bayyinaat

Published time: 21 ,February ,2018      22:14:57
News ID: 236

Karibu ndugu msomaji katika sehemu ya pili na ya mwisho katika kujadili namna ambavyo Uislamu umeweka misingi ya kuweza kujiepusha na mahusiano ambao si sahihi, na ambayo pia yamekatazwa na Mwenyezi Mungu.

1. Utukufu wa Mwanadamu

Miongoni mwa mambo ambayo Uislamu pia umeyaweka katika kumfanya mwanadamu asishiriki katika mahusiano yasiyo sahihi, ni pale ambapo Uislamu umewalingania wanadamu wote kunako kulinda utukufu wa mwanadamu kwa ujumla.

Katika kuelezea hilo Mwenyezi Mungu anasema:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا

"..Kwa hakika tumemtukuza mwanadamu ikiwa ni pamoja na kumpa vipando vya baharini na nchi kavu, na tukamruzuku vitu vingi vizuri vizuri, na tukamfadhilisha juu ya kila kiumbe ambacho tumekiumba”

Huu ni utukufu ambao Mwenyezi Mungu ameuweka kwa mwanadamu, na bila shaka unatakiwa kulindwa siku zote na mwanadamu mwenyewe.

Sasa ikiwa mwanadamu huyu atajua thamani yake mbele ya Mwenyezi Mungu, basi hatokuwa tayari kuona kwamba anaupoteza kwa kushiriki katika mambo ambayo hayafai mbele ya huyo Mungu wake kwa maana atajikuta anajishusha thamani yake na kuwa chini zaidi ya hao viumbe wengine ambao wapo chini ya mwanadamu.

Mtaalamu mmoja kwa jina la Sigmund Freud anasema " Mwanadamu hasa vijana wa kawaida, anaweza kulinda heshima yake na kuepukana na mahusiano ya kijinsia yasiyo salama kwa kutambua thamni yake, kujali afya yake, kutumia wakati wake kwa kufanya mambo yake ya muhimu, kujiepusha na kila mambo ambayo yanaweza kuhemua hisia zake, kujiepusha kutumia mihadarati na pombe. Kama ambavyo mwanadamu baada tu ya kutimiza miaka 20 anatakiwa aanze kuilinda heshima yake....”[1]

Kwa hiyo kumbe jambo la mwanadamu kulinda heshima yake, ni njia sahihi kabisa ya kuepukana na maswala ambayo si sahihi kwa mtazamo wa Dini na Wataalamu wa jamii kwa ujumla. Na ndio maana tunakuta swala hili pia lipo katika Uislamu mtukufu, kwa sababu Uislamu haupingani kamwe na Mitazamo iliyo sahihi.

2. Kuhimiza Ndoa

Jambo lingine ambalo Uislamu umelifanya katika kuhakikisha kwamba mwanadamu anakuwa mbali na mahusiano yasiyo sahihi, ni kuhamasisha wanadamu kunako ndoa, tena si kwa kusema tu kwamba wanadamu wanatakiwa waoe, bali kwa kutumia njia ambazo ni nzuri na za kuvutia kabisa. Angalia baadhi ya njia hizo:

· Ndoa ni Suna ya Mtume (saww)

Leo hii kila mmoja wetu anaona sharafa sana endapo tu atakuwa anajinasibisha na Suna za Mtukufu Mtume Muhammad (saww), kwa maana hakuna jambo ambalo linaweza kumwokoa mwanadamu siku ya kiyama kama kushikamana na mienendo ya Mtume.

Sasa Uislamu unasema kwamba unatakiwa ujue kwamba ndoa pia ni katika mienendo ya Mtume, kwa maana endapo utashikamana nayo basi utakuwa na ufaulu siku ya kiyama. Ndio, kwa sababu ndoa kama itachukuliwa kwa makusudio yake, basi mwanadamu ataepukana na mambo mengi sana katika maisha yake, miongoni mwake ni haya ambayo tunayajadili hapa.

Imamu Ally bin Abi Talib katika kuelezea ndoa na kuwa kwake suna ya Mtume anasema "....Oeni, kwani ndoa ni Suna ya Mtume (saww), na kwa hakika mwenyewe alikuwa akisema " Mwenye kupenda kushikamana na mienendo yangu basi atambue kwamba miongoni mwa mienendo yangu ni ndoa, pia ongezeni watoto, kwani siku ya kiyama nitajifaharisha kwa uma zilizopita...”[2]

Angalia utamu wa njia hii iliyotumiwa na Uislamu, kwa maana ya kwamba mwenye kuielekea ndoa si tu anaielekea kwa ajili ya kuepukana na mahusiano ambayo si sahihi, bali anaielekea ndoa kwa ajili pia ya kushikamana na Suna ya Mtume Muhammad (saww).

· Ndoa ni kuhifadhi dini

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Jaafar Swadiq kutoka kwa babu yake ambaye ni Mtume Muhammad (saww) kwamba amesema:

من تزوج فقد احرز نصف دينه فليتق الله في نصف الباقي

"..Mwenye kuoa basi amemiliki nusu ya dini yake, amche Mwenyezi Mungu katika nusu iliyobaki...”[3]

Kwa maana ya kwamba Mtukufu Mtume Muhammad ameifananisha dini na jambo ambalo linaweza kugawanyika katika nusu mbili, huku nusu moja ikiwa inaweza kufunikwa na ndoa, kama ambavyo nusu nyingine inaweza kufunikwa na kumcha Mwenyezi Mungu. Na hapa ndipo ambapo unaweza kufahamu uzito wa ndoa, mpaka kufikia hatua ya kuwekwa mkabala na kumcha Mungu, ndio, kwa sababu kazi ambayo inafanywa na ucha Mungu, ndio kazi ambayo inafanywa na ndoa, nayo ni kuhakikisha kwamba huyu mwanadamu anakuwa mbali na yale ambayo Mwenyezi Mungu hayataki.

Hii nayo ni njia tamu ambayo Uislamu umeitumia katika kuhamasisha wanadamu kunako jambo la ndoa. Ndoa ambayo ndio itakuja kupambana na mahusiano yote ambayo si sahihi.

· Ubora wa ibada ya mwanandoa

Njia nyingine tamu kabisa ambayo imetumiwa na Uislamu katika kuhamasisha ndoa, ni kuweza kuweka ubora na daraja ya juu katika ibada ya mwanandoa ukilinganisha na ibada ya mseja (bachela).

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Swadiq ambaye amepokea kutoka kwa Imamu Baqir (as) kwamba siku moja alijiwa na mtu, Imamu akamuuliza yule mtu "...Je Una mke wewe?”, yule mtu akajibu "Hapana”, Imamu akasema "....Haipendezi kwamba nikawa na kila kitu katika ulimwengu huu, kisha nikawa usiku nalala hali ya kuwa sina mke..”

Kisha akaongezea kwa kusema "....Rakaa mbili anazoswali Mwanandoa, ni bora kuliko swala za usiku na funga za mchana za mseja (asiye na ndoa)..” Kisha Imamu akatoa pesa na kumpatia yule mtu kwa ajili ya kwenda kuoa.[4]

Pia imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) kwamba amesema "..Rakaa 2 anazoswali mwenye ndoa, ni bora kuliko rakaa sabini za mseja

Hizi zote ni njia za kuweza kuhamasisha wanadamu kunako swala la ndoa kwa mfumo ambao mwanadamu mwenyewe atapenda.

· Maiti ya mseja ni maiti mbaya kabisa

Pia miongoni mwa njia ambazo Uislamu umetumia katika kuhamasisha swala la ndoa, ni kufanya kwamba maiti ya mtu ambaye hakuwa na ndoa ni katika maiti mbaya kabisa.

Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saww) kwamba amesema "...Wabaya na waovu wa maiti zenu ni waseja”.

Hapa kuna jambo lazima tuweke wazi, ili isije kuonekana kwamba Uislamu unatumia njia ya kuwaona watu wasiooa ni waovu na kwamba unawatisha kunako ndoa, hapana, wala sio hivyo, bali hadithi kutoka kwa Mtume inaashiria upande mmoja baina ya pande mbili ambazo zinaweza kupatikana kwa kila ambaye hana ndoa. Upande wa kwanza ni wa mtu ambaye hana ndoa na bado akawa mwema, na upande wa pili ni mtu ambaye hana ndoa na ni mwovu. Upande wa kwanza ni mara chache sana kutokea, kwa maana mwanadamu kama mwanadamu ana hisia zake, sasa anazitibu vipi hizo hisia ikiwa hayupo katika ndoa?, na ndio maana Mtume akasema kwamba maiti ovu ni maiti za ambao hawakuoa, kwa kuangalia kwamba ni maiti ambazo zinakuwa zimefanya mabaya mengi sana ukilinganisha na ambao wameoa na kuelewa maana ya ndoa.

Hizi ni baadhi ya hadithi kutoka kwa Mtume na watu wa nyumba yake tukufu, ambazo zilikuja kwa ajili ya kujibu swali letu la kwamba je, Uislamu umeweka misingi kwa ajili ya kupambana na mahusiano yasiyo sahihi?.

Bila shaka tutakuwa tumefikia katika natija ya kutambua kwamba misingi ipo, tena kwa namna nzuri kabisa.

Tukutane tena katika wakati ujao kwa ajili ya mwendelezo wa makala zetu hizi.

Sh Abdul Razaq Bilal[1] Rejea kitabu cha Sigmund Freud kwa jina la "Mtazamo wa maswala ya kijinsia na athari zake katika jamii” Uk 92

[2] Wasailu Shia Juz 7 Uk 3-4

[3] Wasailu Shia Juz 7 Uk 5

[4] Wasailu Shia Juz 7 Uk 7


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: