bayyinaat

Published time: 15 ,November ,2018      18:46:41
News ID: 362

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, vita vya sasa duniani ni "Vita vya Irada" na kusisitiza kuwa, kwa harakati yao yenye thamani, wanamichezo majeruhi wa vita na walemavu, wameonyesha kuwa wana uwezo, wanajitegemea kiutamaduni na wana irada imara. Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, ameyasema hayo leo asubuhi mbele ya hadhara ya msafara wa wanamichezo wa Iran waliotwaa medali na washindi wa michezo ya Parasia 2018 iliyofanyika nchini Indonesia. Amewaenzi wanamichezo hao majeruhi wa vita na walemavu waliotwaa ushindi na kuliletea taifa heshima na fahari na kueleza kwamba, ushindi huo ni dhihirisho la azma thabiti na kuufanyia kazi uwezo na vipawa vilivyofichika. Ayatullah Khamenei amesema, moyo wa kujiamini walionao wanamichezo majeruhi wa vita na walemavu na hasa wanamichezo wa kike, katika kulinda thamani na tunu zao za kidini na kitaifa ni hatua muhimu sana na ya kupongezwa na akaongezea kwa kusema: Kubebwa bendera ya msafara wa wanamichezo wa Iran na mwanamama aliyevaa hijabu aina ya Chador (buibui la Kiirani), kusimamisha Sala kwa sura ya jamaa na kuhudhuria Sala ya Ijumaa, maana yake ni kusimama imara kwa pamoja kukabiliana na hujuma za mienendo ya maingiliano holela na yasiyo na mipaka ya kijinsia inayozidi kuongezeka duniani na kutosalimu amri mbele ya hujuma hizo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewahutubu wanamichezo hao: Katika hali ambayo, baadhi ya watu wanaoshiriki kwenye medani za kimataifa wanashindwa kusimama kukabiliana na hujuma za matarajio yasiyo na kikomo ya kambi ya ukafiri na uistikbari na kuamua kulegeza misimamo, nyinyi mumesimama imara; na kwa "kuonyesha nguvu za kiutamaduni" mumeilinda hijabu na staha yenu pamoja na vazi lenu la kitaifa na kidini. Kwa sababu hiyo, ninatoa shukurani zangu za dhati na za moyoni kwa msafara wa wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa, moja ya nukta zenye mafunzo katika ushindi na ubingwa waliopata wanamichezo majeruhi wa vita na walemavu ni kutumia uwezo na vipawa vilivyofichika katika nafsi ya mwanadamu na kufafanua kwamba: Ikiwa uwezo na vipawa vya taifa vitatumiwa kwa usahihi, matatizo ya kiuchumi yatatatuka. Msafara wa wanamichezo wa Iran walioshiriki kwenye Michezo ya Tatu ya mashindano ya Parasia 2018 yaliyofanyika nchini Indonesia umejinyakulia jumla ya medali 136, zikiwemo 51 za dhahabu, 42 za fedha na 43 za shaba na kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: