bayyinaat

Published time: 05 ,February ,2018      20:56:29
News ID: 222

Moja ya malengo yaliyopelekea Mwenyezi Mungu (swt) kumuumba mwanadamu bila ya kutenganisha jinsia, ni kuhakikisha kwamba mwanadamu huyu anafikia katika kilele cha juu kabisa cha ukamilifu katika kila nyanja ya maisha yake, mbali na ukamilifu wa maisha yake ni kwamba mwanadamu huyu awe na uwezo wa kufikia yale ambayo Mungu anataka kwa ajili ya maisha yako ya baadaye (akhera).

Lakini sasa swala moja linajitokeza baada ya kufahamu lengo hili, nalo ni kwamba njia gani itumike ili mwanadamu huyu aweze kufikia huo ukamilifu katika maisha ya duniani na ya akhera kwa ujumla?.

Hili ni swali ambalo kila mmoja lazima atajiuliza, hasa ikiwa kweli ana nia ya kuweza kufika katika hayo malengo, wa ila kama hautakuwa na malengo ya kufikia huo ukamilifu basi hautakuwa na haja ya kutafuta njia, bali utafanya kila ambalo linakujia katika fikra zako.

Katika kujibu swali hili kwa mujibu wa maisha ambayo tunaishi katika ulimwengu huu, hakuna njia zaidi ya mbili katika kufikia malengo husika.

Njia ya kwanza ni mwanadamu kuamua kuelekea malengo husika kwa kuamua kupita njia ambayo imewekwa katika  misingi ya kidini na imani zaidi, huku njia ya pili ikiwa ni kufuata na kupita katika njia ambayo imewekwa katika misingi inayopingana na dini.

Katika makala hii sitataka kuelezea ni njia ipi sahihi na ipi si sahihi kwa kumwangalia mwanadamu kama binadamu, bali nitachukua nafasi hii kuzungumza zaidi na kina mama ambao kwa mujibu wa kila mtazamo wa Kidini au Kimaada, wana nafasi kubwa sana katika jamii.

Kwa kuangalia tu kichwa cha habari cha makala hii, utaweza kutambua kwamba nataka kumuelezea mwanamke katika upande gani, bila shaka ni katika upande wa namna gani mwanamke anaweza kufikia ukamilifu wake, ni njia zipi mwanamke apite ili aweze kufikia ukamilifu unaokusudiwa.

Hapa sasa ndio tunarudi katika kujibu swali ambalo tumejiuliza katika Utangulizi wetu, pale tuliposema kwamba hakuna zaidi ya njia mbili katika kufikia malengo husika, ima ufuate njia ambayo imesimamia misingi ya dini, au ambayo imesimamia misingi inayopingana na dini.

Laiti kama swali hili utalichukua na kuwauliza wanawake wa jamii za Kiislamu, basi asilimia kubwa watakujibu kwamba hakuna njia sahihi zaidi ya mwanamke kufuata njia ambayo imewekwa katika misingi ya Kidini, lakini je, ni kipi kinapelekea kuona bado kuna mapingano makubwa baina ya kile wanachoamini na kile ambacho wanakifanyia kazi?, nikiwa na maana kama unaamini kwamba njia iliyojengeka katika misingi ya Kidini ndiyo sahihi, basi huna haja kutenda yale ambayo yanaendana na nadharia yako hii.

Chukulia  mfano wa mwanamke ambaye ana kila ndoto za kufanikiwa katika maisha yake ya dunia na akhera kwa ujumla, ni njia ipi ambayo anatumia?, njia ya kwanza au ya pili?.

Huo ni mfano mdogo tu ambao nimeutoa ikiwa ni kabla ya kubainisha ni njia ipi ambayo ni sahihi kwa ajili ya kufaulu ufaulu ambao Mwenyezi Mungu anautaka.

Sasa twende pamoja katika kuangalia ni njia ipi sahihi ambayo inaweza kumfikisha Mwanamke katika Sharafa ya kweli?, kwa maana nyingine ni njia ipi ambayo inaweza kumfikisha mwanamke huyu katika ukamilifu ambao Mungu anautaka kwake?.

Njia ambayo nimependa kuitumia katika makala hii, ni njia ya kuwasoma baadhi ya wanawake ambao wamefikia katika huo ukamilifu, kwamba wao walipita njia gani mpaka wakafanikisha hilo?.

Fatima Zahraa, Binti yake Mtume Muhammad (saww), ni moja ya wanawake ambao huwezi kukataa kwamba wamefikia ukamilifu wa hali ya juu, wamepata sharafa ambayo mwanamke anapaswa aipate katika maisha yake ya dunia na akhera.

Nimeamua kumchagua mama huyu kutokana na kwamba tupo katika masiku ya kukumbuka masiku ambayo aliaga dunia, wa ila kuna mifano mingi ya wanawake ambao wamefikia ukamilifu na kupata sharafa husika kama itakavyobainika katika makala hii.

Sasa hebu turejee katika maisha ya Bibi Zahraa, je aliendana na njia ipi baina ya njia mbili ambazo tumezitaja katika kufikia malengo husika?, ni njia ya misingi ya kidini, au misingi ya kimaada?.

Kwa ajili ya kuweka wazi zaidi ngoja tusome moja ya matukio muhimu katika maisha yake, pale ambapo alikuwa akitumia muda wake mwingi sana kuwaombea majirani zake, na alipoulizwa na mwanawe kwamba kwanini amekuwa akiwataja sana majirani zake na kuacha kujitaja yeye kama yeye, hakuwa na jibu zaidi ya kusema kwamba "Jirani kwanza kisha wewe mwenyewe”.

Hebu angalia huo msingi, ni mwanadamu gani ambaye anategemea misingi ya kimaada anaweza kukubaliana nao, kwamba jirani yake apate kwanza, kisha yeye ndio apate. Hakuna, maana msingi huu unasimamia katika imani ya kwamba endapo utamwombea  jirani yako jambo fulani, basi Mwenyezi Mungu hawezi kumpa yule kisha wewe akakunyima, kwa hiyo imani inahusika zaidi katika msingi huo.

Mfano mwingine katika maisha ya Bibi Zahraa, ni pale ambapo tunaambiwa hata katika kudai haki zake za halali, hakuwa ni mwenye kujiweka hovyo tofauti na misingi ambayo Mungu anaipenda (Kujisitiri), bali unaambiwa kwamba pamoja na kwamba likuwa na machungu ya kudhulumiwa, bado hakuna ambaye atasimama na kusema kwamba kuna tabia moja mbaya ambayo ilidhihiri katika kudai kwake.

Lakini chukua hali hiyo kisha iweke katika mtazamo wa kimaada, je, Mwanamke mwenye mtazamo huo, anaweza kuyatimiza hayo?, au ndio atasimama kifua mbele bila ya kujali kwamba kuna sharafa yake itapotea katika kusimama kwake huko?.

Hii ni mifano miwili katika maisha ya Bibi Zahraa (AS), lakini kama ulivyosema kwamba shakhsiya za wanawake ambao wamefikia katika sharafa ya juu zipo nyingi ukiachana na Bibi Zahraa (as).

Muangalie Bibi Maryam mama yake Nabii Issa (as), hivi unadhani Mwenyezi Mungu aliamua kumpa nafasi ile ya kuwa mama wa Mtume bila ya vigezo?, chukulia kwamba angekuwa ni mama muovu katika jamii yake, mwenye kusifika na Tabia mbaya na misingi ambayo haiendani na misingi ya Mwenyezi, je bado angetunukiwa nafasi hiyo?.

Bila shaka hapana, bali Mwenyezi Mungu alimwangalia mwanamke huyu kwamba ni wa aina gani kisha ndipo akaja kumpa sharafa ambayo ameipata katika maisha yake ya duniani na hata akhera pia. Na wanawake wengineo ambao nao pia wamefikia katika sharafa ambayo Mungu anaitaka.

Kutokana na mifano hii tunaweza kufikia katika natija ya kwamba, kama mwanamke anatakiwa kufikia katika sharafa ya kweli na ambayo itakuwa ni ya duniani na akhera, basi hana budi kushikamana na njia ambayo misingi yake ni ya Mwenyezi Mungu (swt) tu, kwa maana hao wote ambao wamefikia sharafa hiyo basi wamepita njia hiyo.

Hii ikiwa na maana ya kwamba, mwanamke hawezi pata sharafa ya kweli kwa kujitutumua sehemu ambazo hastahili kufanya hivyo, kuvimba mbele ya ambao hatakiwi kuwavimbia, kuachana na mambo ambayo ameambiwa ashikamane nayo kama vile Hijabu na kujisitiri kwa ujumla.

Lakini kama itakuwa malengo yake yamekomea katika utukufu wa Dunia peke yake, kwamba watu wasimame na kumsifu kwa ushujaa wake wa kurusha maneno na mfano wa mengine ambayo ni katikamambo yasiyo katika misingi ambayo mwanamke anatakiwa ashikamane nayo  (Ikiwa itahesabika ni Utukufu), basi hilo ni chaguo lake binafsi.

     Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal (Abuu Asghar)

 

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: