bayyinaat

Published time: 22 ,January ,2018      20:56:17
News ID: 210
ELIMU YAKE
Kielimu Bibi Zaynab AS alikuwa amebobea mno kiasi kwamba, umashuhuri wa elimu yake uliwafanya wanaume na wanawake wa Bani Hashim wampe lakabu ya "Mwanamke Mwenye Hekima." Kwa hakika Zaynab AS alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bi Zainab AS alisimama kidete na kukabiliana barabara na dhulma za watawala madhalimu na majahili wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein AS. Wanawake na mabinti wa Madina walikuwa wakienda katika nyumba ya Zaynab kwa ajili ya kujifunza elimu na maarifa. Zaynab kwa upande wake alikuwa akiitumia fursa hiyo kuwabainisha masuala mbalimbali ya kidini, kijamii na kisiasa. Darsa hizo za elimu ziliendelea pia wakati Bi Zaynab alipokuwa mjini Kufa baada ya baba yake kuelekea katika mji huo. Katika zama hizo wanawake na mabinti waliokuwa na hamu, shauku na raghba ya elimu walimtumia ujumbe Imam Ali AS na kumueleza kwamba, tumesikia kwamba, binti yako Zaynab kama alivyokuwa mtukufu mama yake, ni chemchemi ya elimu na maarifa na ana elimu na ukamilifu. 
Tunaomba uturusu tuje kwake ili tustafidi na chemchemi ya elimu yake. Mwisho wa kunukuu. Imam Ali AS alimruhusu binti yake Zaynab awafundishe wanawake Waislamu wa Kufa na kuwatatulia matatizo yao ya kielimu na kidini. Zaynab kwa upande wake akatangaza kuwa tayari kwa hilo na kwa muktadha huo kukaanzishwa darsa ya tafsiri ya Qur'ani pamoja na darsa ya maswali na majibu ya shubha na mishkili ya kielimu waliokuwa nayo. Upole, huruma na busara zake ziliwavutia mno wanawake wa Kufa hususan tabia na miamala yake na watu. 
BIBI ZAYYNAB MPOKEZI WA HADITHI
Jina la Zaynab AS limepamba pia kurasa za vitabu vya hadithi na wapokezi wa hadithi ambao wanamtaja kuwa mmoja wa wasimulizi na wapokeaji wa hadithi. Kuna riwaya na hadithi zilizopokewa na Bi Zaynab AS ambazo zinapatikana katika vitabu vya hadithi vyenye itibari vya Kishia kama Man la yahdhuruhul faqih, Wasaailus Shiya na Biharul Anwaar. Zaynab amenukuu hadithi hizo baada ya kusikia kutoka kwa baba na mama yake hivyo akawanukulia watu wengine.
 
UCHAJI MUNGU WAKE
Bi Zaynab kama walivyo watu wengine wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW hakuwa nyuma katika masuala ya kiibada, dua na kunong'ona na Mwenyezi Mungu. Alitambulika kuwa mchaji Mungu na mtu aliyezama katika ibada na uchaji Mungu. Alikuwa akiamka nyakati za usiku na kuacha usingizi na kisha kusimama akifanya ibada na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Mbali na Sala za usiku alikuwa akisoma mno kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani Tukufu. Baada ya tukio la Karbala licha ya masaibu, machovu, mateso na taabu alizokabiliana nazo yeye pamoja na watu wengine wa familia ya kaka yake yaani Imam Hussein AS, katu hakusahau au kughafilika kusali Sala za usiku. Imam Sajjad AS anasimulia akisema: Shangazi yangu Zaynab AS alikuwa akisali Sala zake zote za wajibu na mustahabu tukiwa njiani kutoka Kufa tukipelekwa Sham; na baadhi ya wakati alikuwa akitekeleza taklifu hizo za kidini akiwa amekaa kutokana na njaa kali na kudhoofika mwili. Sifa nyingine kubwa ya Bi Zaynab AS ni uvumilivu na subira isiyo ya kawaida aliyokuwa nayo. Aidha aliondokea kuwa mashuhuri kutokana na kuwasaidia wahitaji na wasiojiweza na inaelezwa kwamba, nyumba yake mjini Madina ilikuwa kimbilio la wasio na uwezo na waliokwama katika mambo yao. Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab (a.s) nchini Iran imepewa jina la "Siku ya Wauguzi".
Imeandaliwa na Almuhtaram Salum Bendera.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: