bayyinaat

Published time: 15 ,November ,2018      18:29:55
Kwa hakika maisha ya Maimamu na Ahlul-Beit wa Mtume SAW, yamejaa maarifa na mafunzo kwa ajili ya kumlea mtu na jamii kwa ujumla. Hata hivyo utawala wa kitwaghuti, kidhalimu na halikadhalika
News ID: 359

Tumo katika siku za kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Hassan Askary AS. Siku kama ya leo mwaka 260 Hijiria, ulimwengu ulikumbwa na ghamu na huzuni kubwa ya kuondokewa na Imam Hassan bin Ali bin Muhammad al-Askari AS, ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume SAW.

Kwa hakika maisha ya Maimamu na Ahlul-Beit wa Mtume SAW, yamejaa maarifa na mafunzo kwa ajili ya kumlea mtu na jamii kwa ujumla. Hata hivyo utawala wa kitwaghuti, kidhalimu na halikadhalika kuwepo vizuizi vingi, kulitatiza harakati na shughuli za Ahlul-Beit AS kwa ajili ya kueneza mafundisho asili ya dini Tukufu ya Kiislamu.

Vizuizi hivyo vilishamiri sana katika kipindi cha Imam Jawad na Imam Ali al-Hadi AS na kushtadi zaidi wakati wa kipindi cha Imam Hassan Askari AS. Watawala wa wakati huo wa Bani Abbas, walimlazimisha Imam Ali al-Hadi na mwanawe Imam Hassan aliyekuwa na umri wa miaka minne wakati huo, kuuhama mji wa babu yao, Mtume Muhammad SAW wa Madina na kuelekea mjini Baghdad huko Iraq ambako kulikuwa makao makuu ya watawala hao.

Baada ya kufariki dunia Imam Hadi AS Imam Hassan Askari AS alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu huku akiwa na umri wa miaka 22. Katika mazingira hayo magumu, mtukufu huyo aliweza kufikisha ujumbe wa mafundisho ya Kiislamu katika nyanja tofauti zikiwemo za kisiasa na kijamii kwa wanafunzi wake. Hata hivyo vikwazo na vizingiti vya aina mbalimbali vilivyowekwa na watalawa wa Bani Abbas, havikuweza kuzuia upendo wa watu kwa Imam Askari AS. Hali hiyo inaonyesha kuwa, nuru ya Mtume Muhammad SAW na Ahlul-Beit wake AS, ni nuru ya haki ambayo kamwe haiwezi kuzimwa.

Zama za Imam Hassan Askari AS zilikuwa zenye misukosuko mikubwa zaidi kwa watawala wa Bani Abbas. Uongozi usiofaa, migogoro ya ndani ya utawala, upinzani wa wananchi, harakati za mara kwa mara dhidi ya watawala na kuenea mafundisho potofu, ni miongoni mwa sababu za machafuko ya kisiasa na kijamii ya kipindi hicho.

Viongozi walikuwa wakiwanyonya na kuwakandamiza raia, huku wakijenga makasri na majumba makubwa ya kifahari na kuwaacha watu wa kawaida katika hali ngumu ya kimaisha. Viongozi hao madhalimu hawakujali umasikini na tabu za raia bali waliendelea kujineemesha katika utawala. Hali hiyo, ilizidisha vizingiti na ukandamizaji wa watawala dhidi ya Imam kiasi kwamba, ilimlazimu mtukufu huyo chini ya mpango ulioandaliwa na utawala, kuripoti katika siku maalumu za wiki katika ofisi za watawala wa wakati huo.

Hata hivyo na licha ya kuweko njama kubwa za watawala hao, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mapenzi na utukufu Wake, aliamua mtoto wa Imam Askari, yaani Imam Mahdi AS ambaye ni mwokozi wa ulimwengu, azaliwe salama salimini. Baada ya kuzaliwa Imam Mahdi AS, Imam Hassan alianza kuiandaa jamii ya wakati huo kukabiliana na hali ngumu itakayoikabili jamii ya baadaye.

Kila alipokuwa akipata fursa, Imam Hassan al-Askari alikuwa akitumia fursa hiyo kuzungumzia hali ya baadaye atakayokuwa nayo Imam Mahdi AS yaani ya ghaiba na kutoweka mbele ya upeo wa macho ya watu pamoja na taathira chanya za uongozi wa mwanawe Imam Mahdi AS kwa walimwengu…

Itaendelea

Na Salum Bendera


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: