bayyinaat

Published time: 21 ,February ,2018      22:09:37
News ID: 235

Karibu tena ndugu msomaji wa makala zetu za kila wakati, na wakati huu ningependa kukukaribisha katika mada ambayo nimeipa anuani ya Uislamu na mahusiano ambayo si sahihi, kwa maana ya kwamba tunataka kuangalia namna ambavyo dini ya Kiislamu imejipanga katika kudhibiti mahusiano haya, na kwamba je kuna njia ambazo zimewekwa kama kinga ya tatizo hili, au ni kwamba unangojea mpaka mwanadamu afanye kosa ndipo apewe adhabu ili kuonyesha kwamba jambo hili si sahihi. Karibu sana.

Kwanza kabisa ndugu msomaji ningependa itambulike kuwa jambo la kushiriki mahusiano ambayo si sahihi ni kosa katika dini ya Kiislamu tukufu, hivyo mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu ni kwamba mwenye kujihusisha na mahusiano hayo ni mtu ambaye anatashiki adhabu kutokana kwamba amepinga matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Pili lazima tutambue kwamba Mwenyezi Mungu hayupo tayari kuona kwamba waja wake wanaangamia kwa kutenda makosa, na ndio maana katika dini kuna jambo ambalo linaitwa "Lutful Ilahiya” "لطف الالهية” .Yaani kwamba Mwenyezi Mungu ana mapenzi na wanadamu kiasi ambacho analazimika kufanya mambo ambayo yatamfanya mwanadamu ashikamane na kumtii yeye tu, kama ambavyo yatamfanya aache mara moja kutenda makosa na kumuasi muumba wake. Na ndipo utakuta kwamba Mwenyezi Mungu anatuma Mitume, Vitabu vya kutoka mbinguni, yote hayo ni katika kuhakikisha kwamba huyu mwanadamu anamtii mola wake na hamuasi kamwe.

Baada ya kutambua hayo sasa ndipo tunafikia katika nukta ya mada yetu ya leo, katika kuzungumzia Uislamu na haya mahusiano ambayo si sahihi.

Tunajiuliza kwa pamoja sasa kunako mambo mawili ambayo ni, Je Uislamu ni miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyaweka kwa wanadamu ili tu wasiweze kumuasi?, na je, ni mambo gani ambayo Uislamu umeyaweka ili mwanadamu asishiriki katika mahusiano yasiyo sahihi?.

Kwa kuanza kujibu swali la kwanza tunaweza kusema kwamba jawabu lipo wazi kwa kila mmoja, hasa baada ya kutambua kwamba dini ya Uislamu kwa ujumla ni dini ambayo imekuja kwa lengo la kumfikisha mwanadamu katika ukamilifu wa dunia na akhera yake. Kwa minajili hiyo sidhani kwamba kutakuwa na "Lutfu” "Mapenzi ya Mungu” zaidi ya hayo, hivyo inabainika kwamba Uislamu pia ni katika mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyaleta ili wanaadamu waweze kuwa karibu na kumtii Mungu, kama ambavyo pia wawe mbali na kumuasi.

Ama katika kujibu swali la pili la kwamba je, kuna mambo ambayo yamewekwa na Uislamu ili wanadamu wasishiriki katika mahusiano ambayo si sahihi?, tunaweza kujibu kwa kusema ndio, na kama ambavyo pia tutaorodhesha baadhi ya misingi na mambo yaliyowekwa na Uislamu ili kuhakikisha kwamba wanaadamu wanakuwa mbali na mahusiano ambayo si sahihi.

1. Misingi ya Kiimani

Hapa najaribu kuelezea kwamba kama ambavyo dini ya Kiislamu inaambatana na mwanadamu kimwili na kimaada kwa ujumla, basi pia utakuta inaambatana naye kimaana na kiimani zaidi. Hivyo basi wakati tunazungumzia mambo ambayo Uislamu umeyaweka kwa ajili ya kumuepusha mwanadamu na mahusiano yasiyo sahihi ni lazima tutanue mawazo yetu zaidi, na tusiishie tu katika njia za kimaada bila ya kushirikisha njia za kimaana pia.

Sasa basi miongoni mwa njia za kimaana ambazo Mwenyezi Mungu au dini ya Uislamu kwa ujumla umeziweka ni pamoja na njia inayoambatana na imani ya mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu (swt). Kwa maana ya kwamba mwanadamu anapokuwa na imani juu ya Mwenyezi Mungu, na akajua kwamba kila sehemu atakayokuwepo, au kila jambo atakalolifanya basi Mwenyezi Mungu ni shahidi na anaona, bila shaka hawezi kushiriki katika mambo ambayo tumekubaliana kwamba ni makosa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu katika Quran Tukufu anasema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ

"...Kwa hakika tumemuumba mwanadamu hali ya kuwa tunafahamu yanayomzunguka katika nafsi yake, ila sisi tupo karibu naye zaidi ya mshipa wake wa koo...”[1]

Sasa ikiwa mwanadamu atafikia katika hatua ya kufahamu kwamba Mwenyezi Mungu yu karibu naye zaidi ya viungo vyake mwenyewe, unadhani kuna nafasi tena ya mwanadamu huyo kufanya uasi na kushiriki mambo ambayo yatamchukiza Mungu wake?.

Na jambo la kupendeza zaidi ni kwamba endapo mwanadamu atafikia hali ya juu katika kumuogopa Mungu wake, basi anakuwa hahitaji tena wa kumlinda wala kumuhukumu, bali utamkuta mwenyewe anatambua kosa lake pale anapoteleza na kukosea. Tunaambiwa katika zama za Mtume Muhammad (saww) masahaba walikuwa wakija kwake na kumwambia kunako makosa yao hivyo aweze kuwaambia adhabu zake na kuzitekeleza.

Cha msingi hapa ni kutambua kwamba moja ya mambo ambayo Uislamu umeyaweka ili tu mwanadamu asiweze kukurubia mahusiano ambayo si sahihi, ni hali ya hofu ya kumwogopa Mwenyezi Mungu ambayo imeweka katika nyoyo za wanadamu.

Ungana nami katika sehemu ya pili ya makala hii ili tuweze kufikia katika natija ya mada hii.

Karibu sana.

Sh Abdul Razaq Bilal[1] Surat Qaaf aya 16


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: