bayyinaat

Published time: 19 ,December ,2018      19:18:05
Imamu akawauliza: “...Je, endapo nitawajuza jambo na kuwaelewesha, mnaweza kwenda kumueleza na kumjuza pia?”. Wanafunzi wakajibu kwa kusema “...Ndio tutafanya hivyo”.
News ID: 377

Lakini jambo ambalo tunaweza kujifunza katika kipindi hichi cha Imamu Askariy, ni namna gani aliweza kuamiliana na watawala madhalimu mpaka kufikia lengo lake kubwa nalo ni kumuhifadhi mkombozi wa ulimwengu.

Historia inatuambia kwamba Imamu hakuwa ni mwenye kudhihirisha moja kwa moja misimamo yake kunako tawala hizo dhalimu, hakuwa ni mwenye kuwapinga hadharani, ili kuepuka madhara makubwa, wala hakuwa ni mwenye kuwakubali kwa siri asije akawachanganya wafuasi wake kunako uhalali na usahihi ni upi. Bali badala yake tunakuta kwamba Imamu Askari alitumia muda mwingi mno kuwafundisha wafuasi wake misimamo sahihi kama ambavyo pia aliwaonyesha mambo ambayo si sahihi katika dini ya Kiislamu. Na kutokana na hilo unakuta kwamba Imamu Askari alikuwa akikubalika na pande zote mbili, upande wa wafuasi wake ambao walikuwa wakijua usahihi na haki yake katika Uislamu, na pia upande wa madhalimu ambao hata kama walikuwa hawataki kuonyesha ukubali wao kunako nafasi yake, lakini kwa kuwa waliona si mwenye kupingana na misimamo yao basi hakuna haja ya kutomuheshimu kwa hilo, kifupi ni kwamba Imamu alipendwa na wote. Na kutokana na heshima hiyo aliweza kuwafunza wafuasi hata maadui pia kwa njia mbalimbali ambazo zilikuwa zikijitokeza, na wakati mwingine hata mbele ya hao watawala bado utakuta imamu alikuwa akitimiza jukumu lake la kuwaongoa watu.

1. Zama za kupambana na shubuha za upinzani

Hiki ni kipindi cha pili katika vipindi muhimu ambavyo Imamu Askari alipitia katika maisha yake, nacho ni kipindi cha kuhakikisha kwamba anakabiliana na kila aina ya shubuha na mkanganyiko ambao unaweza kuonekana katika mafundisho ya Uislamu. Wakati mwingine mikanganyiko hii inakuja kutokana na upungufu wa maarifa, kama ambayo pia wakati mwingine inakuwa ni kutokana na upingaji wa wapingaji hata kama watakuwa wanajua uhakika wa mambo, Imamu hakuweza kutofautisha bali alijibu kwa kila shubuha kwa nafasi yake.

Katika kuelezea kipindi au zama hii, tuangalie moja ya matukio maarufu kutokea katika zama za Imamu, nalo ni tukio la mjadala kwa njia isiyo mubashara baina ya Imamu na Abuu Ishaq Al Kindiy, moja ya maulama na wanafalsafa wakubwa wa Iraq, mwanafalsafa huyu alikuwa muda mrefu sana akijiandaa kuandika kitabu ambacho alilenga ndani yake kuelezea namna ambavyo Quran inapingana yenyewe kwa yenyewe (Tanaqudh) (Contradiction).

Siku moja kundi la wanafunzi wake wakafunga safari na kwenda kwa Imamu Askari kwa ajili ya baadhi ya mambo, na walipoingia tu Imamu aliwagundua na kisha akatamka maneno yafuatayo:

".....Ina maana katika nyinyi hakuna mjuzi na mwenye ushujaa wa kujibu shubuha za mwalimu wenu (akimaanisha Al Kindiy)?..”. Wale wanafunzi wakasema: "....Sisi sote ni wanafunzi wake, na si vyema kupingana na mwalimu wetu katika jambo au mambo asemayo”.

Imamu akawauliza: "...Je, endapo nitawajuza jambo na kuwaelewesha, mnaweza kwenda kumueleza na kumjuza pia?”. Wanafunzi wakajibu kwa kusema "...Ndio tutafanya hivyo”.

Itaendelea.....
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: