bayyinaat

Published time: 02 ,April ,2018      20:53:55
Kwa mfano waweza kulingania watu kwenye dini kwa mantiki na hoja za kielimu, au waweza ukatumia mabavu kuwalazimisha watu kuamini dini wasiyo iamini, hii sana ni pale dini kama hiyo inapokosa hoja za kimantiki za kuwakinaisha watu.
News ID: 287


Fujo ni nini?

Fujo ni kinyume cha upole, na hukusudiwa kwa neno hilo kutumia nguvu au mabavu kwa ajili ya kufikia lengo fulani. Abu Hilal Al-Askariy anasema kwenye kitabu chake AL-FURUUQU LLUGHAWIYYAH:

العنف هو التشديد في التّوصّل الى المطلوب

Fujo ni kutumia mabavu kwa ajili ya kufikia malengo

Kwa mfano waweza kulingania watu kwenye dini kwa mantiki na hoja za kielimu, au waweza ukatumia mabavu kuwalazimisha watu kuamini dini wasiyo iamini, hii sana ni pale dini kama hiyo inapokosa hoja za kimantiki za kuwakinaisha watu. Na haya ndiyo tunayoyashuhudia leo duniani kwa wale wanaojiita Masalafi ambao hawana hoja za kuwakinaisha watu na matokeo yake ni kwamba kikundi hiki mara nyingi hutumia mabavu kulazimisha itikadi zao. Nakumbuka miaka ya nyuma katika baadhi ya misikiti yao walikua wameweka mtu maalum mwenye mkasi ambae kazi yake ilikuwa ni kukata suruali ndefu au kanzu iliyopita nusu ya muundi, yaani wakitaka watu wote wavae kama wao, Kuna haja gani ya kutumia mabavu wakati hili ni jambo linalohitaji hoja na akili.na dini ya Uislamu kama dini iliyojaa mantiki na fikira haihitaji kutumia fujo na vurugu kwa ajili ya kuieneza, kwani Mwenyezi Mungu aliyempa Mtume Muhammad (s.a.w.w) dini hii ili atufikishie sisi wanadamu, wamekataa kuifikisha kwa njia hii (yaani kwa kutumia fujo na vurugu).

Bwana Mtume (saww) anasema:

ان الله رفيق يحبّ الرّفق,و يعطي على الرّفق ما لا يعطي على العنف.............

Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mpole apenda upole, na anatoa kwa mwenye sifa ya kutumia upole, asiyoyatoa kwa mwenye sifa ya kutumia mabavu.

Swahih Muslim j16 Uk.326

Mabavu yana mahala pake na upole una mahala pake, si kila mahala waweza kutumia mabavu. Kuna wakati hekima ina makali kuliko upanga, na kalamu yaweza kuwa na ncha kali kuliko mkuki.

v Fujo sababu na ufumbuzi wake:

Baadhi ya watu wanadhania kuwa tatizo la fujo ni katika matatizo yaliyozuka hivi karibuni katika jamii ya kibinadamu na kwamba hayakuwepo hapo zamani. Hivyo hali hiyo ni katika mambo yaliyozuka katika jamii kutokana na mabadiliko na maendeleo makubwa yalioupitia umma kwa ujumla, haswa baada ya mapinduzi ya viwanda. Na hiyo ni kutokana na kuwepo kizazi kilichokumbwa na taharuki, wasiwasi na kubabaika kutokana na ugumu wa maisha. Aidha kuwepo fujo ni matokeo ya kuwepo hali ya wenye mali na madaraka kuzidi kupanua madaraka yao na kuongeza utajiri wao, wakati mwingine mabavu hutumika kwa malengo hayo, hivyo kuzaa fujo.

Lakini maelezo hayo yaliyotangulia hayana ukweli wote. Kwa sababu tatizo la fujo ni tatizo kongwe mno kabla ya kudhihiri kwa mapinduzi ya viwanda. Ni tatizo kongwe ukongwe wa binadamu mwenyewe.Twaweza kusema kuwa jambo hili lilidhihiri mara ya kwanza pale Qabil alipomuua nduguye Habil, pale walipotoa sadaka ikakubaliwa ya Habil ya Qabil ikakataliwa. Qabil alikasirika akamuua Habil, Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

"Ukininyooshea mkono wako ili uniue mimi sitakunyooshea mkono wangu kukuua, Hakika mimi namuogopa Mwenyeezi Mungu Mola wa walimwengu wote”

Surat Maaidah:28

Kitendo cha Qabil kumuua Habil ilikua ni kitendo cha kutumia mabavu, ni fujo. Lakini Habil alikataa kutumia fujo.

Kila jamii ya kibinadamu inavyobadilika ndivyo na hali ya fujo nayo inavyobadilika, kutoka fujo ya mtu mmoja mmoja hadi kufikia kikundi kimoja kutumia mabavu dhidi ya kikundi kingine, yaweza kuwa ni kikundi cha kabila moja kulishambulia kabila jingine, au dini moja kuishambulia dini nyingine, madhehebu dhidi ya madhehebu au nchi moja kuifanyia uadui nchi nyingine, zote hizo ni aina za fujo ya kikundi.

Quran Tukufu yatueleza namna Mayahudi walivyokua wakiwaua Mitume ya Mwenyezi Mungu (swt), na namna walivyoigeuza Baitul Muqaddas kuwa ni jela ya kuwafungia Mitume na wafuasi wao na kambi ya mateso.

"Hivi kila anapowajieni Mtume na mambo yasiyopendwa na nafsi zenu mnatakabbar kikundi mnakikadhibisha na kikundi mnakiua

Surat Baqarah:87

Katika sehemu nyingine Quran inasema:

"Hilo ni kwa kuwa walikuwa wakizikufuru Aya za Mwenyezi Mungu na wanawaua mitume bila ya haki hivyo ni kwa kuasi kwao na walikua wakichupa mipaka”

Surat Baqarah:61

Imetajwa kwenye vyanzo vya kihistoria kuwa sababu ya kuangamizwa ufalme wa kiyahudi ni jinai yao kubwa ya kutaka kumsulubu Masih Isa bin Maryam (as), lakini Mwenyezi Mungu (swt) akamnusuru Mtume wake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu Ibrahim Al-Khalil (as) alitiwa motoni na watu wa Namrud, Nabii Yahya (as) alipasuliwa kwa msumeno kama mbao vile. Nabii Ismael bin Hizqil (as) walimuua kisha wakamchuna ngozi ya uso wake na kichwa chake.

Hata Mtume wetu Muhammad (saww) hakusalimika na vitendo hivyo vya fujo, mpaka akafikia kusema:

ما أوذي نبيّ مثل ما أوذيت

Hajaudhiwa Mtume yeyote kama nilivyoudhiwa mimi

Mifano yote tuliyoitanguliza ni mifano ya fujo za kikundi si mtu mmoja mmoja, hii si hali nzuri katika jamii, kwani mtu mmoja anapokuwa ni mwovu ni rahisi kumdhibiti. Lakini hali itakuwaje iwapo jamii nzima itakuwa imeharibika na inafanya uovu wa kikundi? Jamii kama hiyo imeharibika na itastahili adhabu kama Wana wa Israil ambao walikua ni jamii ovu, isiyokatazana mabaya ndipo walipostahiki laana ya Mwenyeezi Mungu (swt)……

Itaendelea

Na Sheikh Alhajj Kadhim Abbas


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: