bayyinaat

Published time: 15 ,November ,2018      18:32:40
News ID: 360


Tarehe 8 mwezi wa Rabiul Awwal (Mfungo sita), ulimwengu mzima unaingia katika majonzi na masikitiko kunako kifo cha Imamu wa 11 katika maimamu 12 ambao tumeachiwa na Bwana Mtume (saww).

Hapa namzungumzia Imamu Hassan Al askariy (as), Imamu ambaye ndiye baba wa imamu Al Mahdi (atfs) ambaye ulimwengu mzima upo katika kumsubiri yeye ili aweze kueneza nuru na uadilifu kama ambavyo giza na dhulma vimeenea kwa sasa.

Katika uwanja huu tutajaribu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kumzungumzia japo kwa kifupi Imamu huyu, mpaka kufikia sababu ya kuondoka kwake duniani na kurejea kwa mola wake huku akiwa ni mwenye kuridhiwa.

Jina na Nasaba yake:

Ni Imamu Abuu Muhammad Hassan bin Ally bin Muhammad bin Ally bin Mussa bin Jaafar bin Muhammad bin Ally bin Hussein bin Ally bin Abi Twalib (as).

Alikuwa maarufu kwa baadhi ya majina kama vile Al Askariy, AL Siraj, Al Khalis, Al Swamit, Al Taqee, Al Zakiy. Ila jina la Al Askariy limeonekana kuwa maarufu sana kwake.

Tarehe ya kuzaliwa kwake:

8 Rabiul Thani mwaka 232 H, Madina.

Mama yake ni Sayida Sausan ambaye ni kijakazi kutokea katika nchi ya Morocco, na kuna riwaya ambazo zinasema kuwa jina la mama yake ni Hadith ambaye pia alikuwa ni kijakazi.

Mke wake Imamu pia alikuwa akiitwa Narjis mtoto wa Yashu bin Qaisar Al Rum, ambaye pia alikuwa ni kijakazi.

Ibada yake:

Kama ilivyo kwa maimamu wote kuwa wao ni kigezo chema kwa waja katika swala zima la kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu, ndivyo ambavyo ilikuwa kwa Imamu Hassan Al Askariy pia.

Inapokelewa katika riwaya kwamba baada ya Imamu kuwekwa kifungoni, alikabidhiwa watu wawili maarufu kwa ajili ya kumuudhi tu na kumuweka mbali na Mungu wake, lakini mwisho wa siku watu wale waliangukia kuwa pamoja na Imamu na kuwa ni miongoni mwa wanafunzi bora wa Imamu. Walipokuja kuulizwa kunako sababu ya kubadilika kwao na kuhusu imamu kwa ujumla walisema ".....Tuseme nini kunako mtu ambaye mchana hufunga, na usiku husimama kwa ibada, na hakuna muda ambao anaachana na ibada, ikafikia wakati akituangalia tunahisi kutetemeka na kuingiwa na ambayo hayajawahi kutuingia katika nafsi zetu....”[1]

Hii ni moja ya mifano ya kuonyesha namna ambavyo Imamu alikuwa na kila njia ya kuweza kuathiri na kuwavuta karibu hata maadui zake kwa kutumia Ibada yake tu.

Utukufu wake:

Linapokuja swala la utukufu wa waja wa Mwenyezi Mungu basi kuna mambo mawili ambayo tunaweza kuyazungumzia, kwanza ni pale ambapo mja anakuwa mtukufu mbele ya mola wake, na pili ni pale ambapo mja anakuwa mtukufu mbele ya mola wake pamoja na waja wenzake.

Ukirejea maisha ya Imamu Askariy utakuta kwamba mbali ya kuwa Mwenyezi Mungu ameshawafanya kuwa ni watukufu, bado unakuta pia mbele ya waja ni watukufu, tena la kushangaza ni pale ambapo unakuta hata maadui zake walikuwa mstari wa mbele katika kukiri utukufu wao.

Ahmad bin Ubaidullah bin Khaqan moja ya maadui wakubwa wa Imamu anamsifu kwa kusema "....Sijawahi ona wala sikia katika mji wa Samarra mtu kutokea ukoo wa Ally mfano wa Hassan bin Ally bin Muhammad bin Ally, kuanzia utulivu wake, kujihifadhi kwake, karama zake, na hata katika swala zima la kutangulizwa na waliomzidi umri mpaka mawaziri kwa ujumla.....”

Itaendelea........[1] Sharhu Ihqaqul haq Juz 29 Uk 68


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: