yanamfanya ajikweze.na mwishowe anabadilika na kuachana na asili yake ya kuwa yeye ni mwanadamu na kuwa shetani kamili . na ndiyo maana kwa taarifu nyingine ya Maulama wanasema kujiona na kujikweza ni ushetani, au mwenye sifa hii ni shetani , wanasema ni kwa sababu anawakilisha sifa halisi ya Shetani . na sisi tunafahamu kwamba miongoni mwa mambo yaliyomtoa Shetani (Ibilisi) katika pepo ya Allah ni kujiona na kujikweza pale alipo ona kwamba yeye ni bora kimaumbile kuliko baba yetu Adam na cheo chake kiko juu kwa vile alikuwa anaishi na malaika , akakataa katakata kumsujudia Adam kwa itibari ya ubora na cheo kama alivyodai .

Mitume wengi wa Mwenyezi Mungu walikumbana na matatizo makubwa katika umati zilizotangulia kwa sababu wengi wao walikuwa wanasifika na sifa ya kujikweza na kujiona, kwa vile sifa hii mwisho wake inapelekea pabaya , walikuwa wakiamua kuwaua (yaani mitume) . na hivyohivyo jamii ambayo imetawaliwa na sifa hii mwisho wake watauana wao kwa wao, kwa sababu ya kujiona na kujikweza, na sifa hizi huzaa hasadi (kumuonea kinyongo mwenzako)na hasadi kama kawaida inapelekea kwenye mauaji ya halaiki(genocide).

KUJIONA NA KUJIKWEZA NDANI YA QUR-AN

Ndani ya Quran kuna zaidi ya aya kumi na mbili ambazo zinakemea sifa hii , baadhi yake ni kama hizi zifuatazo: "watawaita wawaambie: kwani vile hatukuwa pamoja nanyi? watawaambia ndiyo ,lakini mlifitini wenyewe, na mkasitasita, na mkatia shaka wenyewe, na matamanio ya nafsi zenu yakakudanganyeni.mpaka ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu, na mdanganyifu akakudanganyeni msimfuate mwenyezi Mungu"(alhadiid 14) .

katika aya hii tunaona makundi mawili, wale ambao walikuwa ni wema na waja wa Mwenyezi Mungu , na wale ambao walikuwa ni waovu na wenye kujiona na kujikweza hadi walifikiwa na mauti wangali wana sifa hii . na siku ya kiyama watachukuliwa na kuingizwa motoni , na wakati wanapelekwa , lile kundi la watu wema litawaona na kuwaambia hivi nyie hamkuwa nasi katika maisha ya dunia ? lile kundi la watu wa motoni watasema , ndiyo wataambiwa tena , hamkujua kuwa dunia ni shamba na mavuno ni siku ya kiama ? hili kundi la watu wema litaendelea kuwaambia , lakini mlifitini wenyewe , mlikuwa na ladha ya kufanya madhambi wakati huo,na leo mtapata uchungu wa kufanya madhambi , mlijikweza na kujiona na kusitasita na kutilia shaka yale ambayo ameyaamrisha Mwenyezi Mungu, na mkadanganywa na Iblis mpaka amri ya Allah ikawakuta katika hali hiyo , yaani mpaka Mwenyezi Mungu akawafisha bado mkiwa na sifa hii ya kipuuzi na isiyokubalika .

Na sehemu nyingine Mwenyezi mungu anasema : "hayo ni kwasababu walisema,hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu.na yakawadanganya katika dini yao yale ambayo wenyewe waliyo kuwa wakiyazua" . (al-imran 24)

ambao wanajiona na kujikweza , hawawi na sifa hizi mbele ya watu tu , bali wanavuka mipaka na kujikweza hata mbele ya muumba wao, inafikia wakati hawaamini hata moto mkali ambao wameandaliwa wale waovu.

HADITHI AMBAZO ZINAKATAZA KUJIONA NA KUJIKWEZA.

Ali bin Abitwalib(a.s)anasema : "ulevi unaopatikana kutokana na kujikweza na kujiona , unaangamiza haraka kuliko ule ambao unapatikana kwa kunywa pombe" .

Katika hadithi ya Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimwambia ibn Masuud , akisema : ewe mtoto wa Masuud usijikweze mbele ya Mwenyezi Mungu na wala usijikweze kwa yale mazuri unayoyafanya ,wala kwa elimu yako, wala kwa matendo yako , wala kwa wema wako , wala kwa ibada zako .

Na haya mambo ambayo yametajwa katika hadithi , mtu asipokuwa makini , yanaweza kuwa sababu za kujiona , kwa kudanganywa na matendo anayoyafanya , mfano anaweza kutoa sadaka kidogo , kasha akajiona na kujigamba kana kwamba yule ambaye alimpa au anampa sadaka , hawezi kuishi isipokuwa kwa kuwepo yeye . au akajiona kwa ibada zake anazozifanya akadhani kwamba yeye ndiye bora kuliko wote .

Hakika mtu mwenye kujiona na kujikweza , mara nyingi ni yule ambaye anafanya jambo dogo na kulikuza na kulifanya kuwa kubwa , na kujiona , eti yeye ni katika watu wema watakao okoka siku ya kiyama , na kuanzia hapo , mtu wa aina hii anatembea kwa maringo na kujidai , na kutangaza kwa watu kile alichokifanya . au anaweza kufanya jambo ovu , na Mwenyezi Mungu akamfumbia macho mpaka wakati maalumu , lakini yeye anadhani kuachwa wakati ule , bila kuadhibiwa na Allah , kuwa yeye ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu , kwa vile yeye anafanya madhambi na hapati adhabu . kwa ujinga wake hajui kwamba katika hekima ya Mwenyezi Mungu ni kumsubirisha yule aliyefanya dhambi , huenda akatubu muda wowote , na asipotubu hapo lazima Allah amwadhibu , hivyo basi hakuna shaka kwamba watu wenye sifa hizi ni wa motoni , kwani wao ni mashetani , na shetani kwa kiburi chake kamwe hakuwahi kutubu . itaendelea ........

Mwandishi : Alhaj Sheikh Kadhim Abbas


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: